1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi yavunja maandamano Ukraine, watatu wauawa

Admin.WagnerD22 Januari 2014

Watu watatu wameripotiwa kuuawa mjini Kiev katika wimbi jipya la maandamano ya kuipinga serikali ya Ukraine, tukio ambalo linaweza kuchochea zaidi mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo, uliodumu kwa miezi miwili sasa.

https://p.dw.com/p/1AvCd
Waandamanaji wakiwasogelea polisi waliojipanga kuvunja maandamano yao.
Waandamanaji wakiwasogelea polisi waliojipanga kuvunja maandamano yao.Picha: Reuters

Polisi iliyavamia maandamano muda mfupi baada ya saa 12 za alfajiri, na kuanza kuvunja vizuwizi vilivyowekwa katika mtaa wa Grushevsky mjini Kiev, na kuanza kuwakamata waandamanaji. Jeshi hilo pia lilitumia magruneti ya kutoa machozi katika eneo walikokuwa wamesimama waandamanaji, ambao nao walijibu kwa kuwarushia mawe.

Mwanamke akizungumza na maafisa wa polisi wakati wakijiandaa kuwakabili waandamanaji.
Mwanamke akizungumza na maafisa wa polisi wakati wakijiandaa kuwakabili waandamanaji.Picha: Reuters

Ripota wa shirika la habari la Associated Press aliwaona wahudumu wa afya wakitangaza vifo vya watu wawili karibu na vizuwizi ambako polisi na waandamanaji wamekabiliana kwa siku tatu. Oleh Bondar, ambaye ni mhudumu wa afya, alisema watu wawili walikufa kutokana na majeraha ya risasi, lakini hakubainisha iwapo risasi hizo zilikuwa za mpira au za moto. Mtu wa tatu alitangazwa kufariki hospitali baada ya kuanguka kutoka jengo refu wakati wa maandamano hayo.

Neno "ugaidi" lazidi kupata matumizi

Waziri mkuu wa Ukraine Mykola Azarov amesema leo kuwa maandamano ya kuipinga serikali yameleta magaidi katika mitaa ya Kiev, na kuonya kuwa vitendo vyote vya uhalifu vitaadhibiwa. Akizungumza na baraza lake karibu na eneo walipokabiliana waandamanaji na polisi mjini Kiev, Azarov alisema magaidi kutoka 'Maidan', akimaanisha uwanja wa uhuru, waliwateka watu kadhaa na kuwapiga, na kutangaza rasmi kuwa watu hao ni wahalifu wanaopaswa kuwajibika kutokana na vitendo vyao.

Amewalaumu viongozi wa upinzani kwa kuchochea mgogoro kwa kutisha maandamano, ambayo anasema yanaivuruga nchi hiyo. Mykola alionya jana Jumanne, kuwa vikosi vya usalama vingetumia nguvu kutawanya maandamano hayo ambamo mamia ya watu wamejeruhiwa.

Mwandamanaji akitumia fataki wakati wa makabiliano kati ya Polisi na waandamanaji.
Mwandamanaji akitumia fataki wakati wa makabiliano kati ya Polisi na waandamanaji.Picha: picture-alliance/AP Photo

Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov alionya siku ya Jumanne kuwa hali nchini Ukraine itashindwa kudhibitiwa. Lavrov alisema ukweli kwamba wito wa viongozi wa maandamano hayo wanaopendelea kujiunga na Umoja wa Ulaya, wa kuwepo na utulivu umeshindwa kutuliza hali, hii inamaanisha kuwa hali ilikuwa inazidi kuwa tete.

Kiini cha mgogoro mpya

Sheria mpya zinazopiga marufuku karibu aina zote za maandamano, ambazo ziliwakasirisha waandamanaji, zilichapishwa rasmi katika gazeti la bunge la Ukraine. Sheria hizo zinaruhusu vifungo vya hadi miaka mitano gerezani kwa wale wanaozuwia majengo ya umma, na kukamatwa kwa waandamanaji wanaoficha nyuso zao au kuva kofia za kujikinga.

Upande wa upinzani ukiongozwa na wanasiasa watatu akiwemo bingwa wa zamani wa mchezo wa ndondi Vitali Klitschko, ulisema ulikuwa tayari kwa mazungumzo lakini ulisisitiza kuwa unataka kufanya mazungumzo na Yanukovych mwenyewe na si wasaidizi wake.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe, rtre,ape.
Mhariri: Charo Josephat