1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ongzeko la uagizaji wa bidhaa za chakula wakwamisha mazunguzo ya Doha

Mohamed Dahman10 Machi 2008

Kundi la nchi 33 zinazoendelea zimeshutumu rasimu ya utaratibu maalum wa kujilinda hususan na ongezeko kubwa la uagizaji chakula kutoka nje kwa nchi zinazoendelea.

https://p.dw.com/p/DLZX
Nyama ya kuku ni mojawapo ya bidhaa za chakula zinazopelekwa katika nchi zinazoendeleaPicha: AP

Shutuma hizo zimetolewa katika mazungumzo yanaoendelea hivi sasa ya Shirika la Biashara Duniani WTO yanayojulikana kama Duru ya Maendeleo ya Doha kwamba rasimu hiyo ni kali mno,haitoshelezi kabisa na ni mzigo na haifai.

Utaratibu huo maalum wa kujilinda unaojulikana kwa ufupi kama SSM umependekezwa kufuatia ogezeko kubwa la uagizaji wa chakula wa mara kwa mara katika masoko ya nchi zinazoendelea katika kipindi cha miongo miwili iliopita.

Nyingi ya nchi hizo imebidi zipunguze viwango vyao vya ushuru hasa kutokana na mipango ya marekebisho ya miundo ya taasisi za fedha za kimataifa kulikopelekea kufungwa kwa viwanda vya uzalishaji wa bidhaa,kuongezeka kwa ukosefu wa ajira vijijini na kuongezeka kwa migogoro ya wakulima katika nchi hizo nyingi.

Utaratibu huo ungeliziruhusu nchi zinazoendelea kuongeza ushuru wao wakati viwango vya uagizaji vitakapopindukia viwango viliopo hivi sasa kwa kiasi fulani.Ushuru wa juu pia unaweza kuwekwa iwapo bei za bidhaa hizo kutoka nje zitapokushuka chini ya viwango fulani.

Rasimu hiyo imependekezwa na mwenyekiti wa mazungumzo hayo ya Kilimo balozi wa New Zealand Crawford Falconer.Kundi la nchi 33 linawakilisha jumla ya nchi 46 zinazoendelea katika mazungumzo hayo yanayofanyika mjini Geneva Uswisi.

Utaratibu huo ni hatua ya kibiashara inayoungwa mkono na kundi la nchi mbali mbali zinazoendelea linaloongozwa na Indonesia na linajumuisha nchi kutoka kila bara zikiwa ni India, China,Ufilipino,Nigeria,Kenya,Senegal,Tanzania, Jamhuri ya Dominika,Jamaica na Bolivia.

Kushutumiwa kwa rasimu hiyo kumekwamisha mazunggumzo hayo.Maudhui ya mwenyketi kama inavyoitwa rasimu hiyo ya Falconer ina vikomo vingi ambavyo hatimae vitakuja kutowa utaratibu usiofaa hivyo ndivyo ilivyosema kundi la mataifa 33 katika mkutano wiki iliopita.

Kufanya mambo hayo yazidi kuwa maguu zaidi nchi tatu zinazoendelea Argentina,Uruguay na Paraguay hivi karibuni zimependekeza vikwazo zaidi kuliko hata vile vilioko kwenye rasimu ya mwenyekiti.

Kwa mujibu wa mjumbe wa G33 ambaye amezungumza kwa masaharti ya kutotajwa jina kutokana na unyeti wa mazungumzo hayo ameliambia shirika la habari la IPS kwamba utaratibu huo wa SSM ni tatizo kubwa na kumwekuwepo na mjadala mkali juu ya suala hilo na kwamba hawakupenda kile alichofanya mwenyekiti huyo.

Kwa mujibu wa mjumbe huyo mazungumzo yanakwenda kombo.

Shirika la Chakula Duniani FAO limegunduwa kwamba taathira ya ongezeko hilo la uagizaji wa bidhaa kutoka nje ni kubwa sana kwa uzalishaji wa bidhaa wa ndani ya nchi.

Nchini Senegal ugizaji wa nyanya ya kopo kutoka Ulaya umeongezeka mara 15 zaidi na uzalishaji wa ndani ya nchi umeshuka kwa asilimia 50.Nchini Burkina Faso uagizaji wa nyanya ya kopo umeongezeka mara nne na kupunguza uzalishaji wa ndani ya nchi kwa nusu.Ghana uagizaji wa mchele umeongezeka kutoka tani 250,000 hapo mwaka 1998 hadi kufikia tani 415,150 hapo mwaka 2003 na kwa ujumla asilimia 66 ya wazalishaji mpunga ndani ya nchi wamerikodi faida mbaya kulikosababisha ukosefu wa ajira.

Nchini Jamaica kuongezeka maradufu kwa mafuta ya mboga kumepunguza uzalishaji kwa asilimia 68.Kenya nako uagizaji wa bidhaa za maziwa kumeongezeka mno na kusababisha kushuka kwa bei za maziwa ya ndani ya nchi.

Kuna suala tata iwapo nchi zinazochukuwa hatua za kudhibiti ongezeko la uagizaji wa bidhaa hizo zinaruhusiwa kuongeza ushuru kupindukia viwango walivyokubaliana wakati wa mazungumzo ya Duru la Uruguay.

Rasimu ya mwenyekiti hairuhusu jambo hilo lakini kundi la G33 linashupalia jambo hilo liruhusiwe.