1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rafael Nadal anyakua taji la tisa la French Open

9 Juni 2014

Rafael Nadal anaamini kuwa ushindi wake wa taji la tisa katika mashindano ya mchezo wa Tennis ya French Open, ulikuwa hatua ya kulipiza kisasi kichapo alichopata mapema mwaka huu.

https://p.dw.com/p/1CEyr
Tennis Herren-Finale Rafael Nadal
Picha: picture alliance/dpa

Mhispania huyo mwenye umri wa miaka 28 alitwaa taji lake kuu la Grand Slam katika miaka 14 ya kazi yake na la tano mfululizo, kwa kumpiku hasimu wake Novak Djokovic katika fainali ya French Open uwanjani Roland Garros mjini Paris. Nadal alishinda kwa seti za 3-6, 7-5, 6-2, 6-4. Lilikuwa ni pambano la 42 ambalo magwiji hao wawili wamewahi kukutana.

Nadal anayeorodheshwa nambari moja ulimwenguni, ambaye rekodi ya ushindi wake katika uwanja wa Roland Garros ni 66 dhidi ya kichapo kimoja pekee, pia ana mataji 14, sawa na Pete Sampras na matatu nyuma ya mshikilizi wa rekodi bora zaidi Roger Federer.

Lakini mhispania huyo aliingia uwanjani akiwa na mawazo ya kichapo alichopata kutoka kwa Stan Wawrinka katika fainali ya Australian Open mjini Melbourne mwezi wa Januari mwaka huu ambapo alihitaji matibabu ya kina kutokana na jeraha la mgongo wake. Nadal alikuwa mwepesi kumsifu Djokovic ambaye alikuwa akilenga kupata taji lake kuu la saba na ushindi wa kwanza katika uwanja wa Roland Garros.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman