1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Presseschau: Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz
28 Mei 2018

Wahariri wanatoa maoni yao juu ya kujiuzulu kwa waziri mkuu mteule wa Italia Giuseppe Conte, na pia kuhusu maandamano ya chama cha mrengo mkali wa kulia cha AfD huko mjini Berlin.

https://p.dw.com/p/2yRnX
Deutschland - Berlin Gegendemo zu AFD Demonstration
Picha: REUTERS

Die Welt

Kuhusu kujiuzulu kwa waziri mkuu mteule wa Italia Giuseppe Conte, baada ya rais Sergio Mattarella kupinga uteuzi wa waziri wa fedha. Gazeti hilo la Die Welt linasema jambo zuri ni kwamba rais Sergio Mattarella hakukubali kushinikizwa. Hata hivyo hatua ya Conte inaweza kuwa na maana ya kufanyika uchaguzi mwingine nchini Italia. Mhariri wa Die Welt anafafanua zaidi juu ya kujiuzulu kwa Giuseppe Conte ameandika, wengi miongoni mwa Wataliani hawakupendezewa na Serikali iliokuwa ikisubiriwa. lakini ni uhalali wa kidemokrasia.

Conte alijiuzulu baada ya mazungumzo ya kuunda serikali kugonga mwamba. Sababu ni kwamba kiongozi wa umoja wa vyama vya mrengo wa kulia alitaka mjumbe wake Paolo Savona awe waziri wa uchumi lakini rais Mattarella alipinga na hakukubali kushinikizwa. Paolo Savona ni mtu anayetambulika kuwa mkosoaji mkubwa wa Umoja wa Ulaya. Savona ni mjumbe wa kiongozi wa Umoja wa vyama vya mrengo wa kulia, The Northern League. Kiongozi wake Matteo Salvini anataka mvutano na Umoja wa Ulaya.

Waziri mkuu mteule wa Italia aliyejiuzulu Guiseppe Conte
Waziri mkuu mteule wa Italia aliyejiuzulu Guiseppe ContePicha: Reuters/A. Bianchi

 die tageszeitung

Mhariri wa gazeti la die tageszeitung anazungumzia juu ya maandamano yaliyofanywa mjini Berlin na chama cha mrengo mkali wa kulia kinachojiita chama mbadala cha (AfD). Mhariri wa gazeti hilo anasema maandamano hayo yalikuwa ni aibu kwa chama hicho na anafafanua kwa kusema vidokezo vya chama hicho cha kishabiki, vimefunikwa. Hayo yalianza kwa kusutwa kwa madai yake kwamba maanadamo yaliyofanyika yalikuwa ya umma. Hesabu zilionyesha kwamba watu walioandaa maandamo ya kuwapinga wafuasi wa chama hicho cha AfD walizidi kwa idadi mara nne.

Lüneburg

Gazeti la Lüneburg linasema Berlin siyo Dresden wala sio Weimer. Kutokana na chama cha AfD kuweza kuwahamasisha wafuasi wake 5000 tu kushiriki kwenye maandamano ya mjini Berlin huo ni ushuhuda wa kutosha kuwa chama hicho kimeambulia patupu hasa kutokana na kujigamba kwake kuwa mtetezi wa maslahi ya umma. Mhariri wa gazeti hilo la Lüneburg anaeleza kuwa idadi ya waandamanaji waliojitokeza kuwapinga mashabiki wa chama hicho walizidi kwa mara  nne. Huo ulikuwa ujumbe wa wazi kwa chama hicho kinachotumia hoja finyu kujijengea umaarufu. Chama hicho kinachojiita chama mbadala hakiwakilishi maslahi ya wengi. Mhariri anaeleza kuwa chama cha AFD kinaongozwa na wapiga mayoe wachache wanaotumia vidokezo vinavyowadanganya hata wao wenyewe.

Neue Osnabrücker

Kuhusu kura ya maoni yenye lengo la kuleta mageuzi katika sheria ya utoaji ujauzito nchini Ireland gazeti la Neue Osnabrücker linasema theluthi mbili ya watu walioshiriki katika kura hiyo ya maoni nchini Ireland wameunga mkono hoja ya kulegeza makali ya sheria juu ya utoaji ujauzito. Hatua hiyo ni ya ujasiri japo imechelewa kuchukuliwa katika nchi hiyo ya Kikatoliki. Sheria hiyo kwa mfano ilikuwa inawaadhibu hata wanawake waliobakwa.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Horst Seehofer
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Horst SeehoferPicha: picture-alliance/dpa/S. Hoppe

Märkische Oderzeitung

Nchini Ujerumani idara kuu ya uhamiaji na wakimbizi ya Ujerumani inasemekana kuwa ilitoa vibali vya uhamiaji zaidi ya 1000 kwa wakimbizi bila ya kuwepo ushahidi wa kutosha iwapo watu hao walistahiki kupewa vibali hivyo. Mhariri wa gazeti la Märkische Oderzeitung anasema waziri wa mambo ya ndani anapaswa kutoa maelezo.

Mhariri huyo anatilia maanani kwamba hazijapita hata siku 100 tangu kuingia madarakani, waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer tayari ameshaingia katika mgogoro mkubwa. Hata hivyo  kutokana na dhima yake kama mbariki wa serikali ya mseto, ni vigumu kutimuliwa au kujizulu lakini ikiwa hatapata suluhisho la haraka la kuisafisha idara hiyo kuu ya uhamiaji na wakimbizi, huenda chama chake cha CSU kikapata pigo kubwa katika uchaguzi wa jimbo lake la Bavaria la kusini mwa Ujerumani.

Mwandishi:Zainab Aziz

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman