1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin kubaki madarakani milele?

Sekione Kitojo
11 Machi 2020

Katika kumbukumbu ya kunyakuliwa jimbo la Crimea rais wa Urusi Vladimir Putin ameanzisha mchakato wa mabadiliko makubwa ya katiba, ambayo yanampa nafasi ya kuendelea kubakia madarakani.

https://p.dw.com/p/3ZCSQ
Russland, Moskau: Präsident Wladimir Putin spricht im Unterhaus zur Änderung der Verfassungsreform
rais Vladimir Putin akilihutubia bungePicha: Reuters/E. Novozhenina

Bunge  la  nchi  hiyo linatarajiwa  leo  kuidhinisha mapendekezo  kadhaa  ya mabadiliko, ikiwa  ni  pamoja  na kumuwezesha  rais Putin  kugombea muhula mwingine  madarakani. 

Russland Moskau Präsident Putin im Parlament
Rais Putin wa UrusiPicha: Reuters/Sputnik/Kremlin/A. Nikolsky

Vladimir Putin alijitokeza katika  bunge  la  Urusi  jana Jumanne , wakati baraza  hilo  la wawakilishi  likijadili  mabadiliko hayo ya  katiba. Katikati  ya mwezi  Januari  Putin  alianzisha kwa  mshangao  wa  wengi mchakato  huo wa  mabadiliko  ya katiba. Kutakuwa  na  mabadiliko mengi  katika  katiba  ya  nchi hiyo, kwa mfano  mshahara wa kima cha  chini.

Lakini   kuhusu  suala  muhimu katika  siasa  za  Urusi, ni  vipi Urusi itaweza kujiendesha  baada ya  mwaka  2024, wakati  muhula wa  Putin  madarakani utakapomalizika  rasmi, kwa mpango  huo  hakuna  jibu  hadi sasa.

Kiongozi wa muda mrefu

Putin, mwenye  umri  wa  miaka 67, amekuwa  madarakani  kama rais  na   baadaye waziri  mkuu kwa  miongo  miwili. Ni  kiongozi aliyeongoza  kwa  muda  mrefu zaidi  nchini  Urusi  ama  kiongozi wa  Kisovieti  tangu  Joseph Stalin.

Russland Moskau Präsident Putin im Parlament
Bunge la Urusi ambalo litajadili na kuidhinisha mabadiliko ya katibaPicha: Reuters/Sputnik/Kremlin/A. Nikolsky

Katiba  ya  nchi  hiyo  katika hali  yake  ya  sasa  inaruhusu rais  kutumikia kwa  mihula miwili  mfululizo, ikiwa  na maana  kwamba  Putin ataondoka madarakani  kama  rais  katika muda  wa  miaka  minne  ijayo. Putin  alitumikia  vipindi  viwili vya  miaka  minne  kama  rais kuanzia  mwaka  2000  hadi 2008. Baada  ya  katiba kufanyiwa  mabadiliko  kutoa ruhusa  ya  mihula  ya  miaka sita, na  Putin  alirudi  kuwa rais  mwaka  2012 na  alichaguliwa tena  mwaka  2018.

Baraza la wawakilishi

Baraza  la  wawakilishi  la  bunge la  Urusi Duma linadhibitiwa  na chama  cha  siasa  ambacho kiko karibu  zaidi  na  Putin, United Russia, ambacho  kwa wingi mkubwa kinaunga  mkono mswada  mpya  wa mabadiliko. Baada  ya  kupitishwa katika  baraza  la  wawakilishi, mswada  huo  unatarajiwa kuidhinishwa  na  baraza  la juu, seneti siku  ya  Jumamosi, na kisha  utapelekwa  katika mahakama  ya  katiba.

Krim Stadt Kertsch
Sehemu ya bandari ya Krasilnikov katika jimbo la Crimea ambalo limenyakuliwa na UrusiPicha: picture-alliance/dpa/Tass/S. Krasilnikov

Putin angependa  kutia  saini kuwa  sheria  mswada  huo hapo Machi 18, katika  kumbukumbu ya  kuchukuliwa  jimbo  la Ukraine  la  Crimea  na  kuingizwa katika  himaya  ya  Urusi.

Putin  amesisitiza  kwamba mabadiliko  hayo  yaidhinishwe kupitia  kura  ya  maoni  nchi nzima  hapo  Aprili 22  ili  kuanza kazi. Mabadiliko  hayo  ni pamoja  na  kuweka  kima  cha chini  cha  mshahara  na  fungu la mafao ya  uzeeni kwa  msingi wa gharama  za  maisha, kipengee ambacho  kinaweza  kusaidia wananchi  kupiga  kura kuidhinisha  mabadiliko  hayo.