1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Olmert asema lazima Israel iondoke katika maeneo inayokalia

Kalyango Siraj30 Septemba 2008

Matamshi yake yanatazamiwa kuzusha mgogoro

https://p.dw.com/p/FRi4
Ehud Olmert asema ili Israel kupata amani ni lazima iondoke katika maeneo inayokaliaPicha: AP

Waziri Mkuu Ehud Olmert wa Israel amesema kuwa nchi yake ni lazima iachane na karibu eneo lote la ukingo wa magharibi inalokalia kwa nguvu mkiwemo Jerusalem ya Mashariki,ikiwa inataka kupata amani ya kudumu na Wa Palestina.

Ameyasema hayo katika mahojiano yaliyochapishwa jumatatu.

Bw Olmert katika mahojiano na gazeti la Israel la kila siku la Yediot Aharonot,ameliambia kuwa alichukuwa anasema hakijawahi kusemwa na kiongozi yeyote wa Israel.

Katika kile kinachoonekana kama tamko la kisiasa la kiongozi anaeondoka madarakani akiwa na madaraka machache, amesema kuwa ni lazima Israel ifikie makubaliano na Wa palestina ,akifafanua kuwa hilo linamaanisha kuwa ni lazima Israel iondoke kutoka katika karibu maeneo yote.

Ameendelea kuwa ni lazima Israel ibakize na asili mia fulani ya maeneo hayo lakini Wapalestina nao wapewe asili mia iliobaki.Amefafanua kuwa bila kufanya hivyo amani haitapatikana.

Miongoni mwa maeneo ambayo anasema ni lazima yatolewe kwa waPalestina kwa minajili ya amani ni Jerusalem akimaanisha upande wa mashariki wa mji huo ambao unakaliwa na waarabu.Mji wa Jerusalem mzima unachukuliwa kama mji mtakatifu na ulikaliwa kwa nguvu na Israel na baadae kuchukuliwa kama sehemu yake baada ya vita vya mashariki ya kati vya mwaka wa 1967.Sehemu hiyo ya mashariki ya mji wa Jerusalem inachukuliwa kama mji mkuu wa Palestina iliohuru.

Matamshi haya ya Bw Olmert ambae anaongoza serikali ya mpito kufuatia kujiuzulu kwake Septemba 21, yanaweza yakazusha mgogoro nchini humo.Kirasmi Israel inauchukulia mji huo kama daima mji wao mkuu na usiogawanyika.

Lakini akikariri matamshi yake Olmert alisema kuwa kusalimu amri sehemu ya mji huo ndio njia pekee ya kuimarisha usalama wa Israel.

Akitetea hoja yake hiyo ametoa mfano wa mashambulio ya mwezi Julai yaliyofanywa na waPalestina kutoka upande wa mashariki wakitumia tingatinga kugonga magari ya wapita njia.Ameendelea kuwa yeyote anaetaka kudhibiti mji huo mzima itamlazimu kuwajumulisha waarabu wote 270,000 kuwa chini ya himaya ya Israel jambo alilosema kuwa haliwezekani.

Amesema kuwa ni lazima uamuzi uchukuliwe, na uamuzi huo unakwenda kinyume na mahitaji yao pamoja na kumbukumbu zao na vilevile kwenda kinyume na sala za Wayahudi za miaka 2,000.

Gazeti hilo limeandika kuwa Olmert ana kiri kuwa alikosea katika maoni yake ya sera zake za kigeni pamoja na vitendo kwa miaka mingi.

Mmoja wa wajumbe wa Palestina katika mazungumzo na Israel,Saeb Erekat,akitathmini matamshi ya Olmert amesema kuwa Israel ni sharti itafsiri matamshi hao katika vitendo ikiwa kweli inataka amani.Ameliambia shirika la habari la AFP kuwa njia pekee ya kuweza kupatikana amani ni kwa Israel kuondoka katika ardhi inayokalia kwa mabavu mkiwemo ukingo wa magharibi.

Bw Olmert aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu Septemba 21 baada ya madai ya rushwa ambayo yalipelekea polisi kumuhoji na kupendekeza kumfunguklia mashtaka.Hata hivyo anaendelea kuongoza hadi serikali mpya itakapoteuliwa.

Kiongozi mpya wa chama tawala cha Kadima, waziri wa mashauri ya kigeni Tzipi Livni,anahangaika kuunda serikali ya mseto ili kuepuka uchaguzi mkuu ambao unaweza kukiweka madarakani chama cha mrengo wa kulia cha Likud.