Papa Francis akutana na kiongozi wa jeshi la Myanmar | Masuala ya Jamii | DW | 27.11.2017

Masuala ya Jamii

Papa Francis akutana na kiongozi wa jeshi la Myanmar

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis amekutana na kiongozi wa jeshi la Myanmar, siku ya kwanza ya ziara yake katika taifa hilo lenye idadi kubwa ya waumini wa madhebu ya Budha.

Myanmar Ankunft Papst Franziskus (Reuters/Osservatore Romano)

 

Papa Francis mwenye umri wa miaka 80, wa kwanza kuzuru Myanmar, alimkaribisha Jenerali Min Aung Hlang katika makazi ya askofu mkuu, kanisa la Mtakatifu Maria, katika mji mkuu Yangon, ambako mkuu huyo wa kanisa Katoliki atakaa wakati wa ziara yake.

Umoja wa Mataifa na Marekani zinalituhumu jeshi la Myanmar kwa kampeni ya safisha safisha ambayo imewalazimu Warohingya 620,000 katika jimbo la kaskazini la Rakhine kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh tangu mwezi Agosti mwaka huu. Ukandamizaji dhidi ya Warohingya ni suala linatakalozingatiwa sana katika ziara ya siku nne ya Papa Francis.

Msemaji wa makao makuu ya kanisa Katoliki, Vatican, Greg Burke, amesema wakati wa kikao cha dakika 15 Papa na mkuu wa majeshi wa Myanmar wamezungumzia jukumu kubwa la maafisa wa taifa hilo wakati huu wa kipindi cha mpito. Greg amesema mazungumzo hayo yalifuatiwa na mabadilishano ya zawadi huku Papa Francis akimpa jenerali Min medali ya kumbukumbu ya ziara yake Myanmar, na Min kwa upande wake akamkabidhi papa kifaa cha muziki  mfano wa boti na bakuli zuri la kutilia mchele.

Myanmar Ankunft Papst Franziskus (Reuters/Soe Zeya Tun)

Watu wakiwa wamejipanga barabara za Yangon kumkaribisha Papa Francis

Mapema leo Baba Mtakatifu Francis alilakiwa katika uwanja wa ndege wa mjini Yangon na watoto kutoka jamii mbalimbali ndogo waliokuwa wamevalia mavazi ya kupendeza, ambao walimpa maua na kukumbatiwa na kiongozi huyo.

Papa kukutana na Suu Kyi

Hapo kesho Papa Francis atakutana na kiongozi wa Myanmar, Aung San Suu Kyi, mshindi wa zamani wa tuzo ya amani ya Nobel, ambaye heshima yake imeshuka kwa kushindwa kuwatetea hadharani Warohingya.

Ziara ya Papa Francis ni fursa ya kihistoria kwa waumini wa kanisa Katoliki nchini Myanmar kumkaribia kiongozi wa kanisa lao. Waumini 700,000 wa kanisa hilo ni jumla ya asilimia moja ya wakazi milioni 51 wa Myanmar na wametawanyika katika pembe mbalimbali za taifa hilo, wengi wakikabiliwa na mizozo.

Takriban waumini 200,000 wa kanisa Katoliki wanamiminika mji mkuu Yangon kwa ndege, treni na magari kuhudhuria misa kubwa ya hadhara itakayofanyika siku ya Jumatano. Papa ataongoza misa mbili mjini Yangon kabla kuondoka.

Papa Francis anatarajiwa kwenda Bangladesh siku ya Alhamisi ambako amepangiwa kukutana na kundi la Waislamu wa jamii ya Rohingya katika mji mkuu, Dhaka. Nur Mohammed, imamu mwenye umri wa miaka 45 wa jamii ya Rohingya katika kambi ya wakimbizi wa Nayapara huko Cox Bazar, nchini Bangladesh, amesema anatumai papa ataiambia serikali ya Myanmar iwakubali Warohingya, iwape uraia na kumaliza ubaguzi wote dhidi yao.

Mwandishi:Josephat Charo/afpe/reuteres/afpe

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

Albanian Shqip

Amharic አማርኛ

Arabic العربية

Bengali বাংলা

Bosnian B/H/S

Bulgarian Български

Chinese (Simplified) 简

Chinese (Traditional) 繁

Croatian Hrvatski

Dari دری

English English

French Français

German Deutsch

Greek Ελληνικά

Hausa Hausa

Hindi हिन्दी

Indonesian Bahasa Indonesia

Kiswahili Kiswahili

Macedonian Македонски

Pashto پښتو

Persian فارسی

Polish Polski

Portuguese Português para África

Portuguese Português do Brasil

Romanian Română

Russian Русский

Serbian Српски/Srpski

Spanish Español

Turkish Türkçe

Ukrainian Українська

Urdu اردو