1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Premier League na La Liga zapamba moto

18 Januari 2016

Katika Ligi ya Premier ya England, kinyang'anyiro cha kutwaa ubingwa wa msimu huu kinaendelea kupamba moto ambapo inaonekana kuwa mbio zimeanza kuchukua mkondo wa farasi watatu

https://p.dw.com/p/1HfVa
Großbritannien Manchester United Trainer Louis Van Gaal
Picha: picture-alliance/dpa/N. Roddis

Arsenal inashika usukani pointi ikiwa na pointi 44 sawa na Leicester isipokuwa ina faida ya magoli mengi. Arsenal ilitoka sare ya bila kufungana goli huku Leicester pia ikikabwa kwa sare ya moja moja na Aston Villa.

Aliyekuwa na tabasamu kubwa mwishoni mwa wiki ni mwalimu wa Manchester City Manuel Pellegrini ambaye vijana wake waliibomoa Crystal Palace nne bila na hivyo kupunguza pengo lao na viongozi Arsenal na Leicester kwa pointi moja tu katika nafasi ya tatu. Na kama hatua ya kuimarisha kikosi chake, Leicester inakaribia kumnunua beki wa timu ya taifa ya Ghana Daniel Armatey kutoka klabu ya FC Copenhagen ya Denmark.

Mkufunzi wa Manchester United Louis Van Gaal anasema klabu yake bado ina fursa ya kushinda ligi ya Uingereza msimu huu. United waliishinda Liverpool 1-0 jana uwanajni Anfield na kupanda hadi nafasi ya tano, pointi saba nyuma ya viongozi Arsenal na Leicester.

Katika kandanda la Uhispania, michuano ya jana Jumapili haikuleta mabadiliko yoyote kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, kwa sababu timu zote tatu za kwanza zilimimina magoli katika milango ya adui.

Atletico Madrid ilisalia kileleni baada ya kupata ushindi wa tatu bila dhidi ya Las Palmas. Wako na pengo la pointi mbili mbele ya Barcelona, ambao wana mchuano mmoja zaidi yao na waliwasambaratisha Athletic Bilbao mabao sita sifuri, matatu yakitoka kwa mfungaji magoli mengi katika la liga Luis Suarez. Wakati huo huo, Barcelona imeondoa wasiwasi wowote kuwa mshambuliaji wake Lionel Messi aliumia hapo jana katika mchuano huo. Taarifa ya Barca imesema vipimo vlivyofanywa leo asubuhi vimeonyesha hakuna jeraha kubwa bali ni maumivu madogo. Barca wana pengo la pointi mbili juu ya nambari tatu Real Madrid, ambao waliwabamiza Sporting Gijon tano moja.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman