1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi nchini Syria washambulia wanaharakati

Halima Nyanza (ZPR)24 Aprili 2011

Wanaharakati wa haki za binadamu nchini Syria, wamesema polisi wa idara ya upelelezi, wamevamia nyumba kadhaa karibu na mji mkuu wa nchi hiyo Damascus usiku wa kuamkia leo.

https://p.dw.com/p/1136B
Machafuko nchini SyriaPicha: picture alliance/abaca

Polisi waliokuwa wamevaa nguo za kawaida na wakibeba silaha, walivamia baadhi ya nyumba katika kitongoji cha Harasta na waliwakamata wanaharakati.

Vikosi vya usalama na wafuasi wa Rais Assad waliobeba silaha, waliwaua takriban watu 112 katika siku mbili zilizopita baada ya siku ya Ijumaa kuwafyatulia risasi waandamanaji wanaodai uhuru wa kisiasa na baadaye katika mazishi ya watu hao yaliyofanyika jana.

Unruhen in Syrien
Wasyria wakishiriki katika mazishi ya wenzaoPicha: picture alliance/dpa

Wakati huohuo, wabunge wawili kutoka katika mji wa Deraa wamejiuzulu kupinga mauaji hayo yaliyofanywa na jeshi.

Kiongozi wa kidini katika mji huo pia amejiuzulu kupinga ghasia hizo. Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani, imewatahadharisha raia wake kuepuka kufanya safari nchini Syria, iwapo itawezekana, na pia kuwashauri raia wake walioko nchini humo kuondoka.