1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni hatari kwa Ujerumani kupeleka meli yake bahari ya sham

Saumu Mwasimba
20 Februari 2024

Mpango wa Ujerumani wa kupeleka meli yake ya kivita ya jeshi la wanamaji katika bahari ya Sham, ni moja ya jukumu hatari zaidi kuwahi kufanywa na jeshi hilo katika kipindi cha miongo.

https://p.dw.com/p/4ccyk
Boris Pistorius | Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius, asema mpango wa Ujerumani wa kupeleka meli yake ya kivita ya jeshi la wanamaji katika bahari ya Sham, ni hatari Picha: Lisi Niesner/REUTERS

Akiwa ziarani Crete nchini Ugiriki alikotembelea meli hiyo ya kivita ya  jeshi la Ujerumani waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Boris Pistrorius amesema sio jambo la kutiwa chumvi pale inapoelezwa kwamba operesheni hiyo ya kupelekwa meli ya kivita ya kikosi cha jeshi la wanamaji la Ujerumani katika bahari ya Sham ndio moja ya operesheni hatari zaidi kuwahi kufanywa na kikosi hicho kwa miongo.

Ni mpango unaohusu hasa kulinda sheria ya kimataifa,uhuru na usalama katika bahari hiyo lakini pia ni mpango unaohusu kuleta uthabiti katika njia hiyo ya shughuli za kibiashara  pamoja na kanda nzima hiyo.

Waziri huyo wa ulinzi wa Ujerumani amebaini kwamba kupelekwa kwa kikosi cha jeshi la wanamaji cha Ujerumani kwenye eneo hilo tete ambacho kitakuwa sehemu ya ujumbe wa kikosi cha Umoja wa Ulaya cha jeshi la wanamaji kwaajili ya kulinda safari za meli dhidi ya wanamgambo wa Kihouthi nchini Yemen,ni ishara kwamba Ujerumani inawajibika kimataifa.

Waasi wa Kihuthi waendelea na mashambulizi Bahari ya Shamu

"Umoja wa Ulaya imeshatowa idhini ya ujumbe wa Aspides kupelekwa. Ujerumani ni moja ya nchi za mwanzo zilizosema zitahusika kwenye mpango huo ikiwa bunge letu litaidhinisha. Na ikiwa bunge litafanya hivyo Ijumaa basi meli yetu ya kivita ya Hesse itakuwa tayari kuanza safari kwenye bahari ya Sharm. Na hatua hiyo sio kuhusu kitu kingine bali itahusika kulinda sheria ya kimataifa,uhuru, safari na usalama wa baharini. Lakini pia itahusu kuweka uthabiti kwenye kanda hiyo,'' alisema waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius

Wahouthi wasema wataendelea kushambulia meli katika bahari hiyo hadi Israel itakapoacha kuishambulia Gaza.

Bahari ya Shamu
Moja ya meli iliyoshambuliwa na waasi wa Kihouthi kutoka YemenPicha: Indian Navy/AP/dpa/picture alliance

Wanamgambo wa Kihouthi kutoka Yemen wamekuwa wakishambulia meli zinazopitia eneo hilo katika kile wanachosema ni kulipiza kisasi hatua zinazochukuliwa na Israel katika Ukanda wa Gaza. Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius hakuondowa uwezekano wa kufanyika mashambulio ya moja kwa moja ya Wahouthi dhidi ya meli ya kivita ya Ujerumani.Ingawa wakati huohuo amesisitiza kwamba operesheni hiyo ni ya kutowa ulinzi.

''Na hivi sasa hilo ni suala la dharura,dharura ambayo meli hii ya kivita inapaswa kuhusika kwenye operesheni hii, operesheni ambayo bila shaka inakabiliwa na kitisho cha kushambuliwa kwa makombora, droni zisizokuwa na rubani, na pengine hata kuvamiwa kwa kutumika maboti ya mwendo kasi''

Wahouthi washambulia meli nje ya pwani ya Kusini mwa Yemen

Kwa mujibu wa waziri huyo wa ulinzi operesheni hiyo ni muhimu sana katika kupeka ujumbe kwa Wahouthi kuhusiana na mashambulizi yao pamoja na kwa nchi zinazowaunga mkono. Jana Jumatatu mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya waliidhinisha mpango wa pamoja wa kupleka meli za kivita  na mifumo ya ulinzi wa anga ya kutowa onyo la mapema katika eneo hilo la bahari ya Sham,Ghuba ya Aden pamoja na maeneo ya bahari ya karibu na eneo hilo.

Meli hizo zitapewa amri ya kushambulia pale tu wanamgambo wa Kihouthi watakapoanzisha mashambulizi yao.Kamandi ya kutowa maelekezo ya kikosi hicho cha Umoja wa Ulaya itakuwa katika mji wa Larissa nchini Ugiriki.

Vyanzo: dpa/reuters/ap