1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ouattara: Gbagbo atang'oka tu

Oummilkher Hamidou21 Januari 2011

Viongozi wa bara la Afrika wameingia mbioni kumshinikiza Laurent Gbagbo akubali kuondoka kwa hiari madarakani, huyu rais anayetambuliwa kimataifa, Alassane Ouattara, akihimiza hata nguvu zitumike ikilazimika.

https://p.dw.com/p/100Q2
Rais Laurent GbagboPicha: Picture-Alliance/dpa

Rais wa Côte d`Ivoire anayetambuliwa kimataifa, Alassane Dramane Ouattara amesisitiza umuhimu wa kutumiwa nguvu ikilazimika, kumng'owa madarakani rais aliyemaliza muda wake Laurent Gbagbo. Ouattara amesema hayo wakati wa mahojiano pamoja na mwandishi wa Deutsche Welle mjini Abidjan.

Mbali na mwandishi huyo wa Deutsche Welle, Ouattara alizungumza pia na waandishi wa Shirika la Habari la Reuters na kudai hatua kali zichukuliwe. Amefahamisha hata hivyo vikwazo vya kiuchumi pindi vikichukuliwa basi vimlenge Gbagbo tuu na na washirika wake na sio raia wa kawaida wa nchi hiyo inayozalisha kakao kwa wingi kabisa ulimwenguni.

Elfenbeinküste / Ouattara / Odinga
Alassane Ouattara na mjumbe wa Umoja wa Afrika Raila OdingaPicha: AP

Akiulizwa kwa muda gani mgogoro huu utaendelea, na kama ukiselelea ataendelea kusalia katika hoteli ya Golf, Ouattara amesema kuwa haamini kuwa mgogoro hu utadumu mud mrefu.

"Nimeshasema na ninasema tena, lengo letu ni kuona hali inarejea kuwa ya kawaida kabla ya mwisho wa mwezi huu. Na ninaamini hivyo ndivyo itakavyokuwa. Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) imesema wazi kabisa, kwamba Laurent Gbagbo lazima ang'oke madarakani. Hayo yamesemwa tangu Disemba 7 iliyopita - wiki sita zimeshapita sasa. Ni sawa kwamba ECOWAS ina muongozo wake na hivi sasa pia viongozi wa kijeshi wanakutana mjini Bamako. Baadae watakuja Bouake kutuarifu. Lakini na sisi pia tunajitahidi upande wetu katika sekta ya kidiplomasia na fedha ili kuhakikisha Laurent Gbagbo anaondoka madarakani. Hawezi peke yake kushindana na ulimwengu mzima." Alisema Ouattara.

Elfenbeinküste UN
Vikosi vya Umoja wa mataifa vinapiga doria mjini AbidjanPicha: AP

Wakati huo huo, Waziri Mkuu mteule wa Côte d'Ivoire, Guillaume Sorro, jana (20 Januari 2011) alikwenda Togo na Burkinafaso, katika juhudi za kuwatanabahisha viongozi wa nchi za Afrika ya Magharibi wazidi kumtia kishindo Gbagbo.

Wakuu wa kijeshi wa ECOWAS walisema baada ya mkutano wao mjini Bamako, Mali, kuwa wako tayari, hata kama wanaendelea na maandalizi.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika katika mazungumzo hayo, Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, yuko Afrika Kusini kwa mazungumzo na Rais Jacob Zuma baada ya kushindwa juhudi zake mjini Abidjan.

Wakati haya yakitokea, Tume ya Umoja wa Mataifa nchini Côte d'Ivoire imesema kiasi ya raia 29, 000 wamekimbilia Liberia na kukimbia machafuko yaliyozuka baada ya uchaguzi wa mwishoni mwa mwaka jana., huku watu wengine 260 wakiwa wameshauwawa kufuatia machafuko hayo.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP, Reuters
Mpitiaji: Mohammed Abdul-Rahman