1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Olimpiki: Brazil yavuna dhahabu katika soka

21 Agosti 2016

Kwa kuubusu mpira na bao ambalo halitasahaulika, nyota mkubwa wa Brazil Neymar aliwapa wenyeji wa mashindano ya Olimpiki muda ambao hautasahaulika katika mashindano haya.

https://p.dw.com/p/1JmN2
Olympia Rio 16 20 08 Fußball Deutschland Brasilien Finale
Kikosi cha timu ya taifa ya Brazil na medali za dhahabuPicha: picture-alliance/dpa/F. Gentsch

Brazil ilishinda medali ya dhahabu ya olimpiki katika soka jana Jumamosi (20.08.2016) kwa mikwaju ya penalti na kuishinda Ujerumani, ikiwa ni ushindi wake wa kwanza katika historia ya olimpiki na kuzusha hali ya furaha kubwa katika taifa hilo baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na kisha kupigiana penalti ambapo Brazil ilishinda kwa mikwaju 5-4.

Olympia Rio 16 20 08 Fußball Deutschland Brasilien Finale
Brazil ikipambana na Ujerumani katika fainali ya olimpiki 2016Picha: euters/M. Brindicci

Kabla ya mkwaju wa mwisho wa penalti kwa Brazil, Neymar aliuchukua mpira na kuubusu na kuuweka katika alama ya penalti.

Kwa kusita kwanza, na kisha mkwaju safi, kwa utulivu aliuelekeza mkwaju wake wavuni na kisha alipiga magoti kabla ya kuvamiwa na wenzake kwa furaha.

Waandika historia

"Imekuwa" alisema Neymar. " Tumeandika historia."

Olympia Rio 16 20 08 Fußball Deutschland Brasilien Finale
Pambano kati ya Brazil na UjerumaniPicha: Reuters/L. Foeger

Ulikuwa ushindi ambao ni zaidi ya soka kwa taifa hilo, ambalo lilikuwa linahitaji mno kitu cha kusherehekea. Brazil imevurugwa na mdororo wa uchumi, kashfa za kisiasa, matatizo ya kiafya kuhusiana uchafuzi wa maji na virusi vya Zika na maswali kuhusiana na iwapo itaweza kuwa mwenyeji wa michezo ya olimpiki.

Matatizo yote hayo yalisahaulika wakati mkwaju wa Neymar ulipotinga wavuni.

Olympia Rio 16 20 08 Fußball Deutschland Brasilien Finale
Neymar akipiga mkwaju wake wa penalti ulioleta furaha kwa BrazilPicha: Reuters/M. Brindicci

Sherehe kubwa zilizuka katika mji wa Rio, ikiwa ni karibu na sherehe zilizofanyika kufuatia vikombe vitano vilivyonyakuliwa na Brazil katika kombe la dunia katika taifa hilo lenye wazimu wa soka.

Fashifashi zilionekana angani kuzunguka uwanja wa Maracana , honi za magari zilisikika na mashabiki waliimba na kupongezana na kumwagiana bia.

Wakati timu hiyo iliposimama katika jukwaa la kukabidhi medali , huku medali za dhahabu zikining'inia shingoni mwao , machozi yalibubujika katika nyuso za Wabrazil wakati uwanja wa Maracana ukihanikiza sauti za mashabiki wakiimba wimbo wa taifa.

Olympia Rio 16 20 08 Fußball Deutschland Brasilien Finale Jubel
Neymar akipiga magoti baada ya kuipatia ushindi BrazilPicha: Reuters/M. Sezer

Ushindi huo unakuja miaka miwili baada ya kipigo cha kudhalilisha cha mabao 7-1 nyumbani dhidi ya Ujerumani katika timu ya wakubwa katika nusu fainali ya kombe la dunia.

Brazil pia ilikuwa inajitoa kutoka katika kutolewa na mapema katika awamu ya makundi ya kombe la mwaka huu la mataifa ya bara la America, Copa America, na ilikuwa katika hali isiyokuwa na uhakika katika duru za mwanzo za kombe la Olimpiki.

Olympia Rio 16 20 08 Fußball Deutschland Brasilien Finale Jubel
Wachezaji wa Brazil wakishangiriaPicha: Getty Images/C. Mason

Shoo ya Mo Farah

Kwa upande wa mbio, Mo Farah, wa Uingereza anakuwa mtu wa pili pekee kunyakua medali ya dhahabu ya mbio za mita 5,000 mara mbili mfululizo katika Olimpiki.

Farah alianza kuongoza muda mfupi baada ya nusu ya kwanza kumalizika na kupambana na changamoto waliyokuwa wakimpa wakimbiaji wengine na kumaliza kwa kutumia dakika 13 na sekunde 3.30.

Olympia Rio 16 20 08 Momente 5000 Meter Herren Mo Farah
Mo Farah wa UingerezaPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Mmarekani, Paul Chelimo, alijinyakulia medali ya fedha, iliyorejeshwa kwake baada ya kukata rufaa baada ya hapo kabla kuvuliwa medali hiyo kwa kukiuka sheria za mistari ya kukimbilia. Hagos Gebrhawit, wa Ethiopia alipata shaba akimtangulia mkimbiaji wa siku nyingi mwenye umri wa miaka 41 Mmarekani, Bernard Lagat.

Caster Semenya, wa Afrika Kusini naye alijinyakulia medali ya dhahabu katika mbio za mita 800, akipambana kutoka nyuma na kumpita Francine Niyonsaba wa Burundi katika kona ya mwisho kabla ya kumaliza akiwa wa kwanza. Semenya alishinda kwa kutumia rekodi ya taifa ya Afrika Kusini ya dakika 1, sekunde 55.28, wakati Niyoinsaba wa Burundi alikuwa wa pili kwa kutumia dakika 1 sekunde 21. Margaret Wambui wa Kenya aliondoka na medali ya shaba kwa kukimbia dakika 1 sekunde 56.89.

Olympia Rio 16 20 08 Momente 800 Meter Frauen Caster Semenya
Caster Semenya wa Afrika kusiniPicha: picture-alliance/empics/M. Egerton

Leo (21.08.2016) ikiwa ni siku ya mwisho ya mashindano ya Olimpiki kuna medali za mpira wa kikapu, volleyball, mbio za marathon, ngumi, mieleka na mingi mingine.

Katika mbio za marathon Ghirmay Ghebreslassie bingwa wa dunia atajaribu kuipatia Eritrea medali ya dhahabu , lakini haitakuwa rahisi sana kwake kwa kuwa atakumbana na upinzani kutoka kwa bingwa mtetezi Stephen Kiprotich wa Uganda. Pia kuna mkimbiaji kutoka Marekani Galen Rupp, aliyeshinda mbio za mchujo za Olimpiki kwa mara ya kwanza tangu kuingia katika mashindano ya marathon .

Mwandishi: Sekione Kitojo / ape /dpae

Mhariri: Yusra Buayhid