1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Penalti tano zakosa nyavu Bundesliga wiki hii

Sekione Kitojo
17 Oktoba 2016

Wapigaji watano wa penalti walishindwa kutumbukiza mpira wavuni wiki hii katika Bundesliga

https://p.dw.com/p/2RKt3
Deutschland VfL Wolfsburg - RB Leipzig
Picha: Getty Images/Bongarts/S. Franklin

Ilikuwa  wiki  ya  saba  ya  Bundesliga  ambayo wachezaji kadhaa  walishindwa  kutumbukiza  mipira  ya  penalti wavuni,  haijawahi  kutokea  katika  historia  ya  kandanda la  Bundesliga.

Kulikuwa  na  penalti  tano kwa  jumla  katika  michezo  ya mwishoni  mwa  juma  ya  Bundesliga  na  yote  ilipotea bila  kutumbukia  wavuni. Emil Forsberg  wa RB Leipzig alikuwa  wa  mwisho  katika  jumla  ya  wapigaji  kukosa penalti yake  dhidi  ya  Wolfsburg  jana  Jumapili.  lakini hata  hivyo  raia  huyo  wa  Sweden  aliweza  kutandika mkwaju  kutoka  mita  20  na  ukaleta  faraja  kwa  Leipzig kwa  ushindi  wa  bao  1-0  dhidi  ya  Wolfsburg  ambayo hadi  sasa  imepata  ushindi  mara  moja  sare tatu  na kushindwa  mara  tatu.

Huyu  hapa Emil Forsberg  mfungaji  wa  bao  hilo.

"Ni  rahisi  tu, tunajituma  sana  na  tunajiamini  sana na tunajua  kwamba  tunaweza. Tunatambua , kwamba tunaweza  kushinda  dhidi  ya  timu  yoyote. Ninajivunia timu yetu."

Deutschland VfL Wolfsburg - RB Leipzig
Kocha wa Wolfsburg Dieter HeckingPicha: Getty Images/Bongarts/S. Franklin

Hali  hiyo  lakini  imeiweka  Wolfsburg  katika  hali ngumu. Wolfsburg  kwa  mara  nyingine  imeshindwa, na  haijaweza kuweka  mpira  katika  nyavu  za  adui. Wlfsburg  imeteleza kwenda  chini  zaidi   na  kutumbukia  katika matatizo. Tangu  timu  hiyo  ilipopata  mafanikio  dhidi  ya  Augsburg , imeambulia  tu  pointi  tatu baada  ya  kutoka  sare  bila kufungana  na  timu  ilizokumbana  nazo. Matokeo  hayo ni maafa  kwa  Wolsburg , timu  ambayo  ilifikia  katika awamu  ya  mtoano  ya  Champions League  msimu uliopita. Timu  hiyo  kwa  sasa  iko  katika  nafasi  ya  14, ikiwa  pointi  mbili  tu  kutoka  eneo  la  hatari  la  kushuka daraja. Kocha  Dieter  Hecking  ametumbukia  sasa  katika ukosoaji  mkubwa , licha  ya  kuiongoza  timu  hiyo kushinda  kombe  la  Ujerumani, DFB Pokal mwaka  2015.

RB Leipzig ni  timu  iliyoundwa  mwaka  2009 , lakini imeibuka  na  kupita  katika  ngazi  mbali  mbali  kutoka daraja  la  nne  katika  muda  wa  miaka  saba  na  kufikia katika  Bundesliga.

Kikosi  chake  cha  chipukizi watupu , ambacho  hakina majina  makubwa , kinakonga  nyoyo  za  mashabiki ambao  hawana  upande  kwa  kusakata  kandanda  safi linalopendeza  machoni.

Deutschland VfL Wolfsburg - RB Leipzig
Yusuf Paulsen (kushoto) wa RB Leipzig akipambana na Jeffrey Bruma wa WolfsburgPicha: picture alliance/CITYPRESS 24/Hay

Pamoja  na  viongozi  wa  ligi  hiyo  bayern  Munich , FC Kolon  iliyoko  katika  nafasi  ya  pili pamoja  na Hoffenheim  ambayo  iko  nafasi  ya  sita , Leipzig  ni  moja kati  ya  timu  chache  ambacho  hazijapoteza  mchezo katika  ligi  ya  Ujerumani  msimu  huu.

Licha  ya  kuongoza  ligi , mabingwa  watetezi  Bayern Munich  wanaonekana  kuyumba  msimu  huu , na  hali hiyo  imesababisha  matamshi  makali  kutoka  kwa mwenyekiti  wa  klabu  hiyo  Karl-Heinz Rummenigge ambaye  amesema  ni  hali  isiyokubalika  kutoka  sare  ya mabao  2-2  dhidi  ya  Eintracht  Frankfurt  ambayo  ilikuwa na  wachezaji  10  uwanjani. Bayern  haijapata  ushindi katika  michezo  yake  mitatu iliyopita.

Huyu  hapa  mshambuliaji  wa  Bayern  Munich Arjen Robben.

1. Bundesliga - Eintracht Frankfurt - FC Bayern Munich
Mshambuliaji wa Bayern Munich Arjen Robben akishangilia bao dhidi ya FrankfurtPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

"Kipindi cha  mzozo? hilo  halina nafasi  ya mjadala  kwa sasa. Tawimu lakini  hazidanganyi. Michezo  mitatu ya hivi karibuni  hatukuweza  kushinda. Inakera , hali  hiyo  si nzuri. Na pia  haikuwa  lazima. Haipaswi  kabisa  kutokea, kwamba  unaongoza  kwa  mabao  2-1  dhidi  ya  watu 10, na  kwamba bado wanapata  nafasi ."

FC Kolon  inaogelea  kwa  sasa  katika  bahari  ya  ushindi baada  ya  kuitandika  FC Ingolstadt  kwa  mabao  2-1 nyumbani na  kuchupa  hadi  nafasi  ya  pili  kutoka  juu  ya kilele  cha  ligi. Nini  siri  ya  mafanikio  ya  FC Kolon msimu  huu, na  nini  matarajio  ya  klabu  hiyo  kongwe katika  Bundesliga, ikiwa  ndio  mabingwa  wa  kwanza  wa Bundesliga ilipoanzishwa  mwaka  1963. Huyu  hapa kocha  anayeleta  mafanikio  Peter Stoger.

"Pointi  tulizonazo na  hali  ilivyo, tunataka  kuiendeleza , na hatutaki  kupunguza  kasi. Ni kazi  zetu, kutimiza  wajibu wetu  kutokana  na  matarajio  yanayoongezeka."

Bundesliga Deutschland 1. FC Köln - FC Ingolstadt 04
Wachezaji wa FC Kolon wakishangilia bao dhidi ya IngolstadtPicha: Getty Images/Bongarts/L. Schulze

Katika  michezo  mingine  TSG Hoffenheim  iliendelea kuwa moja  kati  ya  timu  ambayo  hazijapoteza  mchezo  kwa kuishinda  Freiburg  kwa  mabao 2-1, Schalke 04 ikatosheka  na  sare  ya  bao 1-1  dhidi  ya  FC Augsburg licha  ya  kumpoteza  mshambuliaji  wake  mahiri  Breel Embolo  ambaye  ameumia  mguu  na  atakuwa  nje  ya uwanja  huenda  kwa  mwezi  mzima. Borussia Moenchengladbach  iliambulia  sare  ya  bila  kufungana nayo  na  Hamburg SV.  na  Werder  Bremen  ilionesha kuwa  inaanza  kubadilika  chini  ya  kocha  mpya Alexander  Nurri  kwa  kuishinda  Bayer  Leverkusen  kwa mabao  2-1 .

Mchezaji  wa  kati  wa  Werder  Bremen  Zlatan Junuzovic anasema  ushindi  huo  ulikuwa  muhimu  sana.

