1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSenegal

Sonko, Mwanasiasa wa upinzani nchini Senegal aachiwa huru

Lilian Mtono
15 Machi 2024

Mwanasiasa maarufu wa upinzani nchini Senegal Ousmane Sonko, ameachiliwa huru siku chache kabla ya uchaguzi wa rais nchini humo uliopangwa kufanyika Machi 24.

https://p.dw.com/p/4dXMP
Mpinzani nchini Senegal, Ousmane Sonko
Mwanasiasa maarufu wa upinzani nchini Senegal Ousmane Sonko akizungumza kwenye moja ya mikutano yake ya hadhara mjini Dakar Juni 8, 2022. Picha: Seyllou/AFP

Wakili wa Sonko Bamba Cisse ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba mteja wake aliyekuwa anazuiliwa gerezani pamoja na mshirika wake mkubwa Bassirou Diomaye Faye wameachiliwa huru.

Faye tayari ameteuliwa kuwa mgombea wa upinzani baada ya Sonko kuzuiwa kuwania nafasi hiyo na haikujulikana mara moja namna hatua hiyo inavyoweza kuwa na athari kwenye uchaguzi huo.

Sonko aliyeshika nafasi ya tatu katika uchaguzi wa mwaka 2019 anachukuliwa kuwa kitisho kikubwa kwa chama cha Rais Macky Sall, ambaye hagombei tena baada ya maandamano makubwa ya upinzani ya kumpinga na yaliyodumu kwa miezi kadhaa.

Picha ya pamoja | Macky Sall na Ousmane Sonko
Picha ya wapinzani wakubwa wa kisiasa nchini Senegal, Rais Macky Sall (kushoto) na mpinzani wake mkuu Ousmane Sonko aliyekuwa akizuiliwa gerezaniPicha: Presidency of Senegal / Handout/AA/picture alliance | Seyllou/AFP/Getty Images

Wagombea wa urais nchini Senegal walianza kampeni za uchaguzi siku ya Jumamosi kufuatia wiki za machafuko kote kwenye taifa hilo la Afrika Magharibi baada ya Rais Macky Sall kutangaza kusogeza mbele tarehe ya uchaguzi.

Soma pia:Wito wa kumwachilia mgombea urais wa Senegal kutoka gerezani 

Wanasiasa hawa wameachiliwa muda mfupi baada ya Rais Sall kuiambia serikali yake kuanza mara moja utekelezaji wa sheria ya msamaha mara baada ya kuchapishwa rasmi. 

Sall alipendekeza muswada utakaosamehe vitendo vilivyohusika na maandamano ya kisiasa tangu mwaka 2021.