1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin na Wakimbizi Magazetini

3 Septemba 2014

Siasa ya rais Vladimir Putin kuelekea Ukraine ,sera za Umoja wa Ulaya kuelekea wakimbizi na uchumi wa Ujerumani ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/1D5ki
Rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Joachim GauckPicha: picture-alliance/dpa

Tuanzie na Ukraine ambako rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Joachim Gauck hafichi msimamo wake dhidi ya sera za Urusi.Gazeti la "Rhein-Necker-Zeitung" linaandika:"Yazidi kudhihirika kwamba rais Gauck anafuata ajenda ya kisiasa inayoitaka Ujerumani iwajibike zaidi kimataifa.Upande huo anaonyesha anashirikiana bega kwa bega na serikali kuu ya Ujerumani inayomuachia rais kuwafungulia njia.Kwamba kansela Merkel anajiweka nyuma,na kumuachia rais Gauck atangulie mbele ni sawa na kubadilisha majukumu ya kisiasa na kwa namna hiyo kumfanya rais wa shirikisho akiuke mipaka ya madaraka yake."

Gazeti la "Der neue Tag" linazungumzia msimamo wa rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Joachim Gauck kuelekea siasa ya rais wa Urusi Vladimir Putin katika mzozo wa Ukraine.Gazeti hilo linaandika:"Hata suluhu ina mipaka:Ilikuwa hivyo katika mauwaji ya halaiki ya Rwanda ambako nchi za magharibi zilishindwa.Na imedhihirika katika visa vya kinyama vinavyofanywa na magaidi wa kundi la dola ya kiislam.Ni sawa kwamba rais Gauck anazungumzia kinaga ubaga uchokozi wa Putin.Lakini pia ni sawa kuendelea kuzungumza na kiongozi wa ikulu ya Urusi Kremlin.Putin ana mengi bado ya kupoteza.Na dubu wa Urusi anakuwa hatari zaidi anapojikuta amebanwa."

Italia yazongwa na wakimbizi

Sera za Umoja wa Ulaya kuelekea wakimbizi zinakosolewa.Gazeti la "Eisenacher Presse" linaandika:"Muongozo wa Umoja wa ulaya kuhusu wakimbizi haufai wakati wa migogoro.Mwenye kulinda mipaka ya nje ndie anaewajibika.Katika wakati wa kawaida hilo linavumilika..Lakini pale maelfu wanapomiminika ,nchi kama Italia hujikuta ikizidiwa.Inajikuta imeachwa peke yake.Na ikiwa misaada haitowafikia wanayoihitaji,basi wenye kuhitaji ndio watakaoifuatia kule kule iliko:kwa maneno mengine:katika eneo la neema la kaskazini.Wanawaachia wende wanakotaka.Kwa hivyo ni jambo linaloeweka waziri wa mambo ya ndani Thomas de Maizière anapoonekana anachoka kuvumilia.

Mittelmeer-Flüchtlinge/ Italien/
Wakimbizi wanaoingia Italia kupitia bahari ya katiPicha: picture alliance/ROPI

Uchumi wa Ujerumani wanawiri

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na hali ya kiuchumi nchini Ujerumani.Gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung" linaandika:"Ujerumani inaendelea vizuri.Uchumi wake unanawiri.Fedha za walipa kodi zinamiminika.Ni hali ya kutia moyo japo kama ni ya muda.Tusisahau lakini kwamba kuna mengi yanayohitaji kutendwa tena haraka nchini Ujerumani .Ndio maana litakuwa jambo la maana kama kansela Angela Merkel atazungumza mara kwa mara na wawakilishi wa wafanyakazi na waajiri kuwaelezea kinachostahiki kufanyika ili uchumi uendelee kunawiiri.Miundo mbinu ndio inayokamata nafasi ya mbele.Dhahir pia ni kwamba serikali inalazimika kuwekeza zaidi ili kulinda masilahi yake na wakati huo huo kutoa msukumo kwa ukuaji wa kiuchumi katika Umoja wa Ulaya.

Container stehen am 17.10.2012 in Hamburg
Makontena katika bandari ya kimataifa Picha: picture-alliance/dpa

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Iddi Ssessanga