1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wapiga kura

Mjahida30 Desemba 2015

Raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wamepiga kura leo Jumatano wakiwa na matumaini kuwa uchaguzi huo wa rais na bunge, utasaidia kumaliza miaka kadhaa ya msukosuko wa kisiasa na kidini uliosababisha maelfu ya watu kuuwawa.

https://p.dw.com/p/1HWFf
Afrika Wahlen in Zentralafrika
Raia washiriki uchaguzi wa rais na bungePicha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Watu wanaokadiriwa kufikia milioni mbili wana haki ya kupiga kura katika uchaguzi huo uliyocheleweshwa kwa siku tatu, kufuatia vifaa vya kupigia kura kutofika kwa wakati uliyotarajiwa.

Katika uchaguzi uliyoanza leo vituo vya kupigia kura vilifunguliwa kuchelewa na wapiga kura walilalamikia ukosefu wa masunduku ya kutosha ya kupigia kura na baadhi ya vituo kuwekwa katika maeneo yalioonekana kuwa sio salama.

Baadhi ya watu ambao walikuwa hawajapokea kadi zao za kupigia kura, waliruhusiwa kushiriki uchaguzi kwa kutumia stakabadhi zao za usajili. Hata hivyo katika kituo kimoja cha kupigia kura mjini Bangui raia wa tatu wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo wamekamatwa wakijaribu kupiga kura wakitumia kadi za watu wengine.

Mkaazi wa Bangui Ndaba Suleyman alisema yuko tayari kusimama kwa muda wowote ule, ili mradi ashiriki katika zoezi la uchaguzi kwa nia ya kumaliza mvutano nchini humo kati ya makundi ya waasi ya kiislamu na kikristo.

Afrika Wahlen in Zentralafrika
Baadhi ya raia washiriki zoezi la uchaguziPicha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Uchaguzi huo umefanyika kwa uangalizi wa wanajeshi 11,000 wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, baada ya vurugu kutokea katika kura ya maoni iliyofanyika mapema mwezi huu wa Desemba.

Wagombea wanaoonekana kuwa na nafasi ya kuchukua ushindi miongoni mwa wagombea 30 wanaokipigania kiti hicho cha urais ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani Martin Ziguele, anayeungwa mkono na waasi wa kikristo wa anti balaka, Waziri wa zamani na kiongozi wa waislamu Karim Meckassoua na Mtaalamu wa fedha na Waziri Mkuu wa zamani Anicet-Georges Dologuele.

Katiba haiwaruhusu viongozi wa serikali ya mpito kugombea katika uchaguzi

Rais wa mpito Catherine Samba-Panza hakugombea kwasababu katiba mpya hairuhusu viongozi wa serikali ya mpito kugombea. Tangu Januari mwaka wa 2014 Samba-Panza ameiongoza serikali ya mpito iliyokuwa na jukumu la kurejesha amani nchini humo.

Catherine Samba-Panza Zentralafrikanische Republik 20.01.2014 Bangui
Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba PanzaPicha: Eric Feferberg/AFP/Getty Images

"Watu wengi walidhani hii siku isingefika kufuatia ukosefu wa usalama, na sababu nyengine za maandalizi ya uchaguzi, lakini kama unavyoona tunapiga kura kwa amani, nna fahari kubwa," alisema Panza baada ya kupiga kura yake mjini Bangui.

Huku hayo yakiarifiwa robo ya idadi ya raia wa Jamhuri ya Afrika ya kati ya milioni 4.7- wamepoteza makaazi yao tangu mwezi Machi mwaa wa 2013 wakati waasi wa Kiislamu wa Seleka walipompindua rais mkristo Francois Bozize. Maelfu wameuwawa kufuatia mapigano ya kidini.

Serikali mpya itakayochaguliwa itakuwa na jukumu la kuwapokonya silaha makundi ya waasi yaliojihami, kuiunganisha nchi na kuujenga upya uchumi wa nchi hiyo.

Matokeo ya uchaguzi yanatarajiwa kutolewa ndani ya wiki mbili zijazo, iwapo hapatakuwa na mgombea atakayeshinda kwa wingi wa kura duru ya pili ya uchaguzi itafanyika tarehe 31 mwezi wa Januari.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa

Mhariri: Iddi Ssessanga