1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi wawili wauwawa Misri

30 Juni 2014

Maafisa wawili wa polisi wameuwawa Misri Jumatatu (30.06.2014) wakati wakiteguwa mabomu karibu na kasri la rais mjini Cairo ikiwa karibu mwaka mmoja tokea jeshi kumpinduwa Rais Mohamed Mursi.

https://p.dw.com/p/1CSu4
Muda mfupi baada ya mripuko wa bomu karibu na Kasri la Rais mjini Cairo. (30.06.2014)
Muda mfupi baada ya mripuko wa bomu karibu na Kasri la Rais mjini Cairo. (30.06.2014)Picha: Mohamed El-Shahed/AFP/Getty Images

Kundi la wanamgambo wa itikadi kali la Kiislamu mojawapo ya makundi yaliongoza mashambulizi tokea kupinduliwa kwa rais Mohamed Mursi Julai tatu mwaka jana,lilionya siku chache zilizopita kwamba limetega mabomu katika eneo la mashariki la kasri la rais mjini Cairo.

Haikuweza kufahamika mara moja iwapo Rais Sisi mkuu wa majeshi wa zamani aliyempinduwa Mursi mwenye itikadi kali za Kiislamu na baadae kushinda uchaguzi wa rais wa mwezi wa Mei alikuwako katika kasri hilo la Ittihadiya wakati huo.Wizara ya ulinzi imesema kanali mmoja ameuwawa na polisi wengine kadhaa kujeruhiwa wakati bomu walililokuwa wakijaribu kuliteguwa kuripuka.

Taarifa ya wizara hiyo imesema afisa mwengine wa polisi aliuwawa katika operesheni kama hiyo katika eneo karibu na kasri hilo.

Kundi la wanamgambo la Ajnad Misr au Wanajeshi wa Misri limesema limetega mabomu kadhaa karibu na kasri la rais kuvilenga vikosi vya usalama kabla ya kutambuwa kwamba raia wanaweza kuwa hatarini. Baadae ilitowa taarifa ikisema kwamba imeshindwa kuyaondowa mabomu hayo na kuwataka wapita njia wawe waangalifu.

Mashambulio ya wanamgambo

Mashambulio ya wanamgambo nchini Misri yameuwa takriban polisi na wanajeshi 500 tokea kupinduliwa na kuwekwa gerezani kwa Mursi.Watu wanane wamejeruhiwa katika mfululizo wa miripuko wiki iliopita kwenye vituo vya reli ya chini ya ardhi mjini Cairo hilo likiwa ni shambulio la kwanza tokea Sisis aapishwe kuwa rais wa nchi hiyo.

Majeruhi wa bomu lililoripuka karibu na Kasri la Rais mjini Cairo aikikimbizwa hospitalini. (30.06.2014).
Majeruhi wa bomu lililoripuka karibu na Kasri la Rais mjini Cairo aikikimbizwa hospitalini. (30.06.2014).Picha: picture-alliance/dpa

Sisi ambaye Mursi alimteuwa kuwa waziri wa ulinzi wakati wa uongozi wake wa mwaka mmoja uliojaa vurugu ameahidi kupambana na wanamgambo.Alikuwa kama kiongozi wa Misri kabla ya hata ushindi wake katika uchaguzi wa rais wa mwezi wa Mei na Waislamu wa itikadi kali wanamlaumu kwa kutumia nguvu kuwatawanya watu waliokuwa wakimpinga na kusababisha kuuwawa kwa watu 1,400 katika mapambano ya barabarani tokea kupinduliwa kwa Mursi.

Serikali imekuwa ikililaumu kundi la Mursi la Udugu wa Kiislamu ambalo sasa limetangazwa kuwa la kigaidi kwa kuhusika na mashambulizi hayo ya wanamgambo madai ambayo kundi hilo imeyakanusha.Kundi hilo limesema limeachana na matumizi ya nguvu miongo kadhaa iliopita na limejitolea kudai haki zao kwa njia ya amani.

Siku ya ghadhabu

Muungano wa kupinga mapinduzi unaoongozwa na kundi la Udugu wa Kiislamu umesema leo hii wataandamana kwa ajili ya "siku ya ghadhabu" hapo tarehe tatu Julai ikiwa ni kumbukumbu ya mwaka mmoja tokea kupinduliwa kwa Mursi.

Wafuasi wa rais aliyepinduliwa madarakani Mohamed Mursi.
Wafuasi wa rais aliyepinduliwa madarakani Mohamed Mursi.Picha: DW/M.Hashem

Takriban Waislamu wa itikadi kali 16,000 na wanaotuhumiwa kuwa washirika wao wamekamatwa ambapo 200 kati yao wamehukumiwa adhabu ya kifo katika kesi zilizosikilizwa kwa haraka haraka miongoni mwao ni kiongozi wa Udugu wa Kiislamu Mohamed Badie.

Mursi mwenye anakabiliwa na mashtaka mbali mbali ambapo kwayo akipatikana na hatia anaweza kuhukumiwa kifo.

Ukandamizaji wa vikosi vya usalama umepunguza matumaini ya mabadiliko ya kidemokrasia nchini Misri ambayo yalipata mashiko baada ya vuguvugu la uasi dhidi ya Mubarak miaka mitatu iliopita.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/Reuters

Mwandishi :Mohammed Abdul-Rahman