1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi watatu wauawa katika shambulizi Indonesia

Iddi Ssessanga
25 Mei 2017

Rais wa Indonesia Joko Widodo ameagiza uchunguzi wa kina ufanyike kuhusiana na mashambulizi mawili ya kujitoa muhanga yaliolenga polisi na kuuwa maafisa watatu mjini Jakarta.

https://p.dw.com/p/2dZgT
Explosion in Jakarta Indonesien
Picha: Reuters/D.Whiteside

Maafisa katika taifa hilo lenye Waislamu wengi zaidi duniani hawajaashiria kundi gani wanaamini limehusika na mashambulizi hayo lakini shuku itaiangukia mitandao ya wanamgambo nchini humo inayoliunga mkono kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS. Katika hotuba kwa taifa kupitia televesheni, rais Joko Widodo alisema ameamuru uchunguzi wa kina ufanywe, na aliwasihi raia nchini kote kubakia watulivu na kuendelea kuwa wamoja.

Uchunguzi mkubwa umekabidhiwa kwa kitengo maalumu cha kupambana na ugaidi cha polisi ya Indonesia - Densus 88, ambacho kimetoa mchango mkubwa katika kukandamiza na kuuwa baadhi ya wanamgambo wanaosakwa zaidi nchini humo. Polisi wanaamini walilengwa hasa katika mashambulizi hayo wakati wanajiandaa kutoa ulinzi kwa ajili ya gwaride karibu na kituo cha mabasi cha Kampung Melayu, ambacho ni eneo linalotembelewa zaidi na wenyeji lakini siyo wageni.

Deutschland Indonesien Joko Widodo bei Merkel
Rais wa Indonesia Joko WidodoPicha: Getty Images/S. Gallup

Vikosi vya usalama vyalengwa

Vikosi vya usalama vimekuwa ndiyo vinalengwa zaidi katika miaka ya hivi karibuni na wanamgambo wa Indonesia, ambao kwa sehemu wameondao nadhari yao kwa raia wa nchi za magharibi.  Wakati huo huo, katika mkutano na waandishi habari msemaji wa polisi Meja Jenerali Setyo Wasisto alithibitisha kuwa miripuko hiyo ya mabomu hayo ya kujitoa muhanga ilifanywa na watu wawili, ambao wote walifariki katika shambulizi hilo.

"Tumefanya uchunguzi katika eneo la tukio la mashambulizi ya kujitoa muhanga yaliofanywa na magaidi Mei 24, 2017. Mripuko wa kwanza ulitokea saa tatu kamili za usiku na wa pili ulitokea dakika tano baadae. Miili ya waripuaji hao inaendelea kutambuliwa katika maabara ya uchunguzi ya polisi na kikosi cha kupambana na ugaidi," alisema Meja Jenerali Wasisto.

Ushawishi wa mashambulizi Uingereza, Ufilipino

Setyo hakuweza kueleza bayana ni kundi gani hasa limehusika na mashambulizi hayo, lakini akasema makundi ya kigaidi huenda yamehamasishwa na matukio ya karibuni nchiniUingereza na Ufilipino. Vyombo vya habari vya ndani vimesema tukio ambalo polisi walikuwa wanajiandaa kulipatia ulinzi lilikuwa gwaride la mwenge linalofanyika kwa kawaida kabla ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, unaoanza mwishoni mwa wiki hii.

Indonesien Explosion in Jakarta
Maafisa polisi wakikagua eneo lilipotokea shambulizi mjini Jakarta.Picha: picture-alliance/AP Photo/D. Alangkara

Indonesia imekabiliana kwa muda mrefu na wanamgambo wa Kiislamu na imekumbwa na mashambulizi kadhaa ya katika kipindi cha miaka 15 iliopita, yakiwemo ya kisiwa cha Bali mwaka 2002, ambamo watu 202 waliuawa wengi wao wakiwa watalii wa kigeni. Ukandamizaji endelevu umedhoofisha mitandao hatari zaidi, lakini kuibuka kwa IS kumeonyesha kuwa kivutio kipya kwa wafuasi wa itikadi kali, ambao kwa mamia wamekwenda nje kupigana katika kile wanachoamini ni vita vya jihadi.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre

Mhariri: Saumu Yusuf