1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pacquiao atangaza kuwa astaafu Aprili

22 Januari 2016

Bondia wa Ufilipino Manny Pacquiao amethibitisha kuwa pigano lake la Aprili 9 mwaka huu dhidi ya Tim Bradley litakuwa lake la mwisho

https://p.dw.com/p/1HiKf
Manny Pacquiao
Picha: Getty Images/C. Hyde

Pacquiao, aliye na umri wa miaka 37 na Bradley mwenye umri wa miaka 32, watakutana katika ukumbi wa MGM Grand Garden mjini Las Vegas, eneo ambalo wamekutana katika mapigano yao mawli yaliyopita.

Pacman kama anavyofahamika na mashabiki wake, ni mbunge katika nchini Ufilipino na amesema anataka sasa kuitumikia nchi yake kikamilifu "niliamua kuwa na pigano la mwisho kwa sbabu nimekuwa katika ndondi kwa zaidi ya miaka 25. Umekuwa muda mrefu. Nina jukumu jingine zuri, jukumu kubwa nchini mwangu, kuwasaidia watu. Na vitu vizuri vimefanyika. Nilianza ndondi kumsaidia mamangu, familia yangu na ninamaliza ndondi kuisaidia nchi yangu. Kwa hiyo ni vizuri".

Manny Pacquiao lands a punch against Floyd Mayweather
Manny Pacquaio alishindwa na Floyd MayweatherPicha: Reuters

Pacquiao anasemekana kuwa atagombea kiti cha useneta katika nchi hiyo ya Asia baadaye mwaka huu. Bradely alimpiku Pacman kwa njia ya utata wakati mabondia hao walikutana kwa mara ya kwanza 2012 lakini Mfilipino huyo alilipiza kisasi katika pigano la marudiano mwaka wa 2014, kupitia wingi wa pointi na hivyo kutwaa tena taji la WBO welterweight. Pacman anaeleza mbona anakutana na Bradely kwa mara ya tatu "Niliamua kupigana tena na Tim Bradley kwa sababu ya namna mapigano yetu mawili yalivyokuwa. kumekuwa na maswali mengi na mashaka kutoka kwa mashabiki hivyo niliamua kuwa na pigano la tatu ili kuyajibu maswali hayo. Na bila shaka naamini kuwa ataleta ushindani mkali ulingoni kwa sababu tuliona katika pigano lake la mwisho ameimarika sana".

Pigano hilo la Aprili litakuwa la kwanza kwa Pacquaio tangu aliposhindwa na Mmarekani Floyd Mayweather Jr. kupitia wingi wa pointi, miezi saba iliyopita. Bradley anasema ana yuko tayari kupambana na Pacman kwa mara ya tatu "Naamini kuwa mapigano hayo mawili yalifanyika naman yalivyofanyika. lakini nadhani hili litakuwa tofauti. nadhani ukweli kwamba niko na Teddy Atlas, kwamba nimeimarika zaidi, nahisi nina faida kubwa kabla ya pigano hili. nahisi nitakuwa na ushindani mkali wakati tukipanda ulingoni. Najiskia ni kama sikuwahi kuwa na mapigano hayo mawili. kwa hiyo huyu ni Bradley mpya kabisa, kiakili, kimwili, na nasubiri siku hiyo".

Pacquaio alikuwa na maumivu ya bega lake la kulia wakati wa pigano lake na Mayweather na akafanyiwa upasuaji siku nne baadaye

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Mohamed Khelef