1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

OUAGADOUGOU : Mkutano wa ECOWAS waahirishwa

22 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CChU

Serikali ya Burkina Faso imesema hapo jana inaahirisha mkutano wa kiuchumi wa kanda wa viongozi uliokuwa umepangwa kufanyika kwenye mji mkuu wa nchi hiyo mwishoni mwa juma hili baada ya polisi na wanajeshi kushambuliana kwa risasi na kupelekea kuuwawa kwa watu watano.

Nchi hiyo imesema mkutano huo ulioandaliwa na Jumuiya Kiuchumi ya Mataifa ya Magharibi ECOWAS kwa kushirikiana na Umoja wa Kiuchumi na Fedha wa kanda hiyo umeahirishwa kwa muda usiojulikana kutokana na kuzuka kwa mapambano hayo wiki hii.

Wanajeshi wakiwa na bunduki za rashasha walifanya fujo mjini Ouagadougou mapema hapo Jumaatano baada ya mwenzao mmoja aliyekuwa hakuvaa sare kupigwa risasi na polisi wakati wa msako wa kawaida.

Wanajeshi hao walikitia moto mojawapo ya kituo kikuu cha polisi jijini humo,waliharibu mali katika makao makuu ya polisi na kuwaachilia huru mahabusu kadhaa kutoka mojawapo ya magereza yake kabla ya kurudi kambini kwao.