1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi wa Ujerumani waandamani dhidi ya kufungua mipaka

Maja Dreyer23 Novemba 2007

Ikiwa umesalia mwezi mmoja tu kabla ya mipaka mingi kati ya nchi za Ulaya itafunguliwa kufuatia kujiunga na mkataba wa Schengen, mamia ya polisi wa Ujerumani waliandamana kupinga kufunguliwa huko katika maeneo ya mipaka.

https://p.dw.com/p/CSIK
Kibao cha mpaka ndani ya nchi wanachama wa Schengen
Kibao cha mpaka ndani ya nchi wanachama wa SchengenPicha: BilderBox

Ukipita mpaka kati ya Ujerumani na Ufaransa, hakuna polisi wala maofisa wa forodha. Kitu cha pekee kinachoonyesha kwamba unapita mpaka ni kibao chenye jina la nchi jirani. Tangu mwaka wa 1985, nchi 15 za Ulaya zilitia saini mkataba wa Schengen juu ya kufungua mipaka kwa usafiri huru wa watu na bidhaa, kutoka Norway hadi Ugiriki.

Kuanzia tarehe 21 Disemba nchi nyingine 9 za Ulaya Mashariki zinajiunga na jumuiya hiyo zikiwemo nchi kadhaa jirani na Ujerumani. Siku hizi, waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble yuko safirini kuitembelea mikoa husika ya Ujerumani yenye mipaka na nchi mpya za jumuiya ya Schengen. Akizungumza katika mji wa Frankfurt/Oder, mji ambao unaeneo kwenye pande zote mbili za mpaka kati ya Ujerumani na Poland, waziri huyu aliutetea ufunguzi wa mipaka: “Hatua hiyo ni sawa na inaweza kuwajibika. Haimaanishi kuwa usalama utapungua kwa wananchi, bali usalama utaongezeka.”


Huko mjini Frankfurt/Oder, waziri Schäuble lakini alikabiliwa na upinzani kutoka kwa polisi wake. Mamia ya polisi waliandamana na kudai kwamba ufunguzi wa mipaka haujaandaliwa vizuri. Kwa vile udhibiti wa mipaka hautatekelezwa tena, idadi ya polisi inayofanya kazi huko pia itapunguzwa kwa nusu.

Wengi wa maafisa wa mipaka lakini bado hawajui watafanya nini baada ya Disemba 21, kama anavyosema polisi huyu, Bw. Horst Pawlik: “Maafisa wale watakaokuja wa kazi za alfajiri siku hiyo ya Disemba 21, bado hawajui watafanya nini. Inasemekana kwamba wapige doria kwenye mipaka. Lakini sisi tunajiuliza: Magari yatatoka wapi? Au tutumie baiskeli? Masuali haya hayajajibiwa hadi sasa.”


Jumuiya ya polisi inasema kufunguliwa kwa mipaka kunakuja mapema mno na kwamba kiwango cha usalama katika nchi za Ulaya Mashariki si sawa na kile cha Ujerumani.

Matamshi haya yaliisikitisha pia idara husika katika nchi jirani na Ujerumani, Poland. Waziri wa zamani wa mambo ya ndani wa Poland, Bw. Wladyslaw Stasiak anasema hawafahamu pingamizi hii kutoka kwa polisi wa Ujerumani: “Poland ilitekeleze masharti yote ya mkataba wa Schengen. Watu wengi walifanya kazi sana kwa ajili hiyo. Tuliweka mifumo ya kisasa kabisa ya usalama kwa sababu haya ndiyo yalikuwa masharti ya kujiunga na jumuiya ya Schengen.”


Polisi ya Ujerumani inatambua kwamba kulifanywa juhudi nyingi upande wa Poland na Tsheki, lakini inasema kwamba Ujerumani haijajiandaa vizuri kwa hatua hiyo. Bado hakuna mkakati wa kupiga doria mipaka wala vifaa vinavyohitajika. Wanasiasa lakini wanasisitiza kuwa kufunguliwa kwa mipaka ni bahati kubwa kwa nchi za Ulaya. Waziri Schäuble pia anakumbusha juu ya idara ya pamoja ya Ujerumani na Poland kudhibiti mpaka idara itakayoanza kufanya kazi Disemba.