"Ilikuwa  muhimu  sana, kwamba  tumepata  pointi  tatu kutoka  kwa  timu  ngumu kama hii. Inaonesha  kwamba tuna uwezo, lakini  tunapaswa  kufanyakazi  zaidi na tucheze  kama  timu uwanjani, hilo  ni  muhimu. Kila mmoja wetu, atakayecheza  na  wale  walioko  benchi , kila mmoja  awe  tayari. Ni  hivyo  tu tunaweza  kushinda mchezo."

Katika  ligi  nchini  Uingereza  Premier League , jana Jumapili  Middlesbrough  ilipinduliwa  chali  na  Watford kwa  kuchapwa  bao  1-0, wakati Southampton  iliicharaza Burnley  kwa  mabao  3-1. Arsenal  inashikilia  nafasi  ya pili   sasa  katika  msimamo  wa  ligi  ya  Uingereza  ikiwa na  pointi  sawa  na  viongozi  wa  ligi  hiyo  Manchester City , baada  ya  kuishindilia  Swansea  kwa  mabao  3-2 , Bournemouth  iliikandika  Hull  City   mabao  6 - 1, Chelsea ikairarua  Leicester  mabingwa  watetezi  wa  ligi  hiyo  kwa mabao 3-0. Manchester  City  ililazimishwa  sare  ya  bao 1-1  na  Everton.

Großbritannien Manchester - Fussball Premier League - Manchester City vs Manchester United
Wachezaji wa Manchester City wakifurahia baoPicha: Getty Images/A. Livesey

Lakini  leo  jioni   uwanja  wa  Anfield  road  utachimbika wakati  mafahali  wawili  Liverpool  na  Manchester  United watakapoooneshana  kazi  katika  mchezo  mwingine  wa Premier  League.

Ushindi  dhidi  ya  manchester  United  leo  utamaliza kumbukumbu  chungu  za  Liverpool  kushindwa  na  kikosi cha  kocha  wa  zamani  wa  Chelsea   Jose Mourinho miaka  miwili  iliyopita, amesema  hivyo  mchezaji  wa  kati Jordan Henderson.

Kocha  wa  zamani  wa  Chelsea  Mourinho  aliiongoza klabu  hiyo  ya  mjini  London  katika  ushindi  wa  mabao 2-0  katika  Premier  League  uwanjani Anfield  Aprili mwaka  2014 na  kukatisha  ndoto  za  Liverpool  za  kupata ubingwa  wake  wa  kwanza  wa  ligi  hiyo  tangu  mwaka 1990, na  hatimaye  Manchester  City  kutawazwa mabingwa.

"Ni kocha  wa  kiwango  cha  juu  na  ameonesha  uwezo huo  katika  vilabu  alivyovifundisha," Henderson  alisema hayo  kuhusu  Mourinho , ambae  sasa  ni  meneja  wa timu  ya  Manchester  United.

England Fußballtrainer FC Liverpool Jürgen Klopp
Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp Picha: picture-alliance/empics/N. French

Champions League

Champions  League  inarejea  tena  uwanjani  kesho Jumanne  na  Jumatano , ambapo  Borussia  Dortmund ambayo  imeelemewa  na  majeruhi  ikiteremka katika uwanja  wa  Sporting Lisbon , katika  mpambano  ambao unaonekana  kuwa  kinyang'anyiro  cha  kuwania  nafasi ya  pili  nyuma  ya  Real Madrid  katika  kundi  gumu  la  F. Real Madrid  iko  nyumbani  ikiisubiri  Legia  Warsaw   ya Poland  timu  ya  kwanza  kutoka  Poland  kufikia  awamu hii  katika  muda  wa  miaka  20  iliyopita. Legia Warsaw tayari  imebugia  mabao  nane  katika  michezo  miwili na maporomoko  ya  magoli  yanatarajiwa  katika  mchezo  huo dhidi  ya  Real Madrid.

Real Madrid  imejipasha  joto  kwa  ajili  ya  pambano  hili kwa  kuitwanga  Real Betis  kwa  mabao  6-1 , timu ambayo  ni  bora  zaidi  kuliko  Legia  Warsaw.

