1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ongezeko la joto kupunguzwa hadi chini ya asilimia 2

12 Desemba 2015

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius aliekuwa mwenyekiti wa mkutano wa mjini Paris uliojadili athari za mabadiliko ya tabia nchi aliuwasilisha mswada huo huku akishangiliwa.

https://p.dw.com/p/1HMKP
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius(Katikati) awasilisha mswada wa makubaliano
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius(Katikati) awasilisha mswada wa makubalianoPicha: Reuters/S. Mahe

Waziri Fabius amesema mswada huo ni kabambe, wa haki wa muda mrefu,unazingatia maslahi ya pande zote na pia utaziwajibisha nchi kisheria.Ameeleza kuwa ikiwa utapitishwa, hiyo itakuwa hatua ya kihistoria ya mabadiliko makubwa.

Ongezeko la joto halitazidi asilimia 2

Kulingana na mswada huo,lengo ni kupunguza ongezeko la joto hadi kufikia chini ya asilimia 2. Waziri huyo wa Ufaransa pia amefahamisha kwamba nchi zinazoendelea zitatengewa dola Bilioni 100 kila mwaka kuanzia mwaka wa 2020 ili kuzisaidia kujiweka sawa.

Kwa mujibu wa hati hiyo ukaguzi wa utekelezaji wa hatua ya kupunguza gesi zinazoongeza joto utafanyika kila baada ya miaka mitano na utakuwa sehemu ya mipango ya kitaifa.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa ametoa mwito wa kuuidhinisha mswada juu ya athari za mabadiliko ya tabia nchi uliotolewa leo mjini Paris. Rais Hollande amewaambia wajumbe kutoka nchi karibu 200 waliohudhuria mkutano wa mjini Paris kwamba hati ilioyotolewa leo ni ya kihistoria na italeta manufaa duniani kote.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon pia ametoa mwito kutoka kwenye moyo wake wote kuwataka walioshiriki kwenye mazungumzo ya mjini Paris waupitishe mswada uliotolewa leo.Aliwaambia wajumbe hao kwamba dunia yote inawatazama wao "na ina imani na busara yenu" Katibu Mkuu Ban ametamka kwamba maslahi ya kitaifa yatatimizwa vizuri zaidi kwa kuyatimiza maslahi ya kimataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ahimiza kuidhinishwa mswada wa makubaliano
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ahimiza kuidhinishwa mswada wa makubalianoPicha: Reuters/S. Mahe

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema mswada wa mkataba ni mzuri lakini inapasa kusubiri.

Wajumbe kutoka nchi zaidi ya 190 waliokutana mjini Paris wamefanikiwa kupiga hatua hiyo ambayo haijawahi kufikiwa katika miaka 20 ya mazunguzo juu ya kuzikabili athari za mabadiliko ya tabia nchi- yaani makubaliano kwa nchi zote juu ya kupunguza gesi ya kaboni na nyingine zinazoongeza joto duniani.

Kwenye mkutano wao wajumbe wamekubaliana kuzisaidia nchi masikini kuzikabili athari zinazotokana na kupanda kwa vina vya bahari, na athari za hali mbaya za hewa na nyingine zinazotokana na ongezeko la joto duniani.

Wengine waliandamana wakati wa mkutano wa mjini Paris
Wengine waliandamana wakati wa mkutano wa mjini ParisPicha: Reuters/J. Naegelen

Ikiwa utapitishwa huo utakuwa mkataba wa kwanza unaozishirikisha nchi zote, tofauti na rasimu ya Kyoto iliyozishirikisha nchi tajiri tu. Hata hivyo ikiwa nchi hazitayaidhinisha, yaliyofikiwa mjini Paris ,hapatakuwapo na uzito wa kuziwajibisha nchi kuyatekeleza kisheria.

Badala yake itakuwa hiyari ya kila nchi peke yake kuchukua hatua za kupunguza gesi zinazoongeza joto.

Nchi ziligawanyika juu ya kiwango cha kupunguza ongezeko la joto,katika msingi wa muda mrefu.Nchi nyingi zilisisitiza kwamba joto lipunguzwe hadi kufikia asilimia 1.5 badala ya asilimia 2. Wajumbe wa nchi hizo wamesema kiwango cha asilimia 1.5 ndicho kitachoepusha maafa yanayobabishwa na ongezeko la joto.

Suala jingine la utatanishi lilikuwa juu ya msaada wa fedha kwa nchi zinazoendelea. Umoja wa Ulaya na Marekani zilizitaka nchi zinainukia kiuchumi ambazo ni tajiri kama China na India nazo pia zichangie.

Mwandishi:Mtullya Abdu/ape,rtre,

Mhariri: Isaac Gamba