1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pakistan inawasaka wahusika wa shambulizi la kigaidi

28 Machi 2016

Maafisa nchini Pakistan wameanzisha msako mkali wa kuwatafuta watu waliohusika na shambulizi la kujitoa mhanga lililowalenga Wakristo na kuwaua zaidi ya watu 70 na kuwajeruhi wengine 300 mjini Lahore, Pakistan.

https://p.dw.com/p/1IKjn
Paksitan Lahore Anschlag Kinderspielplatz Selbstmordattentat Polizei
Picha: Getty Images/AFP/F.Naeem

Msemaji wa jeshi la Pakistan, Asim Bajwa amesema msako huo umeanza ili kuwafikisha katika mkono wa sheria waliohusika na mauaji ya watu wasio na hatia. Naibu Inspekta Mkuu wa polisi, Haider Ashraf, ameiambia DW kwamba vikosi vya usalama vimeimarisha ulinzi wa usalama kuzunguka Lahore, mji mkuu wa jimbo la Punjab, kwa sababu wako katika hali ya vita.

''Tunatumia mashirika maalum kama vile ya kupambana na ugaidi, kufanya uchunguzi. Kuna masuala kadhaa yanayotuelekeza kwa mshambuliaji aliyejitoa mhanga na watu walio nyuma ya shambulizi hili,'' Inspekta Ashraf

Mshambuliaji aliyejitoa muhanga alijiripua jana kwenye mji huo katika bustani ya mapumziko ya Gulshan-i-Iqbal, ambako Wakristo wengi walikuwa wamekusanyika kusherehekea sikukuu ya Pasaka. Wengi wa waliouawa ni wanawake na watoto.

Waokozi wakiondoa miili ya wahanga
Waokozi wakiondoa miili ya wahangaPicha: Getty Images/AFP/A. Ali

Kundi la Jamaat-ul-Ahrar lililojitenga na Taliban, limekiri kuhusika na shambulizi hilo, likisema lilikuwa likiwalenga hasa Wakristo. Msemaji wa kundi hilo, Ehsanullah Ehsan, amesema shambulizi hilo linatoa ujumbe kwa Waziri Mkuu wa Pakistan, Nawaz Sharif, kwamba wameingia Lahore na kamwe hawezi kuwazuia. Pakistan ni taifa lenye Waislamu wengi, lakini idadi ya Wakristo ni zaidi ya milioni mbili.

Serikali yatangaza siku tatu za maombolezo

Serikali ya jimbo la Punjab leo imetangaza siku tatu za maombolezo, huku bendera ya taifa ikipepea nusu mlingoti na taasisi zote za elimu kwenye mji wa Lahore, zimefungwa. Shambulizi katika jimbo hilo, sio la kawaida kwa sababu ni moja kati ya majimbo tajiri na yenye utulivu.

Pakistan imekuwa ikijitahidi kupambana na uasi wa Taliban pamoja na ghasia za kidini. Wakati makundi ya Taliban Pakistan na Jamaat-ul-Ahrar yakifanya mashambulizi kadhaa dhidi ya vikosi vya usalama na serikali, pia mara nyingi yamekuwa yakiwalenga Wakristo na Waislamu wa madhehebu ya Kishia.

Viongozi wengi wakiwemo viongozi wa Kikristo pamoja na Waziri Mkuu Nawaz Sharif, wamelaani vikali shambulizi hilo. Nawaz leo amewatembelea majeruhi wa shambulizi hilo waliolazwa hospitalini pamoja na familia zao.

Waziri Mkuu wa Pakistan, Nawaz Sharif na Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-Moon
Waziri Mkuu wa Pakistan, Nawaz Sharif na Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-MoonPicha: Reuters/E. Munoz

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon amelaani vikali shambulizi hilo akisema ni ugaidi unaotisha na ametaka wahusika waadhibiwe haraka kwa mujibu wa sheria. Ban ambaye ametoa salamu zake za rambirambi kwa wahanga na familia zao na kuonyesha mshikamano, ameitolea wito serikali ya Pakistan kuchukua hatua kuhakikisha usalama wa kila mmoja, zikiwemo jamii za watu wachache wanaoishi nchini humo.

Naye mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Malala Yousafzai, amelaani shambulizi hilo huku akiitaka Pakistan na dunia nzima kuungana. Katika mtandao wake wa Twitter, Malala ameandika kwamba maisha ya kila mtu yana thamani na lazima yaheshimiwe na kulindwa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTR,AFP,DPA
Mhariri: Josephat Charo