1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ouattara atazamia kuingia Ikulu karibuni

Admin.WagnerD6 Januari 2011

Wakati jitihada za kuutatua mgogoro wa Cote d'Iviore kidiplomasia zikiendelea, mtu anayeaminiwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa Novemba 2010, Allasane Ouattara, anasema anajitayarisha kuchukua madarakani muda wowote.

https://p.dw.com/p/zuCV
Alassane Ouattara, mtu anayetambuliwa na Jumuiya ya Kimataifa kama mshindi halali wa uchaguzi wa Novemba 2010, nchini Cote d'Ivoire
Alassane Ouattara, mtu anayetambuliwa na Jumuiya ya Kimataifa kama mshindi halali wa uchaguzi wa Novemba 2010, nchini Cote d'IvoirePicha: AP

Alassane Ouattara, anajenga matumaini kwamba, leo-kesho ataingia kwenye Ikulu ya mjini Abdijan, na kwamba baada ya hapo mambo yatarudi kuwa mazuri nchini mwake, kama zile siku Cote d'Iviore ilipotambuliwa kama kigezo cha maendeleo cha Magharibi ya Afrika.

Anasema kwamba anajitayarisha kumpokea Laurent Gbagbo na kumpa hakikisho la usalama wake na namna ambavyo anaweza kuishi Cote d'Iviore, "lakini ni baada ya yeye tu kutambua kwamba alishindwa uchaguzi na mimi ndiye rais mteule, na kwamba ananiwacha niingie ofisini."

Lakini, Ouattara, kuliko mwengine yeyote, anajua kuwa kazi si rahisi kiasi hicho. Leo hii (6 Januari 2011) alinukuliwa akisema kwamba, ana taarifa za uhakika kuwa Gbagbo, alipanga vurugu za baada ya uchaguzi, ambazo hadi sasa zimeshagharimu maisha ya kiasi watu 200.

"Laurent Gbagbo ana damu mikononi mwake. Amekuwa akitumia mamluki kufanya mauaji dhidi ya raia." Ouattara amekiambia kituo cha redio cha Europe 1 cha Ufaransa.

Laurent Gbagbo, kiongozi anayeng'ang'ania madaraka nchini Cote d'Ivoire
Laurent Gbagbo, kiongozi anayeng'ang'ania madaraka nchini Cote d'IvoirePicha: AP

Ouattara ameongeza kwamba, tayari ameshamuandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, kuitaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kutuma timu yake ya uchunguzi na tayari amejibiwa kwamba uchunguzi huo utaanza katika siku za karibuni.

Kauli hii ya Ouattara, inakuja katika wakati ambao jitihada za kimataifa kumtaka Gbagbo aondoke kwa hiari yake madarakani, zikiendelea. Tayari ujumbe wa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika ya Magharibi, ECOWAS; na ule wa Umoja wa Afrika, AU, umeshakutana mara mbili na Gbagbo na Ouattara ndani ya wiki mbili zilizopita.

Mjumbe maalum wa AU katika mazungumzo hayo, Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, na rais wa Kamisheni ya ECOWAS, Victor Gbebo, bado hawajaondoa uwezekano wa nguvu za kijeshi kutumika kumng'oa Gbagbo madarakani, lakini wote wamekubaliana kutumia kila fursa ya kidiplomasia iliyopo kabla ya kufikia hatua hiyo.

Mwenyewe Ouattara, anaamini kwamba shinikizo hili la kimataifa ni kubwa mno kwa Gbagbo kuweza kulihimili kwa muda mrefu, na kwamba haitachukuwa muda mrefu kwa mpinzani wake huyo kung'amua kwamba, kile anachopaswa kukifanya ni kukabidhi madaraka akataka asitake.

"Shinikizo ni kubwa mno. Gbagbo anataka kuleta mchezo, lakini mchezo wake hautadumu sana." Amesema Ouattara.

Wakati huo huo, kikosi cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa kilichopo nchini Cote d'Ivoire, MINUCI, kimeliandikia rasmi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka waongezwe wanajeshi 2000 kwenye kikosi chao, licha ya Gbagbo kutaka kikosi hicho kiondoke haraka nchini mwake.

Cote d'Ivoire imekuwa katika mkwamo wa kisiasa tangu uchaguzi wa marudio wa mwishoni mwa Novemba 2010, ambao Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo na waangalizi wa kimataifa wanasema, Ouattara ndiye aliyeibuka mshindi, lakini Mahakama Kuu ya nchi hiyo ikamtangaza Gbagbo kuwa rais.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters

Mhariri: Josephat Charo