1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin asikitishwa na vikwazo vya Marekani

Oumilkheir Hamidou
15 Juni 2017

Rais wa Urusi Vladimir Putin anasema vikwazo vya nchi za Magharibi vimepelekea shughuli za uchumi nchini mwake kuimarika badala ya kudorora. Amesema hayo kwenye mahojiano ya televisheni.

https://p.dw.com/p/2elkV
Russsland Bürgersprechstunde mit Wladimir Putin
Picha: Reuters/Sputnik/A.Druzhinin/Kremlin

Rais Putin ametoa matamshi hayo katika mahojiano ya moja kwa moja kwa njia ya televisheni ambapo huwa anajibu maswali ya wananchi. Akizungumza katika kipindi hicho cha moja kwa moja cha televisheni ambapo kila raia wa Urusi anaruhusiwa kumuuliza maswali, rais Vladimir Putin ameelezea masikitiko yake kutokana na uamuzi wa baraza la Seneti la Marekani la kurefusha vikwazo, ambavyo anasema ni sehemu ya juhudi za nchi za magharibi za "kuibana" nchi yake. Hata hivyo amesisitiza hatua hizo zimezidi kuipa nguvu nchi yake.

Baraza la Seneti la Marekani limepitisha orodha ndefu ya vikwazo kwa lengo la "kuiadhibu Urusi kwa kuingilia kati katika uchaguzi wa mwaka jana. Vikwazo hivyo vimelengwa sekta ya uchumi na baadhi ya waliohusika na visa vya udukuzi wa mtandao. Vikwazo hivyo vinafuatia vikwazo kadhaa vyengine viliyowekwa na Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya baada ya Urusi kuidhibiti rasi ya Crimea na kuamua kuwaunga mkono waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine.

Putin anasema vikwazo vyote hivyo ni ushahidi jinsi nchi za magharibi zinavyotaka kuibana Urusi na vinatoa pia sura ya mivutano ya ndani nchini Marekani. "Ni ushahidi wa kuendelea mapambano ya ndani nchini Marekani" anasema.

Russland Putin Fragestunde
Baadhi ya walioshiriki mahojiano na Rais Putin Picha: Reuters/RIA Novosti/Kremlin/M. Klimentyev

Asema vikwazo vimeipatia nguvu Urusi.

"Vikwazo hivyo vimeipatia nguvu Urusi ya kujitegemea yenyewe katika kusafirisha mafuta na gesi na  kutumia vipaji na ubunifu wao ili kuimarisha shughuli za viwandani.

Urusi imejibu vikwazo vya Marekani na Umoja wa Ulaya kwa kusitisha bidhaa nyingi za chakula kutoka nchi za magharibi - hatua iliyosaidia kuinua shughuli za kilimo nchini Urusi. Wakulima wa Urusi wameisihi Kremlin marufuku ya kuagizia chakula kutoka nje yaendelezwe hata kama nchi za magharibi zitabatilisha vikwazo, lakini rais Putin amesema "ikiwa washirika wataondowa vikwazo, na wao watafanya hivyo hivyo."

Rais Putin anakiri kwamba mapato ya wananchi yameporomoka na kwamba asilimia 13.5 ya warusi wanaishi katika hali ya dhiki, chini ya dola 170 kwa mwezi.

Masuala mengi aliyoulizwa katika kipindi hicho cha televisheni cha mchujo, yalihusu mishahara duni, nyumba zilizochakaa, kuporomoka huduma za afya na matatizo mengine yanayohusiana na huduma za jamii.

Kama ilivyokuwa katika vipindi kama hicho siku za nyuma, rais Putin amewakaripia maafisa wa taasisi husika kwa kushindwa kuwapatia huduma zinazofaa wananchi na kuwaamuru wairekebishe haraka hali hiyo.

Akiulizwa kuhusu binti zake 2 ambao hawakuonekana kwa muda mrefu hadharani, rais Putin amesema wote wawili wanaishi Moscow na kufanya kazi katika sekta ya sayansi na elimu. Amesema hapendi kuzungumzia kuhusu mambo ya faragha ya familia yake.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP

Mhariri:Josephat Charo