1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin apata ushindi mkubwa

3 Desemba 2007

Matokeo ya awali katika uchaguzi wa bunge nchini Urusi, yanaonesha kuwa Chama cha Rais Vladmir Putin kimepata ushindi wa takriban asilimia 63.

https://p.dw.com/p/CVtI
Rais Putin na mkewe katika mgahawa mmoja jijini Mosko jana JumapiliPicha: AP

Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi wakati karibu nusu ya kura zote zikiwa zimehasabiwa chama hicho cha United Russia Party kinaongoza huku chama cha kikoministi kikamata nafasi ya pili kwa asilimia 11.5.

Hata hivyo kumekuwa na shutuma kuwa uchaguzi huo wa kuwania viti vya 450 vya bunge la nchi hiyo, hakuwa huru na haki.

Hapo jana Kansela Angela Merkel wa Ujerumani aliishutumu serikali ya Putin kwa kuvikandamiza vyama vya upinzani.

Pia alielezea kusikitishwa kwake na kutokuwepo kwa waangalizi kutoka shirika la usalama na ushirikiano barani Ulaya katika uchaguzi huo.

Hata hivyo Kansela Merkel alisisitiza kuwa ni muhimu kudumisha uhusiano na Urusi kwani nchi hiyo ina mchango muhimu katika suala la mzozo wa mpango wa nuklia wa Iran na majaaliwa ya jimbo la Serbia la Kosovo.

Wadadisi wanasema kuwa ushindi wa Putin katika uchaguzi huo utamuweka kiongozi huyo katika ushawishi mkubwa wakisiasa mwakani wakati atakapong´atuka urais kama katiba inavyomtaka.