1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis awasili Bangladesh

Lilian Mtono
30 Novemba 2017

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Fransis amewasili Bangladesh kwa ziara ya siku tatu. Anatokea Myanmar ambako hakuzungumzia kwa uwazi mzozo wa Rohingya na kukabiliwa na ukosoaji mkubwa

https://p.dw.com/p/2oWRp
Papst Franziskus landet in Bangladesch
Picha: Getty Images/AFP/P. Singh

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Fransis amewasili mjini Dhaka,nchini Bangladesh kwa ziara ya siku tatu ambako suala la mzozo wa mamia kwa maelfu ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wanaokimbilia nchini humo, kutoka Myanmar linatarajiwa kuchukua nafasi kubwa katika majadiliano.

Rais wa Bangladesh Abdul Hamid alimpokea Papa Francis katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Hazrat Shahjalal, huku ulinzi ukiwa umeimarishwa kwa kiasi kikubwa. 

Papa Francis amewasili Bangladesh ikiwa ni taifa la pili kuzuru Barani Asia, baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku nne nchini Myanmar iliyogubikwa na ukosoaji dhidi ya uamuzi wake wa kutozungumzia mzozo wa Rohingya hadharani. 

Idadi ya waumini wa dini ya Kikristu ni chini ya asilimia 0.5, miongoni mwa waumini wa Kiislamu nchini Bagladesh, lakini katika miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakishambuliwa na Waislamu wenye msimamo mkali. 

Papa Francis amekabiliwa na ukosoaji kwa kushindwa kutaja "wachache".

Akiwa nchini Myanmar, kiongozi huyo wa kanisa alijikuta katika hali ngumu kidiplomasia, na kujiweka mbali na madai kuhusu jeshi  kuhusika na kampeni ya safishasafisha ya kikabila dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya, licha ya shinikizo la kumtaka kulikabili suala hilo zito hadharani.

Myanmar Rohingya "Refugee Boy"
Watoto katika kambi ya wakimbizi wa Rohingya ya Palong Khali iliyoko karibu na Cox's Bazaar, BangladeshPicha: Reuters/A. Abidi

Lakini pia hakutamka neno wachache katika ziara yake ya siku nne nchini Myanmar, ambapko pia aliongoza ibada mbili na kufanya mikutano ya faragha pamoja na Kiongozi wa Myanmar, Aung San Suu Kyi na mkuu wa jeshi lenye nguvu zaidi nchini humo Min Aung Hlaing.  

Hata hivyo Vatican kupitia msemaji wake Greg Burke jana jioni imepingana na ukosoaji dhidi ya Papa Francis kushindwa kuuzungumzia mzozo huo hadharani, kwamba kunadhihirisha ukosefu wa maadili ya kiuongozi.

Papa Francis aliwahi kuelezea wasiwasi wake kuhusu mateso wanayopitia Waislamu wa Rohingya, na aliliita kundi hilo lisilo na utaifa kuwa ni "ndugu".  

Lakini aliombwa kutolitaja kwa jina akiwa nchini Myanmar ili kuepusha uchokozi dhidi ya Wabuddha wenye msimamo mkali na kuitumbukiza jamii ya Kikristu nchini humo kuanza kulengwa.

Mkuu wa kamati ya uratibu wa ziara hiyo ya Papa nchini Bangladesh Komol Koriya amesema, kundi dogo la Warohingya linataraji kushiriki ibada itakayoongozwa na kiongozi huyo katika bustani ya Suhrawardy Udyan iliyoko mjini Dhaka.

Mwandishi: Lilian Mtono/DPAE/APE/AFPE
Mhariri:yusuf Saumu