1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa ziarani Uingereza

Mwadzaya,Thelma16 Septemba 2010

Baba Mtakatifu Benedict wa XVI anaanza ziara rasmi hii leo nchini Uingereza atakakokutana na Malkia Elizabeth wa Pili mjini Edinburg,Scotland

https://p.dw.com/p/PDDl
Baba Mtakatifu Benedict XVIPicha: AP

Hata hivyo ziara yake hiyo ya kihistoria imegubikwa na mivutano ya kidiplomasia baada ya msaidizi wake mmoja wa ngazi za juu kutoa matamshi yasiyoridhisha katika mkesha wa safari hiyo.Papa Benedict wa 16 anaizuru Uingereza wakati ambapo Kanisa Katoliki linajaribu kuisafisha sifa yake baada ya kufichuka kashfa ya kuwanajisi watoto kote ulimwenguni.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki ulimwenguni pia anakabiliwa na kibarua kigumu wakati wa ziara yake hiyo ya siku nne itakayompeleka Uingereza na Scotland ukizingatia uhusiano na kanisa la Kianglikana la Uingereza baada ya kauli zilizowatolea wito waumini wanaopinga kutawazwa kwa makasisi wa kike na walio mashoga kulihama.

5 Jahre Papst Benedikt XVI Ratzinger Kardinal Papst Johannes Paul 2002 Flash-Galerie
Hayati Baba Mtakatifu John Paul 11 akiwa na Kadinali Ratzinger wa Ujerumani(2002):Baba Mtakatifu wa sasaPicha: AP

Ziara ya kihistoria

Wakati wa ziara ya kwanza ya Kiongozi mkuu wa kanisa katoliki duniani miaka 28 iliyopita, Uingereza ilikuwa na shauku ya kumuona Baba Mtakatifu. Maelfu ya walijitokeza kumlaki Hayati Papa Yohane Paulo wa Pili. Lakini kwa wakati huu, mrithi wake, Papa Benedikto wa Kumi na Sita hatarajii kupata mapokezi kama hayo. Terry Sanderson wa Jumuiya ya Taifa ya Kidini, ni mmoja kati ya watu wengi wanaopanga kuipinga ziara hiyo wala sio,''Ukatoliki. tunampinga Papa. Na kwa kweli tunaungwa mkono kabisa na Wakatoliki ambao pia wanaoshangazwa na baadhi ya mafundisho ya Papa wa sasa na ukweli ni kwamba anaonekana kulirudisha Kanisa nyuma badala ya kufikiria siku zijazo.''alisema pamoja na wenzake wamejiunga na kundi linalojulikana kama 'Mpinge Papa'. Mwanaharakati wa haki za mashoga, Peter Tatchell pia ni mwanachama wa kundi hilo na anadai kuwa,''Wakatoliki wengi, pengine idadi kubwa ya Wakatoliki wa nchi hii hawakubaliani na jinsi Papa anavyopinga matumizi ya uzazi wa mpango, mapadri wanawake, usawa kwa mashoga na matumizi ya condom ili kuzuia kuenea kwa Virusi vya Ukimwi. Katika masuala yote haya, Wakatoliki wengi wamejitoa katika njia ya Baba Mtakatifu,''alifafanua.

Baadhi Wayahudi wanaoipinga ziara hiyo pia watajiunga na maandamano. Wanamshutumu Papa kwa kuwa na chuki dhidi ya Wayahudi na pia wamekasirishwa na uamuzi wake wa kumuondolea kizuizi cha kutengwa katika usharika mtakatifu askofu wa Uingereza ambaye alipinga mauaji ya kimbari dhidi ya Wayahudi. Lakini suala kubwa ni kuhusu kashfa za kuwanyanyasa kingono watoto iliyofanywa na baadhi ya mapadri wa Kanisa Katoliki.

Changamoto nyingine itakayomkabili Baba Mtakatifu ni kuhusu gharama zitakazotumika wakati wa ziara hiyo. Waandamanaji hao wanapinga suala kuwa wao kama walipa kodi watalipa baadhi ya gharama za Euro milioni 14 zilizotengwa kwa ajili ya ziara hiyo.

Flash Format Queen Elizabeth bei der UN UNO Vollversammlung in New York
Malkia Elizabeth wa Pili:Papa Benedict atakutana na mwenyeji wakePicha: AP

Robo tatu hawajali

Hata hivyo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Southwark, Mhashamu Peter Smith anasema amehakikishiwa kwamba hakutakuwa na matatizo yoyote na,''Hawana nia ya kuvuruga ziara hii, sio kwa upande wa kidini au kiraia. Na nadhani kwamba ziara hii itawafanya waachane na mawazo hayo. Namaanisha hakuna mtu yoyote anayeweza kuhakikisha kwamba hakutakuwa na matukio yasiyokuwa ya kawaida ambayo yanaweza kuiharibu ziara hii. Lakini hilo sio lengo,'' alieleza.

Wakati mtazamo ukiwa katika maandamano, imekuwa rahisi kusahau kwamba kwa Wakatoliki milioni nne au zaidi, wataifurahia ziara hiyo ya Baba Mtakatifu. Kura ya maoni inaonyesha kuwa wakati robo ya watu wa Uingereza wanaifurahia ziara hiyo na asilimia kumi wanaipinga, robo-tatu hawajali lolote kuhusu ziara hiyo.