1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Odinga apinga tarehe ya kurudiwa uchaguzi

John Juma
5 Septemba 2017

Odinga amesema kuwa ni sharti hatua za kisheria na kikatiba zitimizwe kabla uchaguzi huo kufanyika. Amependekeza uchaguzi huo urudiwe tarehe 24 au 31 Oktoba wala si tarehe 17 Oktoba jinsi IEBC ilivyotangaza

https://p.dw.com/p/2jMqL
Kenia nach der Annulierung der Präsidentenwahl | Raila Odinga
Picha: picture alliance/AP Photo/B. Curtis

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amesema muungano wa NASA anaouwakilisha hautashiriki katika marudio ya uchaguzi wa rais ambao umeratibiwa kufanyika tarehe 17 Oktoba.

Odinga amesema kuwa ni sharti hatua za kisheria na kikatiba zitimizwe kabla uchaguzi huo kufanyika. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Nairobi, Raila ameongeza kuwa "Huwezi kufanya makosa mara mbili na utarajie kupata majibu tofauti."

Masharti ya Odinga

Baadhi ya masharti ambayo Odinga ameweka ni pamoja na kufutwa kazi kwa baadhi ya maafisa wa tume inayosimamia uchaguzi Kenya, kutathminiwa kwa mitambo ya kuwasilisha matokeo ya uchaguzi kutoka vituo vya kupiga kura na kwamba wagombea wengine wote wanane walioshiriki kwenye uchaguzi huo waruhusiwe kuwania tena kwenye marudio.

Majaji wa Mahakama ya Juu Kenya
Majaji wa Mahakama ya Juu KenyaPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Azim

Odinga ambaye amesema tume ya IEBC haikushauriana na muungano wake wa NASA kabla ya kutangaza tarehe ya kurudiwa kwa uchaguzi, amependekeza uchaguzi huo urudiwe tarehe 24 au 31 Oktoba, baada ya kutimizwa kwa masharti ambayo wametoa.

Jumatatu wiki hii, tume huru ya  inayosimamia uchaguzi na mipaka nchini Kenya- IEBC ,ilitangaza kuwa marudio ya uchaguzi yatafanyika tarehe 17 Oktoba. Kulingana na taarifa rasmi iliyowasilishwa kwa vyombo vya habari, mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati alisema kuwa ni wagombea wawili pekee watakaoshiriki uchaguzi huo- Uhuru Kenyatta wa Jubilee na Raila Odinga wa NASA.

Uamuzi wa Kihistoria

Ijumaa wiki iliyopita, Mahakama ya Juu nchini humo iliyafuta matokeo ya uchaguzi ambayo yalimpa Rais Uhuru Kenyatta ushindi. Mahakama hiyo ilisema kuwa uchaguzi wa urais ulikumbwa na makosa ya taratibu za kikatiba na kanuni zilizohitajika hazikufuatwa kikamilifu. Majaji wa mahakama hiyo walioongozwa na Jaji Mkuu David Maraga, waliamuru uchaguzi huo ufanywe upya ndani ya siku 60.

Rais Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru KenyattaPicha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Kenya na barani Afrika kwa jumla ambapo ushindi wa rais katika uchaguzi umebatilishwa.

Rais Kenyatta alisema anaheshimu uamuzi wa mahakama japo hakubaliani nao. Hata hivyo amekuwa akiwakosoa vikali majaji wa mahakama kwa kile anachosema kuwa kila mara, majaji huhujumu baadhi ya juhudi za serikali. Akiwaita majaji ‘wakora‘ Uhuru Kenyatta ameahidi kuifanyia mageuzi mahakama siku za baadaye.

Hata hivyo matamshi ya Kenyatta yamekosolewa vikali na baadhi ya viongozi na asasi za kijamii kuwa ni vitisho dhidi ya demokrasia na uhuru wa mahakama.

Odinga amewania urais mara tatu na kushindwa. Kila mara alidai uchaguzi ulichakachuliwa dhidi yake.

Mwandishi: John Juma/RTRE/AFPE/

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman