1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Onesphore Rwabukombe ahukumiwa miaka 14 jela

18 Februari 2014

Mahakama moja ya Ujerumani mjini Frankfurt imemhukumu kifungo cha miaka 14 jela meya wa zamani wa Rwanda kwa makosa ya kuandaa mauwaji kanisani wakati wa mauwaji ya halaiki ya mwaka 1994.

https://p.dw.com/p/1BB3C
Onesphore Rwabukombe akizungukwa na mawakili wake mahakamani mjini FrankfurtPicha: imago/epd

Ilikuwa kesi ya kihistoria iliyomalizika baada ya maandalizi ya miaka mitatu.

Mwendesha mashtaka mkuu alitaka mshtakiwa huyo Onesphore Rwabukombe ahukumiwe kifungo cha maisha jela huku mawakili wake wakiidai aachiwe huru.

Jumla ya watu 15 waliitwa kutoa ushahidi wa yaliyotokea.Wengi wao wameletwa makusudi na mahakama hiyo kutoka Rwanda .Wengine wanaotumikia kifungo nchini BRwanda walitoa ushahidi kupitia njia ya mawasiliano ya Video.

Onesphore Rwabukombe,mwenye umri wa miaka 56 amekutikana na hatia ya kuhusika na uhalifu wakati wa mauwaji ya halaiki.Meya huyo wa zamani wa Kiziguro,kati kati ya Rwanda alikuwa anatuhumiwa kuandaa,kuamuru na kusimamia mauwaji katika kanisa moja ambako watu wasiopungua 400 waliuliwa mwaka 1994.

Akivalia suti nyeusi,mbunge huyo wa zamani wa Rwanda akizungukwa na mawakili wake wawili hakutaharuki hukmu dhidi yake ilipotamkwa.

Mawakili wake Wakata Rufaa

Hukmu hiyo iliyotolewa na korti ya mkoa wa Frankfurt ni ya kwanza ya aina yake kuwahi kutolewa na korti ya Ujerumani kuhusiana na mauwaji ya halaiki ya watutsi nchini Rwanda.

Ruanda Völkermord 1994 Hutu Tutsis Gedenkstätte Nyamata
Mabufuu ya wahanga wa mauwaji ya halaiki ya mwaka 1994Picha: AP

Rwabukombe amekuwa akiishi nchini Ujerumani tangu mwaka 2002 baada ya kuikimbia nchini yake na kuomba hifadhi ya ukimbizi barani Ulaya.

Maafisa wa serikali nchini Ujerumani waliamua wasimrejeshe Rwanda, na kukubaliana afikishwe mahakamani humu nchini kwa hofu kesi yake nchini Rwanda isije ikawa si ya haki.

Kuambatana na muongozo washeria ya kimataifa kesi ya mauwaji ya halaiki inaweza kusikilizwa na adhabnu kutolewa kokote kule sio lazma mahala mauwaji ya halaiki yalikofanyika.

Kuuliwa rais wa Rwanda Juvénal Habyarimana April 6 mwaka 1994 ndio chanzo cha mauwaji ya halaiki yaliyoangamiza maisha ya watu laki nane kati ya mwezi wa April hadi Julai mwaka 1994.Hayo ni kwa mujibu wa umoja wa Mmataifa.Wengi wa wahanga hao walikuwa wa kanbila la Tutsi ingawa wahutu wa msimamo wa wastani nao pia walikuwa miongoni mwa wahanga wa mauwaji hayo ya halaiki.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman