1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Puigdemont ataka upinzani wa kidemokrasia dhidi ya Uhispania

Caro Robi
29 Oktoba 2017

Kiongozi wa jimbo la Catalonia Carles Puigdemont ameipinga hatua ya Serikali kuu ya Uhispania kumuondoa madarakani. Amehimiza kufanywa upinzani wa kidemokrasia dhidi ya utawala wa moja kwa moja kutoka Uhispania.

https://p.dw.com/p/2mgvk
Spanien Puigdemont in Girona
Picha: Reuters/R. Marchante

Puigdemont ameilaani serikali kuu kwa kuikandamiza ari ya Wacatalonia wanaotaka uhuru. Ameongeza kuwa hatua ya Serikali ya waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy kuondoa mamlaka ya ndani ya Catalonia, kwa mara ya kwanza tangu utawala wa kidikteta wa Francisco Franco kati ya mwaka 1939-1975 ni uchokozi.

Amesema upinzani wa kidemokrasia ndiyo njia pekee japo hakufafanua mkondo ambao njia hiyo itachukua. Katika taarifa aliyoitia saini kama Rais wa utawala wa Catalonia, Puigdemont amesema hatua zilizochukuliwa na Rajoy za kuvunja serikali, bunge, polisi ya jimbo hilo na kutwaa madaraka ni kinyume na mapenzi ya Wacatalonia.

Uhispania njia panda

Naibu waziri mkuu wa Uhispania Soraya de Santamaria ndiye ameteuliwa kulisimamia jimbo la Catalonia. Puigdemont ameapa kuendelea kufanya kazi kuhakikisha anajenga taifa huru akiwahimiza wafuasi wake kujibu hatua za serikali kuu kwa kutotumia ghasia, matusi na kwa njia za kuwajumuisha kila mmoja na pia kuheshimu maoni ya wanaopinga kujitenga kwa Catalonia.

Spanien | Soraya Saenz de Santamaria
Naibu waziri mkuu wa Uhispania Soraya Saenz de SantamariaPicha: Getty Images/P. Blazquez Dominguez

Waendesha mashitaka walitangaza Ijumaa kuwa watafungua mashitaka ya uasi dhidi ya Puigdemont wiki ijayo. Kiongozi huyo huenda akafungwa gerezani kwa miaka 30 iwapo atakutikana na hatia.

Uhispania inasalia katika njia panda huku ikikumbana na mzozo mbaya wa kikatiba katika historia yake, uliosababishwa na kura ya maonii ya kutaka kujitenga na kujitawala iliyopigwa Oktoba mosi ambayo imetajwa na mahakama ya kikatiba na serikali ya Uhispania kuwa haikuwa halali.

Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy alitangaza kuivunja serikali ya Catalonia pamoja na bunge lake na kuitisha uchaguzi kufanywa Disemba 21 kuwachagua viongozi wapya. Uhispania imesema Puigdemont anaruhusiwa kushiriki katika uchaguzi huo.

Maandamano yanatarajiwa Jumapili

Wanaounga mkono Uhispania kusalia kuwa taifa moja wanatarajiwa kukusanyika leo katika mji mkuu wa jimbo la Catalonia, Barcelona. Maandamano hayo ya kupinga utawala wa Catalonia yanaandaliwa chini ya kauli mbiu 'Catalonia ni sisi sote'.

Spanien Demo für die Einheit Spaniens in Madrid
Waandamanaji wanaopinga Catalonia kujitengaPicha: Reuters/S. Vera

Miongoni mwa watakaoshiriki maandamano hayo ni wawakilishi wa vyama vitatu vya upinzani vya Catalonia, kikiwemo chama cha kihafidhina kinachoongozwa na Rajoy. Maandamano hayo yanaonekana kuwa  mwanzo wa kampeini kuelekea uchaguzi wa Desemba 21.

Wabunge 70 wa Catalonia siku ya Ijumaa walipiga kura kuidhinisha uhuru wa kujitawala wa jimbo hilo tajiri lenye idadi ya watu milioni 7.5.

Wachambuzi wanaonya huenda wiki ijayo, mzozo huo wa kisiasa na kikatiba ukashuhudia wakati mgumu wakati wafanyakazi wa umma katika jimbo la Catalonia watakaporejea makazini na huenda wakakataa kuchukua maagizo kutoka kwa viongozi waliotumwa kutoka Madrid kuiongoza Catalonia kwa muda.

Mwandishi: Caro Robi/afp/ap

Mhariri: John Juma