1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ouattara ataka amani Cote d'Ivoire

12 Aprili 2011

Rais wa Cote d'ivoire anayetambuliwa kimataifa, Alassane Ouattara ametoa wito wa kuwepo amani nchini humo baada ya mpinzani wake Laurent Gbagbo kukamatwa hapo jana na vikosi vya Ufaransa.

https://p.dw.com/p/10rzp
Rais wa Cote d'Ivoire anayetambuliwa kimataifa, Alassane OuattaraPicha: AP

Hata hivyo kiongozi huyo anakabiliwa na jukumu kubwa la kuiunganisha tena nchi hiyo iliyotumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Katika hotuba yake aliyoitoa jana jioni kupitia kituo chake cha televisheni cha TCI, Alassane Ouattara amewataka wananchi kujizuia na njia zozote za kulipiza kisasi na kutoendeleza mapigano, huku akitaka kuwepo kwa wakati mpya wa matumaini.

Amesema nchi hiyo imeufunga ukurasa wa maumivu na hivyo kuwa historia na kuwahimiza vijana wapiganaji kuweka chini silaha zao na ameadhidi kurejesha amani na usalama katika taifa hilo. Akizungumzia kuhusu hatua ya Gbagbo na wasaidizi wake wanaoshikiliwa kufikishwa katika vyombo vya sheria, Ouattara alisema, ''Ili kuweza kuunda taifa linalofuata haki, nitamuomba waziri wa sheria aanze uchunguzi dhidi ya Laurent Gbagbo, mkewe na watu wake wa karibu.''

Ban Ki Moon Pressekonferenz New York
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moonPicha: Picture Alliance/Photoshot

Lakini pia ameahidi kutumia mfumo wa Afrika Kusini wa kuanzisha tume ya ukweli na maridhiano ili kushughulikia uhalifu wote na ukiukaji wa haki za binaadamu. Aidha, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amemtaka Ouattara kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ili kusaidia katika maridhiano kwenye nchi hiyo iliyogawanyika.

Wakati huo huo, msemaji wa Gbagbo, Alain Toussaint leo amevishutumu vikosi maalum vya Ufaransa kwa kufanya mapinduzi ya kijeshi nchini Cote d'Ivoire kwa niaba ya Ouattara. Kwa mujibu wa msemaji huyo aliyekuwa akizungumza na waandishi habari mjini Paris, kukamatwa kwa Gbagbo ni mapinduzi ya kijeshi ambayo lengo lake si jingine bali kudhibiti maliasili za nchi hiyo.

Elfenbeinküste Laurent Gbagbo Verhaftung
Laurent Gbagbo kama anavyoonekana baada ya kukamatwaPicha: dapd

Toussaint ametaka Gbagbo pamoja na familia yake waachiliwe huru. Hata hivyo, msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ufaransa, Bernard Valero amekanusha madai hayo. Na taarifa za hivi punde zinasema kuwa Waziri Mkuu wa Ufaransa, Francois Fillon amesema hakuna haja ya vikosi vya nchi hiyo kuendelea kubakia Cote d'ivoire kwa kipindi kirefu.

Ama kwa upande mwingine Umoja wa Mataifa leo umeteua timu ya wataalamu watatu ambao watachunguza tuhuma zote za ukiukaji wa haki za binaadamu nchini Cote d'Ivoire. Taarifa ya Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa timu hiyo itaongozwa na Vitit Muntabhorn, Profesa wa sheria kutoka Thailand.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wameuambia mkutano mjini Geneva, kwamba hadi sasa watu 536 wameuawa nchini humo tangu mwishoni mwa mwezi Machi. Mbali na vifo hivyo, watu wengine zaidi ya 800,000 wameyakimbia makaazi yao.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE,AFP)
Mhariri:Abdul-Rahman, Mohammed