1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

OPEC kupunguza uzalishaji wa mafuta wa mapipa milioni mbili kwa siku ili kupandisha bei ya mafuta

Mohamed Dahman17 Desemba 2008

Nchi wanachama za shirika la OPEC zinazosafirisha nje mafuta kwa wingi duniani na zile zisizo wanachama wa leo hii zimechukuwa hatua ambayo yumkini ikaondowa katika soko mapipa ya mafuta milioni mbili na laki sita.

https://p.dw.com/p/GI4m
Mojawapo ya machimbo ya mafuta Mashariki ya Kati.Picha: AP

Hilo ni jaribio la kuongeza bei ya mafuta na mapato ya nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika mkutano usio wa kawaida mjini Oran nchini Algeria na kufanya upunguzaji huo wa mafuta wa mkupuo mmoja kuwa mkubwa kabisa kuwahi kufanywa na kundi hilo.

____________________________________________________

Waziri wa mafuta wa Saudi Arabia amesema kwamba shirika hilo la OPEC la nchi wanachama 13 wamekubaliana katika mkutano wao kupunguza uzalishaji wa mafuta wa mapipa milioni mbili kwa siku wa shirika hilo ukiwa ni upunguzaji mkubwa sana kuwahi kushuhudiwa na ni sawa na asilimia 7.0 ya uzalishaji wake wa hivi sasa wa mapipa milioni 27 kwa siku.

Waziri wa mafuta wa Saudi Arabia Ali al- Nuaimi amewaambia waandishi wa habari wakati mkutano huo wa OPEC ukianza kwamba kuna muafaka juu ya kupunguza uzalishaji wa mapipa milioni mbili kwa siku.

Mawaziri wa OPEC wameitisha mkutano huo kuzuwiya kuporomoka kunakoendelea kwa bei ya mafuta ambao hivi sasa umepunguwa kwa asilimia 70 ya vile ilivyokuwa hapo mwezi wa Julai ambapo pipa moja lilikuwa likiuzwa kwa dola 147.Kushuka huko kwa bei ya mafuta kumetokana na kupunguwa kwa mahitaji yake katika nchi zenye maendeleo makubwa ya viwanda duniani zenye kutumia mafuta kwa wingi.

Muda mfupi kabla ya kufunguliwa kwa mkutano huo Urusi ambayo sio mwanahama wa OPEC ambayo inahudhuria mkutano huo na Azerbaijan zimesema ziko tayari kupunguza uzalishaji wao wa mafuta kila mmoja kwa mapipa 300,000 kwa siku.

Maafisa wa shirika hilo la OPEC linalosafirisha nje mafuta kwa wingi duniani walitowa wito kwa nchi zisizo wanachama ziwasaidie kutuliza masoko.Katibu Mkuu wa OPEC Abdallah Salim El-Badri amesema hapo jana kwamba alikuwa akitaka nchi zisizo wanachama wa shirika hilo zinazozalisha mafuta kwa wingi kupunguza uzalishaji wao kwa mapipa ya mafuta 500,000 hadi 600,000 kwa siku.

Mchambuzi Peter Beutel anasema kwa kuwa Wasaudi kwa desturi ni wanachama wa msimamo wa wastani au kwa maneno mengine wenye kupenda amani ndani ya shirika hilo la OPEC wito huu wa kupunguza mno uzalishaji wa mafuta ni habari mbaya kwa watumiaji wa mafuta duniani venginevyo bei zozote zile za juu za mafuta hatimae ziwe zinapelekea uvumbuzi na uchimbaji mpya wa mafuta.

Ameongeza kusema kwamba tatizo kubwa na upunguzaji wa uzalishaji wa mafuta wa mapipa milioni mbili kwa siku au zaidi ni kwamba itamaanisha kuwa OPEC itakuwa takriban imepunguza uzalishaji wake wa mafuta wa mapipa milioni nne kwa siku kwa mwaka huu kima ambacho hakikuwahi kushuhudiwa.

Harakati za kiuchumi duniniani tokea mwezi wa Julai wakati bei za mafuta zilipokuwa juu kabisa zimekuja kusamabaratika kutokana na machafuko ya kifedha yaliosababishwa na utowaji ovyo wa mikopo ya nyumba nchini Marekani yalipozogaa na kuathiri uchumi duniani kote.

Wakati baadhi ya nchi zenye maendeleo makubwa ya viwanda duniani zinazotumia mafuta kwa wingi hususan Marekani,Ujerumani na Japani tayari uchumi wao ukiwa unashuka na nchi nyengine kama vile China zikikabiliwa na kuzorota sana katika kukua kwa uchumi wake mahitaji ya mafuta ghafi yamepunguwa na hiyo kuathiri bei yake.

Lakini uwezo wa OPEC kushawishi upandaji wa bei hatimae kunategemea iwapo soko litaamini kwamba kundi hilo litapunguza kweli uzalishaji wake wa mafuta.