1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Oslo. Mawaziri wa NATO wamaliza mkutano wao.

27 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CC6P

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa ya NATO wanakamilisha siku yao ya mwisho ya mkutano usio rasmi katika mji mkuu wa Norway , Oslo. Mazungumzo hayo yanalenga katika upanuzi zaidi wa muungano huo wa kijeshi wa mataifa ya magharibi wa mataifa 26.Nchi ambazo zinatarajiwa kuingizwa katika muungano huo wa kujihami ni pamoja na Albania , Croatia na Macedonia.Mawaziri hao pia wanatarajiwa kujadili kujenga uhusiano wa karibu na Ukraine, suala ambalo huenda likaikasirisha Russia.Jana Alhamis , mataifa ya NATO yalieleza wasi wasi wake kuhusiana na tamko la rais wa Russia Vladimir Putin la kusitisha majukumu ya Russia katika mkataba muhimu wa kudhibiti silaha. Waziri wa nchi katika ofisi ya waziri mkuu wa Ujerumani Gernot Erler amesema kuna haja ya kuwa na mjadala wa wazi wa kisiasa kutokana na mpango huo wa kuweka ulinzi dhidi ya makombora katika Ulaya ya mashariki.

Mkataba huo wa kudhibiti silaha za kawaida ama CFE, unaweka uwiano wa uwekaji wa ndege za kivita , vifaru na silaha nyingine ambazo hazihusiani na nuklia katika eneo la Ulaya. Tangazo la Putin linakuja kama jibu kwa mpango wa Marekani wa kuweka mfumo wa ulinzi dhidi ya makombora katika bara la Ulaya.