1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi wa Ujerumani wawakamata viongozi wawili wa Kihutu

Sekione Kitojo17 Novemba 2009

Ujerumani imewakamata viongozi wawili wa Kihutu ambao wanatuhumiwa kuendesha kampeni ya mauaji iliyokuwa ikifanywa na makundi ya waasi.

https://p.dw.com/p/KZEX
Haya ni makaburi ya Nyaza nje kidogo ya mji wa Kigali, nchini Rwanda ambako mamia kwa maelfu ya wahanga wa mauji ya kimbari ya mwaka 1994 wamezikwa.Picha: AP

Ujerumani imewakamata viongozi wawili wa Kihutu ambao wanatuhumiwa kwa kuendesha kampeni ya mauaji iliyokuwa ikifanywa na makundi ya waasi, ikiwa ni pamoja na ubakaji na utekaji nyara mashariki mwa Congo.

Dr. Ignace M, mwenye umri wa miaka 46, rais wa jeshi la kidemokrasia la ukombozi nchini Rwanda FDLR, anatakiwa nchini Rwanda kwa uhalifu wa kivita. Maafisa wa Ujerumani hivi sasa wanaliona kundi la FDLR kuwa ni kundi la kigaidi. Maafisa wamesema pia wamemkamata naibu wake Straton M, mwenye umri wa miaka 48. Ofisi ya mwendesha mashataka ya shirikisho la Ujerumani imesema kuwa inatayarisha ushahidi wa kutosha kuwa watu hao wawili wote wanahusika na uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita. Nae mwendesha mashtaka mkuu nchini Rwanda Martin Ngoga amesema kuwa " nafikiri ni hatua nzuri, lakini suala la msingi ni hatua za kesi yenyewe itakavyoendelea. Lakini kwamba wamekamatwa ni hatua nzuri. Na natumaini kwamba kwasababu ilichukua muda mrefu kabla ya kufikiwa hatua hiyo, lakini ni vizuri kwamba hivi sasa imefanyika na tunasubiri kuona nini kitaendelea baadaye.

Watu hao huenda wakakabiliwa na mashtaka nchini Ujerumani. Dr. M pia anashutumiwa kwa kuwa kiongozi wa kundi la kigaidi. Wanamgambo wao wa Kihutu walikimbia kutoka Rwanda baada ya kudaiwa kufanya mauaji ya kimbari nchini humo, na wanashutumiwa kwa kufanya tena wimbi la mauaji katika nchi jirani ya Congo. Mataifa ya Afrika yamelalamika kuwa Wahutu wanaoishi uhamishoni bila matatizo nchini Ujerumani ndio walikuwa wanahusika zaidi.

Dr. M anayeelezwa na upande wa mashtaka kuwa rais wa kundi la FDLR tangu mwaka 2001, alikuwa anaishi katika mji wa Mannheim. Straton M, ambaye alikuwa anaishi karibu na Stuttgart, alikuwa makamu wa rais tangu mwaka 2005 na alikuwa kama mshauri mkuu wa kijeshi na mwakilishi.

Ujerumani ilianza uchunguzi kuhusiana na watu hao mwaka mmoja uliopita, na kukusanya ushahidi kwa kisiri siri.

Waendesha mashtaka wamesema kuwa kundi la FLDR limeua mamia ya raia nchini Congo na kubaka idadi kubwa ya wanawake katika kipindi cha Januari 2008 na Julai 2009, na pia walichoma vijiji, na kuwalazimisha wanavijiji kukimbia kwa hofu.

Mwandishi : Sekione Kitojo/ DPAE

Mhariri : Mohammed Abdul Rahman.