1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

PARIS: Kikosi cha kimataifa kupelekwa Darfur

26 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBoC

Waziri wa ulinzi wa Ufaransa, Hervé Morin, amesema, kikosi kipya cha kimataifa huenda kikapelekwa Darfur mapema mwakani katika juhudi za kutaka kukomesha mapigano katika jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan.

Waziri Morin alikuwa akizungumza mwishoni mwa mkutano uliofanywa mjini Paris, kwa azma ya kuchangamsha utaratibu wa amani katika jimbo la Darfur. Amesema vikosi vya Ufaransa huenda vikawa sehemu kubwa ya wanajeshi 20,000 wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika watakaopelekwa Darfur.

Wakati huo huo waziri wa nje wa Ufaransa, Bernard Kouchner, amesema mkutano huo wa Paris uliunga mkono juhudi za kisiasa za Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.

´Darfur tayari wapo wanajeshi, lakini wanajeshi hao hawakuandaliwa vizuri na hawalipwi. Maendeleo hayawezi kupatikana kwa kuongeza idadi ya wanajeshi wasiolipwa.´

Mapema mwezi huu rais Omar al-Bashir alikubali kuruhusu vikosi vya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kupelekwa Darfur.