1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Palestina kuwasilisha tena azimio la kudai taifa huru

5 Januari 2015

Mzozo kati ya Wapalestina na Israel wafukuta wakati Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Wapalestina akisema atawasilisha upya kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa azmio lenye kutaka kuanzishwa kwa taifa la Palestina.

https://p.dw.com/p/1EFGI
Bendera ya Wapalestina.
Bendera ya Wapalestina.Picha: picture-alliance/dpa/I. Langsdon

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu naye amesema nchi yake haitokubali kuachia wanajeshi wake waburuzwe kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu kwa mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu.

Rasimu ya azimio ambalo linaitaka Israel iaache kuikalia kwa mabavu ardhi ya Wapalestina katika kipindi kisichozidi miaka mitatu limegonga ukuta wiki iliopita wakati lilipowasilishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo wajumbe wanane kati ya kumi na tano wa baraza hilo waliunga mkono lakini kulikuwa na kasoro ya kura moja iliokuwa ikihitajika kuweza kupitishwa kwa azmio hilo.

Marekani na Australia zilipiga kura ya kulipinga azimio hilo lilipowasilishwa Jumanne iliopita wakati wajumbe wa nchi nyengine tano hawakushiriki kupiga kura.Kutokana na kasoro ya kura hiyo moja ilimaanisha kwamba Marekani ilikuwa haina haja ya kutumia kura yake ya turufu.

Akizungumza wakati wa kufunguwa sherehe za maonyesho kuhusu Jerusalem hapo Jumapili mjini Ramallah Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas amesema Wapalestina wataliwasilisha tena azimio hilo kwa baraza la Usalama.

Azimio la Wapalestina halikushindwa

Abbas amekaririwa akisema "Hatukushindwa.Baraza la Usalama limetuangusha.Kwa nini tusifanye hivyo ? Pengine tukafanya hivyo baada ya wiki moja.Tunaliangalia suala hilo na washirika wetu hususan Jodan kwa sababu wako karibu nasi na wanatujali. Tutaliwasilisha tena azmio hilo iwe mara ya nne au hata ya tano.Hatutoachana na hatua hiyo hadi hapo baraza la usalama litakapotukubalia."

Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Wapalestina.
Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Wapalestina.Picha: picture-alliance/dpa/Alaa Badarneh

Wapalestina walielezea kuvunjika kwao moyo sana na kusema kwamba Nigeria ilijitowa dakika za mwisho licha ya kuahidi kupiga kura ya kuliunga mkono azimio hilo kwa sababu ya kile inachoonekana kuwa shinikizo au ahadi kutoka Marekani.

Baada ya kukataliwa kwa azimio hilo Rais Abbas aliwasilisha nyaraka za kujiunga na mahakama ya kimataifa ya uhalifu yenye makao yake makuu mjini The Hague Uholanzi hapo Ijumaa na siku moja baadae Israel imesema inasitisha uhamishaji wa mamilioni ya dola mapato ya kodi kwa Wapalestina ambayo huyakusanya kila mwezi kwa niaba ya Wapalestina.

Israel yawaonya Wapalestina

Waziri Mkuu wa Israel Banjamin Netanyahu amesema hapo Jumapili mjini Jerusalem kabla ya kuanza kwa mkutano wake wa baraza la mawaziri kwamba serikali ya Wapalestina imejiweka kwenye mkondo wa mgongano na Israel kwa kutaka kujiunga na mahakama ya ICC.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanjahu.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanjahu.Picha: Reuters/G. Tibbon

Netanyahu amesema "Serikali ya Wapalestina imeamuwa kukabiliana na taifa la Israel na hatutokaa tu kimya bila ya kuchukuwa hatua.Hatutoruhusu wanajeshi na makamanda wa Israel waburuzwe kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu mjini The Hague. Viongozi wa serikali ya Wapalestina ndio wanaostahiki kukabiliwa na mkono na sheria kwa kuuda ushirika na kundi la Hamas la wahalifu wa kivita."

Israel inaona kampeni ya kidiplomasia ya Abbas kuwa ni jaribio la kuiweka kando nchi hiyo na kuepuka mazungumzo ya moja kwa moja na nchi hiyo na kufikia maridhiano.Israel imetaka kufufuliwa kwa mazungumzo hayo ya amani ya moja kwa moja lakini imekataa wito wa Abbas wa kusitisha ujenzi wa makaazi ya walowezi ya Kiyahudi kama masharti ya kufanyika kwa mazungumzo hayo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa

Mhariri : Iddi Ssessanga