1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Olimpik:Phelps atamba

12 Agosti 2008

Michael Phelps anyakua medali yake ya 9 ya dhahabu.

https://p.dw.com/p/EvWn
Michael PhelpsPicha: AP

Michezo ya 29 ya olimpik ikiendelea kwa siku yake ya 4 hii leo,muamerika Michael Phelps anaendelea nae kutia fora katika hodhi la kuogolea. Phelps leo amenyakua medali yake ya 9 ya dhahabu ya olimpik huku akilenga kuivunja ile rekodi ya Mark Spitz ya medali 7 kutoka mchezo mmoja wa olimpik.

China inaendelea nayo kutamba katika orodha ya medali na imenyakua medali nyengine ya dhahabu mara hii katika mchezo wa Gymnastics.

Katika ringi ya mabondia, Bruno Julie wa Mauritius amemtimua nje Thabiso Nketu wa (Lesotho) wakati Mghana Issah Samir, amekiona cha mtema kuni kutoka kwa Hector Manzanilla wa Venezuela.

Muogoleaji wa Marekani Michael Phelps ameandika jina lake miongoni mwa mabingwa wa kubwa wa Olimpik kwa kunyakua leo medali yake ya 9 ya dhahabu ya olimpik-hii ikiwa ni rekodi.Ni mwanariadha wa kimarekani Carl Lewis pekee ,muogoleaji Mark Spitz,Paavo Nurmi wa Finnland na mrusi Larysa Latynina ndio walioshinda medali nyingi za dhahabu za olimpik kama Michael Phelps.lNa kwavile amenyakua medali yake ya 3 tu ya dhahabu kutoka michezo hii ya Beijing,ana kila nafasi ya kuwapikua hao wote hapo kesho jumatano atakaposhiriki katika finali 2 za kuogolea.

Phelps aliongo´za juhudi za Marekani za kuwapiku wachina kileleni mwa orodha ya medali,lakini China ikadai "jogoo la shamba-Marekani,halitaachiwa kuwika mjini Beijing.

Timu ya wasichana wa China ya gymnastic ilitamba na hivyo China, iliomaliza nafasi ya pili nyuma ya Marekani katika michezo iliopita ya Olimpik mjini Athens,Ugiriki,imepania kweli kuparamia kileleni mwa ngazi ya medali pale michezo hii itakapofungwa August 24.

Machina wametawala medani ya vyuma vizito-weight-lifting na wameshinda michezo 4 kati ya 6.Wakashin da medali zote 3 za dhahabu katika kupigambizi zilizotolewa hadi sasa na halkadhjalika wakashinda katika kutunga shabaha kwa bunduki na hata judo.

Mabondia wa Afrika walijitosa jana ringini kama vile akina Okoth wa Kenya.Katika mapambano 32 ya leo jumaane, tayari Emanuel Nketu wa Lesotho amechapwa makonde na Mmauritius Bruno Julie.Mghana Issah Samir ametimuliwa nje ringini na Hector Rangel wa Venezuela.

katika orodha ya medali leo siku ya 4 ya mashindano, China inaongoza kwa jumla ya medali 18-kumi na moja zikiwa za dhahabu, tatu za fedha na 4 za shaba.China inafuatwa na Marekani nafasi ya pili yenye jumla ya medali 21,lakini 7 tu ni za dhahabu,sita za fedha na 8 za shaba.

Korea ya kusini inafuata nafasi ya 3 huku Zimbabwe ikiongoza orodha ya Afrika kwa medali zake 2 za fedha kutoka hodhi la kuogolewa.Ujerumani inaifuata Zimbabwe nafasi ya 20 pia ikiwa na medali 2 zote za shaba.Nchi nyengine ya Afrika iliondoka na medali hadi sasa ni Algeria-moja ya shaba.