1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Olympiki yaendelea: Uhispania hoi

30 Julai 2012

Ni siku ya tatu leo(30.07.2012) katika mashindano ya Olimpiki mjini London,timu za riadha za mataifa ya Kenya na Ethiopia zinatarajiwa kuwasili kesho mjini London, tayari kwa kinyang'anyiro kinachoanza August 3.

https://p.dw.com/p/15glw
Spain's Alberto Botia consoles his team mate Alvaro Dominguez (L) after losing their men's Group D football match against Honduras in the London 2012 Olympic Games at St James' Park in Newcastle July 29, 2012. REUTERS/Nigel Roddis (BRITAIN - Tags: SPORT OLYMPICS SPORT SOCCER)
Timu ya vijana ya Uhispania yatolewa na mapemaPicha: Reuters

Tayari wanamichezo wameanza kuvunja rekodi katika michezo hii ya Olimpiki. Matarajio yalikuwa huenda rekodi chache zitavunjwa katika michezo hii ya London, ikilinganishwa na rekodi 25 zilizovunjwa katika michezo ya Olimpiki ya mjini Beijing miaka minne iliyopita. Tayari rekodi tatu zimekwisha vunjwa katika siku mbili za mwanzo katika mchezo wa kuogelea.

Spain's Mireia Garcia Belmonte waves after competing in a women's 200-meter individual medley swimming heat at the Aquatics Centre in the Olympic Park during the 2012 Summer Olympics in London, Monday, July 30, 2012. (AP Photo/Daniel Ochoa De Olza)
Rekodi 3 zimevunjwa katika kuogeleaPicha: dapd

Katika mchezo wa Judo , wachezaji wanaopewa nafasi ya juu kunyakua medali za dhahabu katika mchezo huo, Wang Ki-Chun wa Korea ya kusini, na Riki Nakaya wa Japan wamefanikiwa kupita katika duru za mwanzo leo.

Pia kumekuwa na michezo ya duru za mwanzo za kulenga shabaha , Badminton na tennis.

Wanamichezo wa mataifa ya Afrika walifanya vizuri katika michezo ya kandanda na mpira wa kikapu .

Tiki taka yashindwa kutamba

Nao mashabiki wa soka wa Uhispania ilibidi wakabiliane na hali mbaya ya kushindwa leo baada ya timu yao iliyokuwa inashiriki mashindano ya Olimpiki kulazimika kuyaaga mashindano hayo mjini London na mapema baada ya kupokea vipigo mara mbili mfululizo dhidi ya Japan na Honduras kwa kuzabwa bao 1-0 kila mchezo. Vipigo hivyo vimesababisha Uhispania ambayo timu yake ya wakubwa ni mabingwa wa dunia na kombe la mataifa ya Ulaya mara mbili mfululizo kufunga virago na kurejea nyumbani kwa huzuni.

Honduras' Jose Mendoza celebrates with his team mate Jose Velasquez after defeating Spain in men's Group D football match at London 2012 Olympic Games
Wachezaji wa Honduras wakifurahia kuichapa Uhispania bao 1-0 katika sokaPicha: Reuters

Wachezaji wa Uhispania walishindwa kuzuwia kuonyesha hasira zao pale mwamuzi kutoka Venezuela Juan Soto kuwanyima penalti mbili katika kipindi cha pili cha mchezo wao mjini Newcastle. Baada ya timu ya wakubwa ya Hispania kuzoa kila taji ulimwenguni, kikosi chake cha vijana wa umri wa miaka 23 kimeonesha sifa mbaya kwa dunia kwa kuonyesha hisia za hasira kwa kumzingira fera alipopuliza firimbi ya mwisho. Gazeti la Hispania la Marca limeandika, Uhispania yatoa mkono wa kwaheri kwa michezo ya olimpiki mjini London huku wakitia aibu.

Michuano ya vijana Afrika

Duru ya kwanza ya michuano ya timu za taifa za vijana wenye umri chini ya miaka 20 katika bara la Afrika ilifanyika jana na timu ya taifa ya Kenya iliweka matumaini yake hai baada ya kutoka sare ya bila kufungana na mafarao wa Misri mjini Cairo, Uganda ikaisambaratisha Ghana kwa kuifunga mabao 3-1 mjini Kampala, Rwanda ikatoka kidedea kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mali . Tanzania, hata hivyo, ni timu pekee ya Afrika mashariki kushindwa kutamba , wakati ilipokubali kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya mabingwa watetezi Nigeria nyumbani mjini Dar Es Salaam.

Zambia imepita baada ya Lesotho kujitoa mashindanoni, na Algeria inaingia moja kwa moja katika fainali kutokana na kuwa mwenyeji wa fainali hizo.

Dar Young Africans ni mabingwa wa kombe la Kagame la vilabu vya Afrika mashariki na kati. Ni miezi mitatu tu iliyopita Yanga iliadhibiwa na watani wake wa jadi Simba kwa kufungwa mabao 5-0 katika mchezo wa mwisho wa ligi, na kusababisha kukosa nafasi ya kuliwakilisha taifa katika mashindano ya Afrika. Leo hii Yanga ni mabingwa wa kombe hilo la Kagame, baada ya kuibanjua Azam FC kwa mabao 2-0 katika fainali mwishoni mwa juma.

Mwandishi : Sekione Kitojo /

Mhariri : Miraji Othman