1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin akubalika Italia

10 Juni 2015

Matteo Renzi amemkaribisha Vladimir Putin wa Urusi ingawa hakuonesha dalili za kuutibua uhusiano wake na washirika wake wa kimataifa kuhusiana na suala la vikwazo vya Umoja wa Ulaya ilivyowekewa serikali ya Urusi.

https://p.dw.com/p/1Feju
Putin na Renzi katika maonesho ya Expo 2015 mjini Milan
Putin na Renzi katika maonesho ya Expo 2015 mjini MilanPicha: Reuters/F. Lo Scalzo

((Waziri mkuu wa Italia Matteo Renzi amemkaribisha Rais Vladimir Putin wa Urusi ingawa waziri mkuu huyo hakuonesha dalili za kuutibua uhusiano wake na washirika wake wa kimataifa kuhusiana na suala la vikwazo vya Umoja wa Ulaya ilivyowekewa serikali ya Urusi.

Wiki mbili kabla ya Umoja wa Ulaya kutoa uamuzi wake ikiwa irefushe vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi kutokana na hatua yake ya kulinyakua jimbo la Crimea lililokuwa katika himaya ya Ukraine,waziri mkuu wa Italia Matteo Renzi ameusifu urafiki uliopo tangu jadi kati ya nchi yake na Urusi,lakini pia hakusita kuzungumza tofauti zilizopo kuhusiana na suala la mgogoro wa Ukraine.

Kauli ya Renzi imekuja baada ya mkutano wake na Putin uliofanyika kufuatia mapigano kati ya wanajeshi wa serikali ya Ukraine na waasi wanaoungwa mkono na Urusi katika upande wa Mashariki mwa Ukraine, kuzuka upya baada ya kushuhudiwa miezi kadhaa ya utulivu kiasi.

Urusi bado inakubalika kwa Italia kuliko ilivyo kwa nchi nyingine nyingi za Umoja wa Ulaya na ni kwasababu utawala huo wa mjini Moscow unaitazama Italia kama nchi pekee inayositasita kuunga mkono vikwazo vya Umoja huo dhidi ya Urusi na inaoongoza kupigia upatu mazungumzo na Moscow.Viongozi wote wawili Putin na Renzi wamesema suala la msingi la kuumaliza mgogoro wa Ukraine ni utekelezwa kamili wa makubaliano ya mjini Minsk ,ambayo kwa mujibu wa Renzi ni hatua pekee itakayomaliza mvutano, matatizo, mgawanyiko, vikwazo na kulipizana kisasi cha kuwekeana vikwazo.

Kwa upande wake Putina ambaye anazipinga tuhuma kwamba nchi yake ndiyo inayopaswa kubebeshwa dhamana kwa kuufadhili mgogoro wa Ukraine, ameinyooshea moja kwa moja kidole cha lawama serikali ya Ukraine ambayo Urusi inasema imehusika kuyachokoa mapigano ya hivi karibuni ili kuutia kishindo Umoja wa Ulaya uongeze vikwazo vyake dhidi ya Urusi.

Rais Putin akubaliwa nchini Italia
Rais Putin akubaliwa nchini ItaliaPicha: Reuters/A. Garofalo

Rais Putin amesema ni bahati mbaya kwamba makubaliano ya Minsk hayatekelezwi kikamilifu ila ni sehemu tu ya makubaliano hayo ndiyo inayotekelezwa kwa sasa. Pamoja na hayo waziri mkuu wa Italia Matteo Renzi ameonekana kuzidi kuchoma mwiba kwenye kidonda kwa kutangaza wazi kwamba anatarajia kuhudhuria na timu ya nchi yake michuano ya soka ya Kombe la dunia mwaka 2018 itakayochezwa UrusI; kauli ambayo inafuta kabisa uwezekano wa Italia kujihusisha katika hatua yoyote ya kususia michezo hiyo kutokana na kashfa za rushwa zilizolitikisa Shirikisho la Soka Duniani, FIFA.

Putin anategemewa kukaribishwa vizuri atakapokutana na kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, huko Vatican ambaye nyuma ya pazia amebeba dhima kubwa katika mazungumzo juu ya dola la Palestina pamoja na uhusiano kati ya Marekani na Cuba. Tayari Marekani imeshamtolea mwito kiongozi huyo wa kidini mwenye ushawishi, kuikosoa Urusi kwa kujiingiza kimabavu zaidi katika mgogoro wa Ukraine.

Mwandishi: Saumu Mwasimba RTRE/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef