1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Berlin yauvamia msikiti kwa tuhuma za ugaidi

Oumilkheir Hamidou
28 Februari 2017

Maafisa wa serikali ya jiji la Berlin wameamuru upigwe marufuku msikiti mmoja ulioko katika mtaa wa Moabit. Msikiti huo ulikuwa ukichunguzwa kwa muda mrefu sasa na polisi

https://p.dw.com/p/2YNNV
Deutschland Razzia in Berlin
Picha: Reuters/C. Mang

Leo asubuhi polisi wamevivamia vituo 24, ikiwa ni pamoja na nyumba za watu, ofisi mbili za mashirika na vyumba viwili vya jela katika mitaa ya Moabit na Tegel mjini Berlin. Msemaji wa polisi amesema askari polisi 460 walishiriki katika opereshini hiyo iliyoanza tangu tangu saa 12 za alfajiri. Polisi wanasema msikiti huo umegeuzwa kituo wanakokutania wafuasi wa itikadi kali ya dini ya Kiislam. Polisi wanasema Anis Amri,  raia wa Tunisia aliyefanya shambulio la kigaidi katika soko la X-Mas mjini Berlin alikuwa kila wakati akenda katika msikiti huo. Kwa mara ya mwisho alinaswa katika kamera akiingia ndani ya msikiti huo usiku wa kuamkia decemba 19 mwaka jana. Itakumbukwa Anis Amri aliendesha lori  decemba 19 iliyopita kati kati ya umati wa watu waliokuwa katika soko la X-Mas na kuwauwa 11 na 50 wengine kujeruhiwa.

Deutschland Razzia bei Moschee-Verein Fussilet 33 in Berlin
Msikiti wa "Fussilet 33" mjini Berlin umefungwa na serikaliPicha: Reuters/F. Bensch

Amri ya kupigwa marufuku msikiti huo ilitolewa tangu Februari 15 iliyopita. Na tangu wiki moja sasa wakuu wa msikiti huo waliamua wenyewe kuufunga msikiti huo. Waziri wa ndani wa jimbo la Berlin, Andreas Geisel amesema wakuu hao wa jumuia ya Fussilat wamebatilisha pia mkataba wa kupanga jengo msikiti huo ulimokuwemo.

Andreas Geisel anapanga kuzungumza na waandishi habari baadae hii leo mjini Berlin ili kutoa maelezo zaidi kuhusu opereshini hizo za polisi dhidi ya msikiti wa Fussilat 33.

Duru za polisi zinasema katika msikiti huo watu walikuwa wakikusanya fedha kwaajili ya kugharimia mashambulio ya kigaidi nchini Syria. Katika darsa zilizokuwa zikitolewa,waumini ambao wengi wao ni waturuki na wengine wa kutoka eneo la caucasus walikuwa wakipatiwa mafunzo ya itikadi kali , wakiandaliwa kujiunga na wanamgambo wa Dola la Kiislam IS nchini Syria.

Polisi walikuwa wakichunguza pirika pirika zilizokua zikiendelea ndani ya msikiti huo kutoka kituo cha polisi kilichokuwa upande wa pili wa jengo hilo, na baadhi ya wakati kwa msaada wa kamera.

Suala la kupigwa marufuku msikiti huo limekuwa likijadiliwa tangu mwaka 2015. Kufuatia shambulio la kigaidi la decemba iliyopita uchunguzi ukaimarishwa.

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/AP/dpa/

Mhariri: Iddi Ssessanga