1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ocampo ataka viongozi wa ngazi za juu Sudan wakamatwe

Bruce Amani16 Desemba 2011

Mwendeshaji mkuu wa mashtaka katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu, Louis Moreno Ocampo, amesema maafisa wakuu Sudan wanaokabiliwa na kesi katika mahakama ya ICC, wanendelea kusababisha mauaji ya halaiki Darfur.

https://p.dw.com/p/13U3B
Rais wa Sudan Omar Al Bashir na mwendesha mkuu wa mashtaka wa ICC Luis Moreno Ocampo
Rais wa Sudan Omar Al Bashir na mwendesha mashtaka wa ICC Luis Moreno OcampoPicha: AP/Montage DW

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita, ICC, imetoa vibali vya kukamatwa rais Omar Al Bashir kwa tuhuma za mauaji ya halaiki pamoja na aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani, Ahmed Haroun, na kiongozi wa kundi la wanagmabo la Janjaweed, Ali Kushay, kwa uhalifu wa kivita katika jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan.

Kiongozi wa mashtaka Luis Moreno Ocampo hivi majuzi aliwaomba majaji wa mahakama hiyo kutoa waranti wa kumkamata waziri wa ulinzi, Abdelrahim Mohamed Hussein, kuhusiana na Darfur. Akilihutubia baraza la usalama la umoja wa mataifa, Moreno Ocampo alisema ni muhimu kwa maafisa hao wote wanaokabiliwa na mashtaka kwa sababu wanaendelea kusababisha uhalifu mkubwa katika jimbo la Darfur.

Pia aliliambia baraza hilo kuwa nchi mwanachama wa mahakama ya ICC, Malawi, ilikosa kutimiza jukumu lake kwa kushindwa kumkamata Bashir wakati alipoizuru nchi hiyo. Kenya pia ilishindwa kumkamata Bashir wakati alipoitembelea nchi hiyo mwaka jana, lakini mahakama moja mjini Nairobi ilitoa uamuzi hivi majuzi kuwa serikali ni sharti imkamate rais huyo wa Sudan, ikiwa atazuru nchini humo tena.

Balozi wa Sudan katika umoja wa mataifa, Daffa Alla Elhag Ali Osman, amemshtumu vikali Ocampo kuhusiana na swala hilo la Darfur, akisema kuwa ombi lake la hivi karibuni la kufunguliwa mashtaka waziri wa ulinzi liliibua maswali mengi ya kisheria. Alimshtumu kiongozi huyo wa mashtaka kwa kuibagua serikali ya Sudan.

Naye Ocampo anasema serikali ya Sudan imekataa kushirikiana naye katika uchunguzi wake. Sudan siyo mwanachama wa mahakama ya ICC na haiitambui. Lakini baraza la usalama la umoja wa mataifa liliiwasilisha kesi ya Drafur kwa mahakama hiyo mnamo mwaka 2006, na kufanya ushirikiano wa sudan katika swala hilo kuwa la lazima.

Wakati huo huo baraza la usalama limekubaliana kwa kauli moja kupanua jukumu la wanajeshi 4,000 wa Ethiopia walioko katika jimbo la Abyei, wanaojulikana kama UNISFA, ili kusaidia Sudan na Sudan Kusini kushika doria katika eneo hilo la mzozo.

Mwendesha mashtaka wa ICC Luis Moreno Ocampo, kulia, na kaimu waziri wa haki nchini Libya Mohammed al-Alagi, kushoto, akiwasili Tripoli
Mwendesha mashtaka wa ICC Luis Moreno Ocampo, kulia, na kaimu waziri wa haki nchini Libya Mohammed al-Alagi, kushoto, huku akiwasili TripoliPicha: dapd

Kwingineko Moreno Ocampo amesema kuwa kifo cha aliyekuwa rais wa Libya, Muammar Gaddafi, aliyekamatwa na kisha kuuwawa na waasi mwezi Oktoba huenda ulikuwa uhalifu wa kivita. Amesema wanalizungumzia swala hilo na mamlaka husika na wanatayarisha mpango wa kuwa na mkakati mathubuti wa kuchunguza uhalifu huo wote. Kutokana na shinikizo kutoka kwa washirika wake wa magharibi, baraza la mpito la Libya limeahidi kuchunguza jinsi Gaddafi na mwanawe wa kiume, Motassim, walivyouwawa.

Mwanawe mwengine Gaddafi, Saif Al-Islam sasa yuko kizuizini nchini humo na Libya inapanga kumfungulia mashtaka nchini humo badala ya kumkabidhi katika mahakama ya ICC mjini the Hague. Ocampo pia amesema kuwa anachunguza madai kuwa wanajeshi waliompinga Gaddafi na NATO pia walihusika katika uhalifu wa kivita.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters

Mhariri: Miraji Othman