1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Operesheni ya kijeshi yanukia Syria bila UN

Frank Bettenfeld28 Agosti 2013

Uwezekano wa Umoja wa Mataifa kuidhinisha mashambulizi dhidi ya Syria ni mdogo sana, lakini tayari Marekani na washirika wake wanafanya maandalizi ya mashambulizi kupitia dhana ya uwajibikaji wa kimaadili.

https://p.dw.com/p/19Xl2
The US aircraft carrier Carl Vinson (R) and the cruiser USS Bunker Hill (L) sit anchored off Manila Bay after arriving on May 15, 2011 for a four-day port of call accompanied by three other warships. The Carl Vinson is making a port call in the Philippine capital after its crew buried Osama bin Laden's remains in the Arabian Sea AFP PHOTO / JAY DIRECTO (Photo credit should read JAY DIRECTO/AFP/Getty Images)
USA verstärken Marine-Präsenz vor syrischer KüstePicha: Jay Directo/AFP/Getty Images

Wiki moja baada kutokea shambulio linalodaiwa kuwa la kemikali nchini Syria, mataifa kadhaa yameanza kupeleka vikosi kujiandaa na mashambulizi. Siku ya Jumatatu waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza William Hague alielezea uhakika kwamba gesi ya sumu ilitumiwa na vikosi vitiifu kwa rais Assad. Uchunguzi wa karibu juu ya shambulio hilo unaendelea kufanywa na wakaguzi wa Umoja wa Mataifa. Iwapo watabainisha kuwa kweli gesi hii ilitumiwa na upande wa serikali, hakuna kitakachozuia mashambulizi ya kijeshi.

Rais wa Marekani Barack anasema utawala wa Assad laazima uwajibishwe. ***FREI FÜR SOCIAL MEDIA***
Rais wa Marekani Barack anasema utawala wa Assad laazima uwajibishwe.Picha: Reuters

Muungano wa hiari
Kulingana na muktadha wa sheria hata hivyo, mashambulizi hayo yatakuwa yanakiuka sheria za kimataifa, kwa kuwa uhalali wake unaweza kutokana tu na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, ambako China na Urusi zinaweza kuzuia mpango huo kwa kutumia kura zao za turufu. Kwa nchi hizo mbili, uingiliaji kijeshi kutoka mataifa ya nje siyo njia ya kuleta suluhu.

Kama litafanyika shambulizi la kijeshi, haitakuwa mara ya kwanza kwa Marekani kuchukua hatua kama hiyo pasipo idhini ya Umoja wa Mataifa. Rais wa zamani wa Marekani George W. Bush, kupitia kile alichokiita muungano wa hiari, aliyaongoza mataifa kadhaa kuivamia Iraq mwaka 2003, kwa madai ya kuikomboa kutoka mikononi mwa Saddam Hussein.

Kabla ya uvamizi huo, Marekani ilijaribu kupitisha hoja yake ndani ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, kuonyesha kuwa kulikuwepo silaha za maangamizi nchini Iraq, ambapo waziri wa ulinzi wa wakati huo Collin Powell aliwasilisha ushahidi wa madai hayo katika baraza.

Hata hivyo, kulikuwa na mashaka makubwa kwa upande wa Ufaransa, Urusi na Ujerumani kuhusiana na ushahidi huo, na waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Joschker Fischer, alieleza bayana kuwa hakuridhika na ushahidi wa Marekani. Na kwa hakika mashaka yake yalikuja kutimia, baada ya kubainika kwamba ushahidi uliyowasilishwa katika umoja wa mataifa ulikuwa wa kughushi. Collin Powell alikiri kufanya makosa na kujiondoa katika ulingo wa siasa.

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron anakutana na maafisa wa juu serikalini na jeshi kujadili mikakati.
Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron anakutana na maafisa wa juu serikalini na jeshi kujadili mikakati.Picha: Getty Images/Afp/Carl Court

Ulinganisho na Kosovo
Lakini kwa Manfred Eisele, Meja Jenerali mstaafu wa jeshi la Ujerumani Bundeswehr, mazingira ya uingiliaji kati nchini Iraq siyo sawa na yaliyopo nchini Syria hivi sasa. Lakini anaona ulinganifu kati ya Syria na Kosovo mwaka 1999, ambako waasi wa kabila la Albania walipigana vita vya kujitenga na serikali ya Yugoslavia.

Wakati wa mgogoro huo zilijitokeza ripoti za mara kwa mara juu ya ukiukaji wa haki za binaadamu na mauaji ya kimbari yaliyokuwa yakifanywa na jeshi la Yugoslavia. Urusi ilikubali katika baraza la usalama lakini ilipinga uingiliaji kati wa vikosi vya kimataifa, hali iliyoilaazimu jumuiya ya kujihami NATO kuingilia kati bila idhini ya Umoja wa Mataifa.

Andreas Bock, mtaalamu wa siasa kutoka chuo kikuu cha Augsburg anakubaliana na maoni ya Eisele, na anasema Kosovo kulikuwepo na ukiukaji wa dhahiri wa haki za binaadamu uliohalalisha uingiliaji kati. Anasema hata kama hatua hii ilikuwa inakwenda kinyume na sheria za kimataifa, kulikuwepo na wajibu wa kimaadili kwa jamii ya kimataifa kusimama pamoja.

Haki dhidi ya maadili
Hata hivyo, uingiliaji wa namna hiyo kwa misingi ya ubinaadamu bila idhini ya Umoja wa Mataifa ulisitishwa mwaka 1990, pale vikosi vya jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika magharibi ECOWAS, vilipoingilia kati nchini Liberia vikiongozwa na Nigeria. Eisele anasema wakati huo dunia haikuwa na maslahi na kilichokuwa kinaendelea nchini Liberia, kwa sababu mauaji yalikuwa yakitokea barani Afrika. Lakini anasema hali iliyokuwepo wakati huo ilikuwa inalinganishwa na hali ya Kosovo.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande alisema hata bila idhidi ya Umoja wa Mataifa laazima Assad achukuliwe hatua.
Rais wa Ufaransa Francois Hollande alisema hata bila idhidi ya Umoja wa Mataifa laazima Assad achukuliwe hatua.Picha: Reuters/Kenzo Tribouillard/Pool

Sheria mpya

Ili jamii ya kimataifa iweze kuingilia kati hali kama hizo bila kuzuiwa na kura za turufu za wanachama watano wa kudumu wa baraza la usalama, serikali ya Canada ilianzisha dhana ya sheria ya wajibu wa ulinzi mwaka 2001, na kuendelezwa na kamati ya wataalamu wa sheria za kimataifa. Kulingana na dhana hiyo, kanuni ya kutoingilia kati masuala ya ndani ya nchi nyingine inasita kutumika pale unapotokea ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu. Kwa kuwa hakuna msimamo wa pamoja katika baraza la usalama, Marekani, Uingereza na Ufaransa zinaweza kutumia dhana hii kuingilia kati nchini Syria.

Mwandishi: Marcus Lütticke
Tafsiri: Iddi ISmail Ssessanga
Mhariri: Daniel Gakuba