1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Osama auawa, azikwa baharini

2 Mei 2011

Marekani imesema mwili wa kiongozi wa mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda, Osama Bin Laden, umezikwa baharini baada ya kuuwawa katika operesheni iliyoendeshwa na wanajeshi wake nchini Pakistan.

https://p.dw.com/p/117Zp
Osama bin Laden
Osama bin LadenPicha: AP

Baada ya kuuwawa kwa kiongozi huyo, maafisa waandamizi nchini Pakistan walisema maziko yake yatatekelezwa kwa taratibu na tamaduni za dini ya Kiislamu. Taratibu hizo ni pamoja na mwili wake kuzikwa katika kipindi cha masaa 24 baada ya kutokea kifo.

Ama kwa upande wao wanachama wa mtandao wa Al- Qaeda katika Rasi ya Uarabuni, Mtandao wa Osama Bin Laden, nchini Yemen wamekiita kifo cha Osama kuwa ni janga kubwa katika harakati zao.

Akizungumza kwa njia ya simu na Shirika la Habari la Ufaransa, AFP, mmoja kati ya wanamtandao hao, amesema hawakuamini waliposikia taarifa za kifo cha kiongozi wao. Amesema, hata hivyo, aliwasiliana na wenzao wa Pakistan ambao walithibitisha kifo hicho.

Rais Barack Obama
Rais Barack ObamaPicha: AP

Awali, Rais Barack Obama wa Marekani alitangaza kwamba Osama Bin Laden ameuwawa katika mashambulizi yaliyofanyika jana nchini Pakistan na kumaliza harakati zilizodumu kwa takribani miaka 10 za kumwinda kiongozi huyo aliyepanga shambulio la Septemba 11 mwaka 2001.

Akizungumza usiku wa kuamkia leo katika Ikulu ya Marekani, Rais Obama amesema " haki imetendeka" dhidi ya kiongozi huyo wa wapiganaji wa kiislamu aliyefanikisha mashambulizi kadhaa katika maeneo tofauti duniani kote.

"Marekani iliendesha operesheni iliyofanikisa kuuwawa kwa Osama Bin Laden. Kiongozi wa Al- Qaeda. Gaidi aliyeshiriki mauwaji ya maelfu ya watu wasio na hatia, wanawake na watoto." Amesema Rais Obama.

Kifo cha Bin Laden ni hatua muhimu ingawa haijawa wazi kama inaweza kubadili vita ya kimataifa dhidi ya mtandao wa kigaidi au kufanikisha kumalizika haraka kwa vita dhidi ya Taliban nchini Afghastan.

Ramani ya Pakistan ikionesha mji wa Abbottabad alipouawa Osama Bin Laden
Ramani ya Pakistan ikionesha mji wa Abbottabad alipouawa Osama Bin Laden

Chanzo kimoja cha habari kutoka katika operesheni za kijeshi za Marekani zinasema Osama alipigwa risasi kichwani. Kifo chake pia kilithibitishwa na maafisa tofauti nchini Pakistan.

Kifo cha Osama kimepokelewa kwa shangwe, nderemo na vifijo katika miji ya Washngton na New York. Hakika umekuwa ushindi mkubwa wa usalama wa kitaifa kwa Obama tangu aingie madarakani mapema 2009 na utampa nguvu ya kisiasa atakapowania tena kiti cha urais 2012.

Obama atakamilisha kwa urahisi vita vya karibu muongo mmoja vya Afghanistan, vilivyoanza Septemba kumi na moja 2001, baada ya shambulio lililowaua takriban watu 3,000 nchini Marekani.

Afrika Mashariki Osama atakumbukwa kutokana na kufanikisha mauaji ya takribani watu 224 huku wengine 5,000 wakijeruhiwa baada ya kufanikisha mashambulizi katika balozi za Marekani nchini Tanzania na Kenya.

Mwandishi: Sudi Mnette/RTR/
Mhariri: Nyiro Charo, Josephat