1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papandreou kukutana na Rais Obama

Kabogo Grace Patricia9 Machi 2010

Kiongozi huyo wa Ugiriki ameitolea mwito Marekani kupambana na walanguzi wanaotaka kuisambaratisha safaru ya euro.

https://p.dw.com/p/MO78
Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou.Picha: AP

Waziri mkuu wa Ugiriki, George Papandreou, ameitolea mwito Marekani kupambana na walanguzi katika masoko ya fedha, huku kukiwa na taarifa zilizozagaa kwamba baadhi ya fedha za Marekani zimewekwa kando kwa ajili ya kuisambaratisha sarafu ya Euro.

George Papandreou hii leo anatarajiwa kukutana na Rais Barack Obama wa Marekani mjini Washington, baada ya kiongozi huyo wa Ugiriki kuelezea wasi wasi kwamba walanguzi wanahujumu jitihada zake za kuiondoa nchi yake katika tatizo kubwa la madeni. Papandreou, ambaye aliwasili nchini Marekani akitokea Ufaransa na Ujerumani, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kutafuta kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa, alitangaza mikakati yake itakayojaribu kupunguza nakisi katika bajeti yake kwa asilimia 12.7.

Taarifa zinaeleza kuwa fedha zimetengwa kwa ajili ya kuisambaratisha sarafu ya euro inayotumiwa na mataifa 16 ya Ulaya, ikiwemo Ugiriki. Hata hivyo, Papandreou alionya kuwa athari zitakazotokana na njama ya kuisambaratisha sarafu ya euro zitaiathiri pia Marekani na ametaka Ulaya na Marekani zishirikiane kupambana na walanguzi. Papandreou alisema, ''Ulaya na Marekani zinahitaji kushirikiana na kukataa walanguzi ambao wanataka tu kupata faida bila kujali athari kwenye mfumo mzima wa kiuchumi duniani, pamoja na athari za kibinaadamu katika kupotea nafasi za ajira na kuvurugika kwa mfumo wa malipo ya uzeeni.''

Aidha, taarifa ya Ikulu ya Marekani-White House imesema kuwa mazungumzo kati ya Papadreou na Rais Obama yatahusu zaidi masuala ya kiuchumi. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, viongozi hao watazungumzia mageuzi ya kifedha na hatua ya kuufufua uchumi.

Mkutano wa Rais Obama na Waziri huyo Mkuu wa Ugiriki unafanyika wakati Kamisheni ya Ulaya inajiandaa kutoa mapendekezo ya kuundwa kwa Shirika la Kimataifa la Fedha la Ulaya. Msemaji wa Kamisheni ya Umoja ya Ulaya ya uchumi na fedha, amesema taarifa zaidi ya jinsi shirika hilo litakavyofadhiliwa zitatolewa hadi ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu. Wakati huo huo, Papandreou anatarajiwa kuomba msaada wa kifedha kutoka kwa Marekani. Lakini serikali yake inayokabiliwa na migomo kufuatia wananchi kupinga hatua ya Ugiriki kupunguza matumizi yake ya fedha, imependekezea kuwa huenda ikaomba msaada kutoka Shirika la Kimataifa la Fedha-IMF- kama nchi washirika za Umoja wa Ulaya zitakataa kuisaidia.

Kwa upande  wake, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton, baada ya mazungumzo yake na Papandreou, alisema kiongozi huyo wa Ugiriki wala serikali ya nchi hiyo haijaomba msaada wowote wa Marekani. Bibi Clinton alisema Marekani inataka kushirikiana na mataifa mengine kufanyia mageuzi masoko ya fedha ambayo hayajadhibitiwa na kwamba Ugiriki inaitaka Marekani inayofanya kazi na kundi la mataifa 20 yaliyostawi kiviwanda-G20 kufanya mabadiliko katika mfumo wa udhibiti wa serikali zinazotawala baadhi ya taasisi za fedha ambazo zimeleta hasara siyo tu kwa Ugiriki, bali pia katika mataifa mengine ikiwemo Marekani.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri: Miraji Othman