Champions League Borussia Dortmund v Real Madrid
Borussia Dortmund ilipopambana na Real Madrid katika Champions LeaguePicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Katika  kundi E  Bayer  Leverkusen  ya  Ujerumani inaisubiri  Tottenham Hotspurs  ya  Uingereza. Kipigo ilichopata  Tottenham  dhidi  ya  Monaco  katika  mchezo wa  kwanza  kimeleta hamasa  kubwa   katika  kundi  hili , kwa  kuziweka  Tottenham  na  Leverkusen  katika  mbinyo wakati  zikiingia  katika  mpambano  huo.

Spurs  ilifanikiwa  kurekebisha  mambo  ilipopambana  na CSKA  Moscow , lakini  Leverkusen  haijashinda  mchezo hadi  sasa  katika  kundi  lake.

CSKA Moscow  ni  wenyeji  wa  Monaco.

Michezo  mingine  ni  ya  kundi  G, ambapo Club  Brugge inaisubiri  FC Porto  ya  Ureno  na  mabingwa  wa Uingereza  Leicester  ina  miadi  na  Copenhagen  ya Denmark. Dinamo  Zagreb  inatoana  jasho  na  Seville  ya Uhispania  na  Lyon  ya   Ufaransa  ni  wenyeji  wa Juventus  Turin  ya  Italia  katika  kundi H.

Michezo  hiyo  itaendelea  tena  Jumatano  ambapo  Bayen Munich   ya  Ujerumani  inapambana  na  Eindhoven  ya Uholanzi , Celtic  inawasbiri  Borussia  Moenchengladbach ya  Ujerumani , Atletico  Madrid  inakwenda  kucheza  na Rostov  ya  Belarus  na  barcelona  iko  nyumbani  ikiisubiri Manchester  City  ya  Uingereza, mchezo  utakaoikutanisha timu  hiyo ya  katalani  na  kocha  wake  wa  zamani  Pep Guardiola.

Pep Guardiola UEFA Champions League
Kocha wa Manchester City Pep GuardiolaPicha: picture-alliance/dpa/P. Powell

Bafana Bafana 

Na  chama  cha  kandanda  nchini  Afrika  kusini  kimesema leo  kwamba  nahodha  wa  zamani  wa  timu  ya  taifa  ya nchi  hiyo  Bafana Bafana  Neil Tovey yuko  katika  hali mbaya  baada  ya  kuugua  kiharusi, mara  ya  pili  katika muda  wa  miaka  miwili. Tovey  alikuwa  nahodha  wa bafana bafana  katika  wakati  ambapo  timu  hiyo  ilionesha kiwango  cha  juu  kabisa  cha  mchezo  kwa  kunyakua kombe  la  mataifa  ya  Afrika. Alipata  kiharusi  wakati  wa mazowezi  jana  Jumapili. Tovey  mwenye  umri  wa  miaka 54 ni  mkurugenzi  wa  ufundi  wa  shirikisho  la  kandanda la  Afrika  kusini.

Kenya  imemteua  mchezaji  wa  zamani  wa  mchezo  wa rugby  nchini  humo  Innocent Simiyu  kuwa  kocha  mpya wa  timu  ya  taifa. Simiyu  mchezaji  wa  zamani  wa  timu ya  taifa  anachukua  nafasi  ya  Benjamin  Ayimba  kwa mkataba  wa  miaka  miwili, na  amepewa  jukumu  la kuiongoza  Kenya  katika  mchezo  wa  kwanza  wa  kundi la  timu  saba  katika  michezo  ya  dunia  ya  mwaka  2017 Dubai  Desemba  mwaka  huu.

Richard Omwela  mwenyekiti  wa  chama  cha  mchezo  wa Rugby  nchini  Kenya , aliwaambia  waandishi  habari , kwamba  Simiyu  alipata  nafasi  ya  juu  katika  usaili , na ndipo  alipoteuliwa  kuwa  kocha  wa  taifa.

 

Mwandishi : Sekione  Kitojo / afpe / dpae  / rtre  / ape

Mhariri: Mohammed Khelef