1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pande nne kuzungumzia amani , Mashariki ya kati.

Charles Mwebeya21 Februari 2007

Mkutano wa pande nne kutafuta amani ya mashariki ya kati unaaza leo mjini Berlin hapa ujerumani .

https://p.dw.com/p/CHJe
Waziri mambo ya nje Frank Walter Steinmeier wa ujerumani(kushoto)ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo akiwa na Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert.
Waziri mambo ya nje Frank Walter Steinmeier wa ujerumani(kushoto)ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo akiwa na Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert.Picha: AP

Ajenda kuu katika Mkutano huo unaozihusisha nchi za Marekani , Russia , Umoja wa ulaya na Umoja wa mataifa itakuwa ni makubaliano ya mgawanyo wa madaraka na uundwaji wa serikali ya kitaifa kati ya Rais Mahmud Abbas wa chama cha Fatah na kundi la Hamas.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Condoleeza Rice, atajaribu kuzishawishi pande nyingine katika mkutano huo kuitambua serikali inayotarajiwa ya umoja wa kitaifa ya mamlaka ya Palestina.

Kukubalika kwa serikali hiyo ya muungano wa mamlaka ya Palestina itategemea endapo Hamas itakubali na kuitambua Israel kama taifa , kuacha mashambulio ya kigaidi na kuheshimu mazungumzo hayo.

Vile vile Bi. Rice anahitaji washirika wa mazungumzo hayo kumuunga mkono Rais Mahmud Abbas katika utawala wake dhidi ya Hamas , chama chenye wabunge wengi katika bunge la Palestina.

Rais Abbas ambaye kwa hivi sasa anafanya ziara katika nchi za Ulaya, hapo jana aliwasili nchini Uingereza na pia atazitembelea Ufaransa na Ujerumani kwa kile kinachoonekana kama kutafuta uungwaji mkono dhidi ya Hamas.

Rais huyo wa mamlaka ya Palestina amesisitiza makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni mjini Macca, kati ya chama chake cha Fatah na Hamas yatatimiza masharti yaliyowekwa na pande hizo nne .

Pande nne zinazokutana hii leo mjini Berlin , zinalichukulia kundi la Hamas kama kundi la kigaidi , kutokana na msimamo wake wa kutoitambua Israel na kudaiwa kuendeleza ghasia katika eneo hilo la mashariki ya kati, Hatua iliyopelekea kusitisha misaada katika taifa la Palestina.

Wiki iliyopita Israel ilisema haitoitambua serikali yoyote ile ya Palestina itakayolihusisha kundi la Hamas.

Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert , alisema Rais George Bush naye ameungana na nchi yake katika msimamo huo.

Kwa upande wake ,Russia imetaka mazungumzo hayo kuangalia namna pande hizo zinatakavyojihusisha na serikali ya muungano baina ya chama cha Fatah na Hamas.

Mkutano huo vile vile utaangalia hali ngumu ya kiuchumi inayolikabili taifa la Palestina, na unategemewa kuridhia pendekezo la nchi za umoja wa ulaya kuendelea kutoa dola milioni 160 kama msaada wa kibanadam katika taifa la hilo.

Chini ya pendekezo hilo , Msaada huo wa kifedha wa umoja wa ulaya , utajenga taasisi za kiserikali chini ya Rais Abbas, hatua inayopelekea uwezekano wa kujenga taifa la Palestina.