1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Munich ilifahamu kuhusu kitisho cha ugaidi

2 Januari 2016

Uchunguzi uliofanywa na vyombo vya habari vya Ujerumani umeonyesha kuwa maafisa walijua kuhusu uwezekano wa kutokea shambulizi katika mji wa kusini wa Munich kabla ya siku kuu ya Krismasi.

https://p.dw.com/p/1HX2F
München Bayern Terrorwarnung Polizei Hauptbahnhof
Picha: Reuters/M. Rehle

Gazeti la Ujerumani la Süddeutsche, pamoja na mashirika ya utangazaji ya WDR na NDR yaligundua kuwa maafisa - wakiwemo wa ofisi za mambo ya ndani na mwendesha mashtaka - walikuwa na habari ya uwezekano wa kutokea shambulizi la kigaidi mjini Munich tangu Desemba 23.

Mkuu wa polisi mjini Munich amesema walikuwa na "habari za kuaminika" kuhusu kitisho cha ugaidi, hali iliyowalazimu mamlaka mjini humo kufunga kituo cha treni. Waziri wa mambo ya ndani Thomas de Maiziere amesema katika taarifa kuwa hali barani Ulaya na Ujerumani inaendelea kuwa mbaya katika Mwaka Mpya.

Mkuu wa polisi wa Munich Hubertus Andrae akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Ijumaa (01.01.2015) amesema "kwa sasa bado wanausalama wa ziada 1,000 wako kazini."

Polisi wamemwagwa katikati ya mji huo na katika viuo viwili vya treni kikiwemo kituo kikuu ambavyo ilibidi kufungwa saa za mwisho mwisho za mwaka 2015 baada ya polisi kutowa onyo la shambulio la kigaidi kwa kuzingatia dokezo la shirika la ujasusi la kigeni.

München Bayern Bahnhof Terrorwarnung Polizei Reisende
Polisi wanaendelea kuweka ulinzi mjini MunichPicha: Reuters/M. Rehle

Taarifa kamili juu ya tishio hilo na watu wanaohusika bado haziko wazi lakini duru moja ya ujasusi imewataja watu waliopanga mashambulizi ni watano hadi saba na wanatokea Syria na Iraq wakiwa na mafungamano na kundi la Dola la Kiislamu.

Hata hivyo Andrae amewaambia waandishi wa habari kwamba wamezichunguza data kuhusiana na majina ya watu hao lakini hadi sasa hawajuwi iwapo majina hayo ni sahihi, iwapo watu hao wako kweli na wako wapi.

Hofu ingalipo

Maafisa usalama wa Ujerumani wanaamini kwamba watu kadhaa wameingia Ujerumani kati ya mwezi wa Oktoba na Novemba wakisafiri kwa kutumia paspoti za Syria nambari za pasi hizo zikiwa sawa na zile zinazomilikiwa na Kundi la Dola la Kiislamu.

Mmiliki mmoja wa mkahawa mjini humo ameliambia shirika la habari la dpa kwamba "uwezekano wa kufanyika shambulio umezidi kuongezeka kwa sababi hivi sasa Ujerumani imejihusisha katika vita." akimaanisha uamuzi wa Ujerumani wa hivi karibuni kutowa vikosi vyake na msaada mwengine wa kijeshi kwa muungano unaopambana na Kundi la Dola la Kiislamu nchini Syria. Ameongeza kusema ni "suala la mahala gani kutafanyika shambulio hilo."

Miji mikuu ya Ulaya imekuwa katika hali kubwa ya tahadhari tokea mwezi wa Novemba wakati wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu walipouwa watu 130 katika mashambulio ya risasi na kujitowa muhanga mjini Paris na kuzusha hofu kwamba wanaweza kufanya mashambulizi mengine wakati wa shamra shamra za Krismasi na Mwaka Mpya.

Mwandishi: Sekione Kitojo/AFP/DW
Mhariri: Bruce Amani