1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis awaombea baraka wanaowasaidia wakimbizi

Caro Robi25 Desemba 2015

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis katika ujumbe wake wa Krismasi, amewaombea baraka watu na serikali zinazowasaidia wahamiaji na wakimbizi duniani.

https://p.dw.com/p/1HTht
Picha: picture-alliance/AP Photo/G. Borgia

Katika hotuba ya kutoa ujumbe kwa ulimwengu, Papa Francis amewafariji wale wote wanaokimbia umasikini mkubwa na vita nchini mwao na kulazimika kufanya safari katika mazingira magumu mno yanayohatarisha maisha yao.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani amewaombea wale wote wanaojitolea kwa ukarimu wao kuwasaidia wahamiaji na wakimbizi kwa kuwapokea, kuwapa hifadhi na kuwasaidia kuyajenga upya maisha yenye hadhi kwao na kwa wapendwa wao.

Papa Francis amesema anaunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa katika kuikomesha mizozo inayoendelea Syria na Libya na kuongeza kuwa wanaomba kuwa makubaliano yanayofikiwa katika Umoja wa Mataifa, yatavikomesha haraka vita na kusadia katika kuboresha hali ya kibinadamu kwa watu wanaoteseka.

Papa aomba mizozo itafutiwe ufumbuzi haraka

Kama ilivyo desturi, ilipofika saa sita mchana, kiongozi huyo wa waumini bilioni 1.2 wa Kanisa Katoliki duniani, alisimama katika roshani ya Kanisa la Mtakatifu Petro kutoa ujumbe kwa ulimwengu ujulikanao kwa lugha ya kilatini Urbi et Orbi. Amewaombea wanaokumbwa na mizozo Mashariki ya Kati, Afrika na kwingineko duniani.

Papa Francis katika Roshani ya Kanisa la Mtakatifu Petro
Papa Francis katika Roshani ya Kanisa la Mtakatifu PetroPicha: Reuters/A. Bianchi

Baba Mtakatifu amesikitishwa na idadi kubwa ya wanawake na wanaume wanaonyimwa haki yao ya kuwa na maisha ya hadhi, watoto wanaosajiliwa kama wapiganaji, wanaoathirika na dawa za kulevya na kusema kama mtoto Yesu wanakumbwa na baridi, umaskini na kukataliwa.

Hata hivyo amesema alipozaliwa Mungu, matumaini na amani yamezaliwa na palipo na amani, hakuna nafasi ya chuki na vita. Ameombea amani kati ya Waisrael na Wapalestina, Syria, Libya. Iraq, Yemen, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Burundi, Sudan Kusini, Ukraine na Colombia.

Papa Francis pia amewakumbuka waathiriwa wa mashambulizi ya kigaidi ya Bamako, Paris na Tunis yaliyofanywa na makundi yenye itikadi kali na kuwahimiza wanasiasa kutafuta yaliyo mema na kuyalinda maisha ya watu wao.

Mzozo wa wakimbizi changamoto kubwa

Ujumbe wake kwa ulimwengu unakuja siku chache baada ya shirika la kuwashughulikia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR na shirika la kimataifa la uhamiaji IOM kusema zaidi ya wahamiaji na wakimbizi milioni moja wameingia barani Ulaya mwaka huu, ikiwa ni mara nne ya idadi ya wakimbizi walioingia Ulaya mwaka jana.

Wakimbizi wakielekea katika mpaka wa Macedonia
Wakimbizi wakielekea katika mpaka wa MacedoniaPicha: Getty Images/M. Cardy

Ujumbe wa kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani unakuja wakati ambapo bara la Ulaya linakabiliwa na changamoto kubwa ya kuushughulikia mzozo wa wakimbizi ambao haujapata kushuhudiwa tangu kumalizika kwa vita vya pili vikuu vya dunia.

Awali katika misa ya mkesha wa sherehe za Krismasi, Papa Francis alitoa ujumbe wa kuwahimiza wakristo kutopenda anasa za dunia ambazo ni kujilimbikizia mali, tamaa, uroho na ubadhirifu, bali watumie msimu huu wa kusherehekea Krismasi-kuzaliwa kwa Yesu Krsito kuonyesha huruma, kuwa wakarimu kukubali maadili ya maisha ya kawaida yenye uwiano na kuzichunguza nafsi zao.

Mwandishi: Caro Robi/dpa/Reuters/afp

Mhariri: Isaac Gamba