1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

John Kerry ataka ufafanuzi zaidi juu ya hatima ya rais Assad

mjahida23 Machi 2016

Pande mbili zinazohasimiana zinazoshiriki mazungumzo ya amani mjini Geneva, Uswisi zimebadilishana nyaraka zinazoainisha nafasi muhimu kwa kila upande katika mazungumzo hayo.

https://p.dw.com/p/1II52
Schweiz Syrien Konferenz in Genf Bashar al-Jaafari
Picha: Getty Images/AFP/Fabrice Coffrini

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria Steffan de Mistura amesema nyaraka hizo zinaweza kutumiwa kujua iwapo kuna matakwa sawa kati ya serikali ya Syria na upinzani, kabla ya kuahirishwa mazungumzo hayo baadaye wiki hii.

"Kila upande unapaswa kuonyesha kuwa una nia ya kweli ya kupata suluhu ya kisiasa katika mzozo huo ulioingia mwaka wake wa tano," alisema de Mistura.

Mazungumzo hayo yanatarajiwa kuahirishwa siku ya Alhamisi na kuanza tena baadaye mwezi Aprili. Hapo jana Staffan de Mistura alisema mashambulizi yaliyofanyika mjini Brussels yaliyosababisha mauaji ya watu 31 yanaonyesha umuhimu wa kutafuta suluhu ya kudumu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe Syria yaliyosababisha mauaji ya watu 270,000 kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa.

Schweiz Syrien-Friedensgespräche in Genf
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria Steffan de MisturaPicha: Reuters/R. Sprich

"Tunahitaji kuuzima moto wa vita nchini Syria, tunahitaji kupata suluhu ya kisiasa, ili kuhakikisha sote tunamakinika na wasyria pia wanamakinika ili kwa pamoja tuangalie kitisho cha kila mmoja ulaya, duniani nchini Syria na kwengineko," aliongeza kusema de Mistura.

Waziri John Kerry wa Marekani kuijadili Syria pamoja na rais Vladimir Putin wa Urusi

Huku hayo yakiarifiwa Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry anatarajiwa kuelekea Urusi kukutana na rais Vladimir Putin pamoja na Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergey Lavrov kuzungumzia makubaliano ya kusitisha mapigano Syria na namna ya kuwaadhibu wale watakaokiuka makubaliano hayo.

Siku ya Jumatatu Urusi iliionya Marekani kuwa itaanza kuwashughulikia wale watakaokiuka makubaliano ya kusitisha mapigano Syria, iwapo Marekani itakataa kushirikiana juu ya adhabu inayohitaji kupewa wakiukaji hao.

USA John Kerry in Washington
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John KerryPicha: Getty Images/M. Wilson

Kando na hilo kulingana na maafisa wa Marekani, katika mazungumzo hayo Waziri Kerry atatafuta ufafanuzi zaidi kutoka kwa Putin na Lavrov kujua msimamo wa Urusi juu ya kipindi cha mpito wa kisiasa nchini Syria hasa juu ya hatima ya rais Bashar al Assad.

Wakati huo huo kamati ya Kimataifa ya msalaba mwekundu imesema msafara wa malori 27 umepeleka chakula na misaada mengine katika maeneo yaliyozingirwa ya Al-Houla karibu na mji wa Syria wa Homs. Vikosi vya serikali ya Syria vimekuwa vikizuwiya misaada kufikishwa katika eneo hilo kuanzia mwezi May mwaka 2012. Lakini hata baada ya misaada kuanza kufikishwa huko bado upinzani unaishutumu serikali ya rais Bashar al Assad kuendelea kuyazingira maeneo mengine nchini Syria.

Mwandishi:Amina Abubakar/AP

Mhariri:Josephat Charo