1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pande hasimu Yemen zajiandaa kusitisha mapigano

Mjahida8 Desemba 2015

Serikali ya Yemen imesema pande mbili zinazohasimiana zinajiandaa kuanza wiki moja ya usitishwaji mapigano wakati mazungumzo ya amani yanayoongozwa na Umoja wa Mataifa yakiendelea Uswisi.

https://p.dw.com/p/1HJRS
Rais wa Yemen Abed Rabbo Mansur Hadi
Rais wa Yemen Abed Rabbo Mansur HadiPicha: Reuters/F. Al Nasser

Kwa miezi kadhaa sasa Umoja wa mataifa umejaribu kuwaleta pamoja wanajeshi tiifu kwa serikali ya Yemen na waasi wanaoungwa mkono na Iraq, ili kumaliza mapigano yaliyosababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulisukuma taifa hilo katika mgogoro wa kibinaadamu.

"Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya serikali na waasi yanapaswa kuanza kutekelezwa kuanzia tarehe 15 Desemba na majadiliano kuanza moja kwa moja," alisema waziri wa mambo ya nje wa Yemen Abdel Malak al-Mekhlafi alipozungumza na shirika la habari la AFP.

Kwa upande wake mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Ismail Ould Cheikh Ahmed, amesema kusitishwa mapigano ambayo yameendelea kushika kasi tangu muungano unaoongozwa na Saudi Arabia ulipoanza kuwashambulia waasi mwezi Machi, ni muhimu hasa kwa wale waliojikuta ndani ya mapigano hayo.

watu waliyotiifu kwa waasi wa Houthi
watu waliyotiifu kwa waasi wa HouthiPicha: Reuters/K. Abdullah

Ould Cheikh ameongeza kuwa wajumbe wa pande tatu watahudhuria mazungumzo hayo yatakayofanyika nje ya mji wa Geneva na kudumu kwa muda ambao bado haujajulikana.

Wajumbe wa pande tatu watahudhuria mazungumzo ya amani Geneva

Mazungumzo hayo yatalenga maeneo manne muhimu, ikiwemo usitishwaji wa kudumu wa mapigano, na kuondolewa makundi yaliojihami katika maeneo wanayoyadhibiti. Mikakati ya kujiamini utakuwa suala jengine litakalojadiliwa ikiwemo kutanua uingiliaji katika maeneo kunakohitajika misaada ya kiutu ambapo wafanyakazi wa kutoa misaada hiyo wameuwawa na kutekwa nyara.

Wajumbe hao watajaribu kutafuta mustakbal wa kisiasa nchini Yemen, taifa lililokumbwa na mgogoro mbaya tangu wapiganaji walipoudhibiti mji mkuu sanaa hatua iliyosababisha serikali kukimbilia Saudi Arabia kabla ya kurejea katika mji wa pili kwa ukubwa wa Aden mwezi uliyopita.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Ismail Ould Cheikh Ahmed
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Ismail Ould Cheikh AhmedPicha: picture-alliance/dpa/M. Trezzini

Ujumbe utakaohudhuria mazungumzo hayo utawajumuisha wawakilishi kutoka serikali ya rais Abedrabbo Mansour Hadi, waasi wa Houthi, na maafisa wa bunge waliotiifu kwa rais wa zamani Ali Abdullah Saleh.

Kulingana na chanzo cha habari kutoka baraza la mawaziri la rais Hadi, usitishwaji huo wa mapigano utadumu kwa siku saba, kama ilivyoandikwa katika barua iliyotumwa na rais Hadi kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo bado waasi hawajathibitisha kama wataheshimu uamuzi huo wa kusitishwa mapigano, lakini mjumbe wa Umoja wa Mataifa Ould Cheikh Ahmed amesema anauhakika waasi hao watakuepo katika mazungumzo ya kutafuta amani ya Yemen.

Muandishi Amina Abubakar/AFP/Reuters

Mhariri Yusuf Saumu